KUPELELEZWA. Tambua kuwa kama kunaweza kuwa na sababu za msingi au za kimaslahi, watu wanaweza kukupeleleza.
A. Malengo yao kukupeleleza yanaweza yakawa ni.
1. Kuujua uwezo wako
2. Kuujua udhaifu wako na jinsi ya kukushinda
3. Kujua jinsi gani wanaweza kukukwamisha
4. Kujua mbinu zako za kufanikiwa ili na wao wazitumie wafanikiwe kupitia mbinu zako.
5. Kukuwinda kwa lengo la kukudhuru, kuangalia ni jinsi gani watakudhuru kwakukuvizia ili wakuingize kwenye mtego wao.
Maelezo. Mara nyingi sana kuna watu wanaweza kumfutilia mtu hata bila yeye kujua kama anafuatiliwa.
Ni vema uwe makini sana na wapelelezi ambao wanatafuta kuujua undani wako, pia jihadhari kuwa na tabia ya kubwabwaja (kusema sema) hovyo kwani unaweza kumgawia adui mbinu ya kukushinda baada tu ya kujiweka wazi.
Inashauriwa mtu uwe na siri, usiwe mwepesi wa kijiweka wazi au kupenda kutoa taarifa muhimu za maisha yako (kwa watu ambao si lazima kwao kuzijua).
Mara nyingi watu wengi wanajikuta wamekwama na kushindwa kujua ni kwa nini, kumbe ni sababu ya adui kujua siri zako na kisha akaamua kukukwamisha.
Aidha, wengine wamepoteza maisha kwa sababu ya siri zao kuvuja kwa adui zao. Siri inafananishwa na mji wenye boma (fensi) Kama huna siri ni sawa na nyumba ambayo haina uzio (fensi).
Kwa hiyo kuficha siri zako za maisha, au kiuchumi, familia, na mambo muhimu ni kujiwekea ulinzi wako binafsi.
B. Hatari ya kupelelezwa na kutolewa kwa hai wa mtu maarufu.
Inapasa kujua, kwa kadiri unavyokuwa mtu maarufu na idadi ya maadui inaongezeka, kama vile idadi ya watu wanaokupenda inavyoongozeka.
Wapo wanaochukia tu kiwango chako ulichofikia na pia wapo ambao kwa njia moja au nyingine ni maadui kwako. Hivyo hutafuta njia ya kukumaliza. Hivyo kama ni mtu maarufu inapasa uwe na tahadhari kubwa katika kuhusiana na watu.
Kwa mfano ukiwa mtu maarufu kwa upande wa uongozi au siasa. Kuna watu unaweza kuwaharibia mambo yao, kwa mfano wewe ni polisi na umemkamata mtu akiwa na dawa za kulevya, na alikuomba ufanye mpango umuachie na ameahidi kukupa pesa, lakini ukakataa kwa kutunza maadili ya kazi yako na pengine pia kwakujua ubaya wa madawa ya kulevya na jinsi jamii inavyopata athari kwa madawa ya kulevya, au ni kwa kuheshimu maadili ya dini, sasa hili ni jema katika kutekeleza majukumu yako lakini kwa yule muhalifu ni baya sana.
Kitakachoendelea ni kutafutwa na wenzake wanaofanya kazi pamoja ili wakumalize kwa njia moja ama nyingine.
Au inawezekana wewe ni hakimu ambaye unahukumu keshi mbalimbali, kuna watu watahitaji uwasaidie kesi yao iende vizuri ikiwa na maana upindishe sheria ili wasitiwe hatiani, au pengine keshi nyingine ni za uongo tu, mtu amemtungia mwenzake uongo na kutaka kumkomoa na hivyo wanafikiria kumtumia hakimu ili atoe hukumu potofu kwa kuwafurahisha wao, au kuna watu wana kesi mbaya sana, kwa mfano mauaji, ubakaji, au uvunjaji na uporaji.
Sasa watu kama hawa kwakuwa tayari wanajua kesi yao ni ngumu kwao, hivyo wataanza kumshawishi hakimu ili asiwatie hatiani. Sasa ikitokea amekataa kupokea rusha na akahukumu kesi kwa haki, hivyo hao watu watachukia na kumuona ni mbaya, na tayari wanafikiria jinsi ya kumlipiza kisasi au kumkomoa.
