'Lowassa' awaita Watanzania kuchangia damu mwezi ujao

NA DIRAMAKINI

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Charles Sabinian (maarufu Lowassa) amesema, mwezi ujao wa Mei, 2023 anatarajia kuratibu tukio kubwa la kukusanya damu kwa ajili ya kusaidia wanaopata changamoto ya damu nchini.
Tukio hilo linatarajiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo hususani katika Kata ya Makurumla, Dar es Salaam.

Lowassa ameyasema hayo wakati akizungumzia kuhusiana na maandalizi ya tukio hilo ambalo amefafanua kuwa, linatarajiwa kuwa na tija kubwa, kwani kiasi chochote cha damu itakayopatikana itasaidia kuokoa maisha ya watu wengi wenye uhitaji.

"Mungu akitujalia afya na uzima tunatarajia tukio hilo litakuwa na tija zaidi na damu ya kutosha itapatikana kwa ajili ya kusaidia ndugu zetu ambao wanapata changamoto ya damu ndani na nje ya Dar es Salaam.

"Tukio hilo litafanyikia Makurumla katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam na tayari nimeshatoa hamasa kwa vijana mbalimbali wa bodaboda, wanawake pamoja na vijana wanasiasa. Ninatarajia tutapata matokeo mazuri kupitia zoezi hilo muhimu,"amefafanua Lowassa.

Lowassa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Vijana katika Taasisi ya Tanzania Peace Foundation (TPC) amesema ni wajibu wa kila mmoja ndani ya jamii kufahamu kuwa, kuchangia damu ni jambo jema na la heri.

Pia wanapaswa kutambua umuhimu wa kushiriki zoezi hilo ili kusaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya damu kwa dharura ikiwemo kina mama wajawazito na watoto, vijana licha ya kuwa zoezi hilo ni la hiari nchini.

"Ndugu zangu Watanzania, licha ya kuwa uchangiaji wa damu ni jambo la hiari, lakini kuna umuhimu mkubwa wa kila mtu kutambua wajibu wake wa kuchangia damu, kutokana na uhitaji mkubwa wa damu kwa wagonjwa wa dharura katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya maeneo yetu, halmashauri, manispaa, mikoa na Taifa.

"Na kila mmoja wetu anapaswa kujua kuwa, muda wowote yeye ni muhitaji wa damu kwa dharura, hivyo tuna wajibu wa kujitolea kuchangia damu, ili kuwa na damu ya kutosha katika benki za damu, ndiyo maana nimeamua kuja na hamasa hii muhimu kwa ajili ya jamii na Taifa letu,"amefafanua Lowassa.

Amesema, wao kama wanasiasa na Watanzania ni jukumu lao kuhamasisha watu kujitoa kuchangia damu kwani hakuna kiwanda kinachoweza kutengezeza damu ya kumuongezea binadamu, bali ni binadamu pekee ndio wenye uwezo wa kuokoa maisha ya wagonjwa kwa kuchangia damu popote pale nchini.
Wakati huo huo, Lowassa ameendelea kuwaasa vijana kuvaa jukumu la kuwajibika kama vijana hasa katika kushiriki mikutano mbalimbali ya serikali ili kuwa na nafasi ya kushirikishwa katika mipango na mikakati mbalimbali.

Amesema, kupitia mikutano na shughuli mbalimbali za kijamii na Kitaifa ni eneo muhimu kwa vijana kumegeana fursa za kuziendea ndoto na malengo yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news