NA DIRAMAKINI
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi amesema Shirika la Maaendeleo la Aga Khan (AKDN) limekuwa likijitahidi kuimarisha afya na ustawi wa jamii ulimwenguni kote pamoja na Zanzibar.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo Aprili 25, 2023 katika uzinduzi wa Kituo cha afya cha Kliniki cha Aga Khan jijini Zanzibar.
Ni kituo ambacho kitatoa huduma za dharura, huduma za kibingwa pia wagonjwa watapata huduma za afya zilizounganishwa kidijitali na Hospitali ya Aga Khan iliyopo jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali ya Zanzibar inatambua umuhimu wa huduma bora za afya hivyo sekta hiyo imepata mageuzi makubwa ambayo yanajumuisha huduma za afya kwa ngazi ya shehia, wilaya hadi mkoa kupitia hospitali za rufaa ikiwa na jumla ya vituo vya afya 172 ambavyo vipo katika wilaya 11 Zanzibar.