Kwenye uongozi, unapokuwa kiongozi ni lazima kutakuwa na watu wataumia kupitia uongozi wako, na kukuona kama wewe ndio kikwazo cha mambo yao yasiende, hivyo tayari watapanga njia ya kukukomesha. Au pengine wanahitaji waipate nafasi yako (cheo chako). Ndipo mipango miovu itakapoanza kupangwa.
Tadhari za watu maarufu katika hili.
Hawapaswi kumwamini mtu yoyote, bali wanapaswa kuishi kipelelezi kama wao wanavyopelelezwa.
Kila wanachofanya kwanza wafikiri kuhusu usalama wao. Wanapokula, kunywa, kuvaa, kusafiri, kulala kitu cha kwanza kujiuliza ni vipi usalama wao utakavyokuwa.
Kwa nini watu maarufu wengi na viongozi hufuata huduma za kijamii nje ya nchi?.
Kwa mfano shule ya watoto wao, makazi, matibabu. Majibu haya, ni kwa sababu za kiusalama zaidi.
Kuna watu wanaweza kufuatilia hata watoto wako ili wawadhuru, kwa hiyo wanaposomea nje ya nchi yao inakuwa nafuu na salama kwao, au kuna watu wananunua nyumba nje ya nchi yao mataifa ya kigeni, hii ni kwa sababu za kiusalama zaidi kwani inafikia hatua maisha ya mtu yanakuwa mashakani katika taifa lake jinsi anavyo windwa.
Au kutafuta matibabu nje ya nchi, kwa mfano kama umewahi kusikia viongozi wanaenda kutibiwa nje ya nchi au watu maarufu wanaenda kutibiwa nje ya nchi pengine hata mafua tu, hii nikutokana na kuhofia usalama wao sio tu kwa sababu wamekuwa na pesa nyingi za kuchezea, ila wanahofia wapelelezi, kwani wapelelezi wanaweza kumfatilia mtu hadi anapokuwa mgonjwa, wapi atatibiwa, ili wawatafute madaktari wasio waaminifu wakudhuru. Kwa mfano wanaweza kukuwekea dawa nyingi (overdose) Au kukupiga sindano ya sumu na kisha ukafa (Nasema sio kila daktari bali wale madaktari wenye tamaa ya mali na wasiozingatia miiko ya taaluma yao). Ndio maana watu wengi ambao wanajua kuwa wanatafutwa huwa hawakubali kutibiwa hospitali yoyote nchini kwao. Mara nyingi wanaenda nje ya nchi, au kama ni ndani basi wanatafuta hospitari ambayo wanaamini usalama wao utazingatiwa.
Mambo ya kuzingatia kwa watu maarufu.
1. Wamtegemee Mungu. Zaburi 127:1 Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. Mithali 3:5.6 Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.
Kwakweli pamoja na mbinu nyingi tunazoweza kufundisha, lakini tujue kuwa mlinzi hodari ni Mungu. Tunapokuwa na imani hiyo itakuwa ni zaidi ya ulinzi. Kuna hatari nyingi ambazo hatuzioni lakini Mungu anatuepushia. Katika mengi ya kujilinda lakini dakika za mwisho tutarejea katika kusema Mungu pekee ndiye mlinzi wetu.
2. Unapotoka kwenye ratiba zako za kila siku baada ya kukutana na watu wengi, hakikisha unapokula chakula unawe mikono kwa sabuni tena unawe vizuri, kwani kuna watu wanaweza kuweka sumu kwenye mikono yao (kinganja)ili mnaposalimiana mkono wako uchukue sumu iliyokwenye mkono wake hata bila ya wewe kujua, na unapoenda kula chakula kwa wale ambao hutumia mikono wanaweza wakala na sumu, au pia ile sumu inaweza kudhuru maeneo mengine kama macho au pua unapoishika. Pia inashauriwa kula kwa kutumia kijiko ni salama zaidi kuliko kutumia mkono.
