NA WAKILI BASHIR YAKUB
+255714047241
1. Kama atakuwa kwenye ndoa na mtu mwingine ambaye sio baba yako basi ikitokea wakaachana mali zako zitagawiwa. Baba yako wa kambo atachukua mali zako.
2. Kama akifa, ndugu zako watataka wagawane hizo mali katika mirathi sababu ni za mama yao. Upate tu bahati wakuelewe na wakurudishie hizo mali, vinginevyo huwezi kukwepa kuziingiza kwenye mirathi ili ndugu wazichukue. Na hapa hata ukipata ndugu mmoja mkorofi tu basi mali zako zinachukuliwa.
3. Mama akiumwa akawa hajitambui au hana nguvu huwezi kutumia hizo mali kwasababu hawezi kusaini. Kama ni fedha benki, kununua, au kuuza kitu haiwezekani sababu mmiliki hayupo.
4. Kesi au hatia yoyote inayoweza kutokea kwenye hizo mali itaenda kwa mama yako. Anaweza kushitakiwa na kwenda jela kama kuna tatizo lilitokana na hizo mali. Mfano gari/nyumba imehusika kwenye uhalifu, matatizo ya kikodi, uhujumu uchumi nk.
5. Jambo lolote la kisheria likitokea juu ya hizo mali wewe kama wewe huwezi kuchukua hatua sababu huna mamlaka(Locus). Huwezi kushitaki, huwezi kulalamika, nk. Mama mmiliki ndo anaweza kufanya hivyo.
6. Utapata ugumu kwenye kuzitumia, mfano ni nyumba unataka kuchukua mkopo, wewe kama wewe huwezi kuweka rehani mpaka mama akuombee. Hii ni kwa kila kitu/kila muamala unaotaka kufanya lazima mama afike kusaini. Itakutesa sana.
7. Mama atakuwa hana maelezo amepata vipi hizo mali, anafanya biashara gani. Kwa hili ipo siku anaweza kuingia kwenye mgogoro na mamlaka TAKUKURU nk. Habari ya nimeandikwa jina tu hapa haina nafasi sababu sheria iko wazi kuwa aliyeandikwa ndiye mmiliki kamili(Registration Conclusive Proof of Ownership).
8. Pia mama mwenyewe kama sio muaminifu anaweza kufuja mali hizo kwa urahisi sana sababu zipo kwenye majina yake. Kumbuka pamoja na kuwa mama lakini bado ni binadamu.
Sasa unaweza kuchagua, uandike jina lako au la mama kwa kuhofia ukiachana na mkeo msije kugawana🙏🙏.