Kamishna wa Elimu atoa maagizo vitendo vya ukatili shuleni

NA FRED KIBANO

SERIKALI imewataka Maafisa Elimu wa mikoa na halmashauri nchini kufuatilia vitendo vya ukatili vinavyofanywa mashuleni ili kuboresha mazingira salama, rafiki na wezeshi kwa watoto.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo Aprili 3, 2023 jijini Mwanza na Dkt. Lyabwene Mtahaba, Kamishna wa Elimu wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri Tanzania Bara (REDEOA) ambaye amemwakilisha Prof. Adolf Mkenda Waziri wa Elimu, Sayani na Teknolojia.

Dkt. Mtahabwa amesema Sekta ya Elimu inakabiliwa na changamoto ya mmomonyoko wa maadili, uwajibikaji hafifu na ukatili kwa watoto ambapo tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 60 ya ukatili unatokea nyumbani na asilimia 40 unatokea shuleni.

“zipo baadhi ya changamoto zinazoweza kuathiri juhudi za Serikali katika kutoa Elimu Bora kama vile kumomonyoka kwa maadili kwa baadhi ya jamii, vitendo vya ukatili kwa watoto nje na ndani ya shule, uwajibikaji hafifu kwa baadhi ya watumishi katika Sekta ya Elimu,” amesema Dkt. Mtahabwa.

Dkt. Mtahabwa amesema watoto hawapati haki ya kupata likizo, hawapewi kazi za mikono ili waweze kujitegemea ambapo na hivyo amewataka Viongozi hao kusimamia ushirikiano wa jamii na shule ili kuleta mabadiliko ya elimu kote nchini.

Akitoa neno la ukaribisho kwa Mgeni rasmi, Dkt. Charles Msonde Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais TAMISEMI amesema baadhi ya shule zimekuwa na changamoto ya kukosa wanafunzi wanaojiunga na darasa la tano lakini pia kuwepo kwa wanafunzi asilimia 71 waliojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 kukosa umahiri wa somo la kiingereza hali iliyopelekea kuandaa Mkakati Maalum wa kufundishia wenye vigezo 22 ikiwa ni pamoja na kuimarisha Ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa darasa la kwanza na pia kuimarisha ufundishaji wa darasa la tatu.

Naye Mwenyekiti wa REDEOA, Bi. Germana Mng’ao ameishukuru Serikali kwa kupeleka Miradi ya kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ya BOOST (Shule za Msingi) na SEQUIP (Sekondari), kuwajengea uwezo walimu wa Sekondari zaidi ya 13,000 na kuwapatia walimu vishikwambi nchi nzima kuimarisha ufundishaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news