3. Unapoenda kwenye sherehe au mikutano ya watu wengi, wakati wa kupata chakula, unatakiwa uchote mwenyewe, na soda uchague mwenyewe kwa mkono wako usiache mtu akuchagulie soda, na maji. Na hakikisha unatoka mapema kabla ya wote au utoke pamoja na wengine na uongozane nao.
4. Usipende safari za usiku ukiwa peke yako, au usipende kupita njia za vichochoro au giza au maeneo ambayo yanaukimya sana.
5. Usiwe na mazoea ya kupata huduma sehemu moja hata watu wakakariri kuwa huwezi kukosena hapo.
6. Usiwe na marafiki usiowajua
7. Usipende kuongea maneno mengi, hasa yale yanayohusu siri za maisha yako au ratiba zako za maisha
8. Umuhimu wa kuwa na ulinzi nyumbani kwako, na umuhimu wa kutembea na walinzi kila unapotoka.
9. Kuwa na ulinzi maeneo ya shughuli zako kwa mfano kama wewe ni Mchungaji Kanisani kwako kuwe na walinzi (mashemasi) wanaojua kumpeleleza muhalifu iwapo ameingia kanisa kwa kujifanya kama yeye ni muumini (Aidha, Mchungaji ukifikia viwango vya umaarufu au kuhisi kutafutwa, usipokee vyakula vinavyotolewa na waumini haswa usio wajua vema kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kama unga, mafuta ya kula mchele nk., bali muumini akitaka aihudumie nyumba ya mchungaji kwa chakula atoe pesa au waende kununua pamoja na muhudumu wa Kanisa anayeaminika na Mchungaji).
Au pia kama wewe ni mwimbaji kwenye majukwaa au matamasha, au kiongozi wa siasa unafanya mikutano ya hadhara au vikao. Basi ni muhimu sana uwe na watu wanaopeleleza mazingira ya usalama wako.
10. Usiwe unaishi sehemu moja kwa muda wote, bali unaweza unakosekana mara kadhaa katika makazi yako kiasi kwamba mtu asiweze kutabiri kupatikana kwako nyumbani kwako.
viii. Kupeleleza/ kujifunza kupeleleza, umuhimu wa kuwa mpelelezi. Katika mataifa mengi yaliyoendelea sana utagundua wamefanikiwa sana katika idara za upelelezi.
Nchi zenye maendeleo makubwa nyingi ni magwiji katika eneo la upelelezi. Upelelezi ni njia muhimu sana ya kufanikisha mambo mengi sana au ni mbinu ya kuwashinda wale wanaoshindana nawe kiakili zaidi kuliko kutumia nguvu.
Upelelezi unasaidia kugundua siri nyingi ya kufikia malengo mapana. Upelelezi unasaidia kupata majibu sahihi ya kufikia lengo lako.
Upelelezi ni mbinu ya kugundua yaliyofichika na kuweka mikakati ya kuyafanikisha. Kuujua undani wa mtu au jambo au taasisi bila wenyewe kuwa na habari kuwa wamechunguzwa na siri zao zimejulikana.
Watu wengi wanakuwa na upelelezi usiokuwa wa kimaendeleo, kama vile kusoma meseji ya wapenzi wao kuona kama wana wapenzi wengine au kufuatilia nyendo za wapenzi wao, au wengine wanafuatilia maisha ya watu wengine au majirani zao, ili kupata habari (story) za kupigia umbea mitaani.
Lakini hawafanyi upelelezi wa kimaendeleo wa kuchunguza njia ya kufikia maendeleo makubwa kwa kungundua siri nyingi ambazo watu wanazitumia na wanatajirika na hawapo tayari kuzitoa kwa wengine.
Kwa mfano kuna matajiri wengi wameficha mbinu zao za kiutajiri ili watu wasiige, sasa wapelelezi kazi yao kutafuta siri za watu hawa…Inaendelea, Makala hii inatoka katika kitabu cha KUWA NA UWEZO MKUBWA KIAKILI. KWA MAULIZO AU KUPATA KITABU HIKI MUHIMU SANA WASILIANA NA;
Mwandishi wa Makala hii ni Mchungaji wa Kanisa la MGCT. Nyantira Kitunda Dar es salaam. Anapatikana kwa simu 0717528272.Email.kusomavitabu@gmail.com