NA DIRAMAKINI
MGAO wa Usawa wa Kaunti nchini Kenya umeongezeka kwa shilingi bilioni 15.4 za Kenya. Hii inamaanisha kuwa kaunti zitapokea shilingi 385.4 Bilioni katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ikilinganishwa na shilingi 370 Bilioni za sasa.
Kiwango hicho kipya ni sawa na asilimia 23 ya hesabu za mapato kwa mwaka wa fedha 2019/2020 zilizokaguliwa hivi karibuni na zilizoidhinishwa na Bunge.
Hatua hiyo inafuatia kupitishwa kwa Mswada wa Mgawanyo wa Mapato (Mswada wa Bunge la Kitaifa Na. 9 wa 2023) na Rais William Ruto.
Ili kuleta usawa wa maendeleo nchini, Hazina ya Usawazishaji ilitengewa shilingi 8.3 Bilioni.Hii ni ongezeko la shilingi 1.2 Bilioni kutoka mgawo wa mwaka huu wa fedha wa shilingi 7.1 Bilioni.
Katika maendeleo hayo mapya, vitengo vilivyogatuliwa pia vitatengewa shilingi 11.1 Bilioni kama mgao wa ziada kutoka kwa sehemu ya mapato ya Serikali ya Kitaifa.
Aidha, watapokea shilingi 33.2 Bilioni kama mgao wa ziada kutoka kwa mapato ya mikopo na ruzuku. Muswada huo uliosainiwa Alhamisi hii katika Ikulu ya Nairobi unatoa njia ya maandalizi ya makadirio ya matumizi ya kila mwaka kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.