Kamishna Jenerali Lyimo atangaza vita mpya dhidi ya dawa za kulevya nchini,kuanzia na vijiwe vyote

NA GODFREY NNKO

KAMISHINA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Aretas James Lyimo ametaja malengo yake ambayo ameingia nayo ili kuhakikisha mamlaka hiyo inadhibiti kabisa biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ameyasema hayo leo Aprili Mosi, 2023 mkoani Mtwara wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa ambapo mamlaka hiyo inashiriki kikamilifu katika mbio za mwenge huku akiweka wazi mipango yake ya kuhakikisha wanakabiliana na changamoto hiyo.

"Mimi kama Kamishna mpya wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, malengo yangu ambayo nimeingia nayo ni kuhakikisha tunadhibiti kabisa usambaaji wa dawa za kulevya, lakini pia kuhakikisha kwamba tudhibiti na kupambana na uingizaji wa dawa za kulevya nchini.

"Kwa hiyo nitoe wito kwa watumiaji wa dawa za kulevya kuacha wenyewe kutumia dawa za kulevya, lakini pia kwa wale wauzaji na wasambazaji wa dawa za kulevya kuacha kabisa hiyo biashara ya dawa za kulevya, kwani kuanzia sasa tunafanya operesheni kabambe nchi nzima, lakini tutahakikisha vijiwe vyote vya wauzaji, na watumiaji wa dawa za kulevya tunavisambaratisha,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Pia amefafanua kuwa, "Na tutafanya opereheni kabambe nchi nzima na tutakamata wote wanaofanya biashara ya dawa za kulevya. Lakini pia tutafanya operesheni kila kijiji, mikoa yote kuhakikisha kwamba wale wote ambao wanalima bangi na mirungi tutahakikisha kwamba tunawakamata na kuteketeza mashamba yao, kwa hiyo nitoe wito kwa jamii nzima, mashirika ya dini, na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba tunatoa taarifa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuweza kufanikisha operesheni mbalimbali tutakazofanya nchini kudhibiti dawa za kulevya.

"Kwa hiyo, niiombe jamii na nitoe wito kwao kutambua kuwa,ushirikiano wao utaiwezesha hii nchi ikuwa salama bila ya dawa za kulevya, kwani dawa za kulevya zina madhara makubwa sana, yanapoteza nguvu kazi ya taifa. Kwa hiyo tukisaidiana wote kama jamii, tutahakikisha kwamba tunadhibiti dawa za kulevya nchini.

"Lakini cha kwanza tutakachoanza nacho ni kudhibiti vijiwe vyote vya dawa za kulevya nchini,Lengo tunapunguza uhitaji wa dawa za kulevya, lakini pia tutapambana sambamba na wale wote waletaji wa dawa za kulevya kutoka nje ya nchi, nje ya mipaka na ndani ya Tanzania, lakini pia tutaimarisha ushirikiano wa Tanzania, kikada pamoja na Kimataifa kuhakikisha kwamba tunadhibiti dawa za kulevya nchini,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Mbio za Mwenge kitaifa kwa mwaka 2023 katika uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara leo Aprili Mosi , 2023 zimezinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

Aidha,Kamishana Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),Aretas James Lyimo amesema, ushiriki wao katika mbio hizo una umuhimu mkubwa.

"Tupo hapa Mtwara katika tukio hili la uwashaji wa Mwenge, kwa sababu Mwenge unatembea nchi nzima kwa ajili ya kukemea maovu, kuhakikisha kwamba, maovu yanaondoka kwenye jamii nchini, na sisi kama Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya,dawa za kulevya ni sehemu moja wapo ya maovu ambayo yanakemewa na Mwenge.

"Kwa hiyo sisi ni sehemu ya Mwenge, na tuko hapa kwa ajili ya kuitaka jamii kuhakikisha inaachana na matumzi ya dawa za kulevya, inaachana na biashara ya dawa za kulevya,na mwisho wa siku katika mikakati yetu ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama bila dawa za kulevya.

"Na kuhakikisha Tanzania nzima, watu wote na wananchi wote tutahakikisha kwamba hakuna matumizi ya dawa za kulevya. Na ndiyo dira na ndiyo lengo letu na ndiyo mapambano yetu dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya,"amefafanua Kamishna Jenerali huyo.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya. Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news