NA DIRAMAKINI
KAMATI iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ili kutathimini utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeanza kazi rasmi kwa kukutana na Waziri wa wizara hiyo,Mheshimiwa Dkt. Stergomena L. Tax jijini Dodoma.
Mheshimiwa Dkt. Tax (katikati mstari wa kwanza) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Kutathmini utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Simba (wa pili kushoto mstari wa kwanza), Wajumbe wa Kamati pamoja na Sekretarieti ya Kamati hiyo. (Picha na Wizara ya Mambo ya Nje).
Wakati wa kikao hicho cha Aprili 18, 2023 jijini humo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Tax amewapongeza wajumbe wa kamati hiyo kwa kuaminiwa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia na amewaahidi wizara itatoa ushirikiano unaohitajika ili kamati hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
"Hii ni kamati muhimu sana na ni matumaini ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kuwa, mtafanya kazi nzuri itakayoleta mapendekezo yatakayoboresha utendaji wa wizara ili kukidhi malengo ya Serikali ya kukuza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa Kimataifa,"Mheshimiwa Dkt.Tax amewaeleza wajumbe wa kamati hiyo.
Waziri Mhe.Dkt.Tax amesema, wajumbe wa kamati hiyo takribani wote ni wenyeji wa Wizara ya Mambo ya Ndani na wabobevu katika masuala ya diplomasia, hivyo ana uhakika kwa muda waliopewa na hadidu za rejea walizopewa, watafanya kazi itakayokidhi matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.
Mhe. Dkt. Tax (katikati mstari wa kwanza) akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Kamati Kutathmini utendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Simba (wa pili kushoto mstari wa kwanza) pamoja na Wajumbe wa Kamati hiyo.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe saba ambao ni mabalozi wastaafu akiwemo Mheshimiwa Hassan Simba Yahya (Mwenyekiti), Mhe.Ramadhani Muombwa Mwinyi (Mjumbe), Mhe.Mwanaidi Sinare Maajar (Mjumbe), Mhe.Peter Allan Kallaghe (Mjumbe), Mhe.Tuvako Nathaniel Manongi (Mjumbe), Mhe.Jack Mugendi Zoka (Mjumbe) na Mhe.George Kahema Madafa (Mjumbe).
Hata hivyo, kamati hiyo iliundwa Machi 23, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.