NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof. Sospeter Muhongo ametembelea Kijiji cha Kusenyi, Kata ya Suguti na kutoa pole kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea Aprili 2, na Aprili 3, 2023 na kushuhudia uharibifu uliotokana na mafuriko pamoja na kugawa chakula cha dharura.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo Aprili 4, 2023 ambapo taarifa hiyo imesema chakula alichogawa Mbunge huyo ni pamoja na Magunia 25 ya mahindi, kila gunia lenye kilo 108 na maharage kilo 100.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa,"Vitongoji vilivyoathirika sana Kitongoji cha Nyabweke, Kaya 26 zimeathirika sana
Kitongoji cha Kwikuyu, Kaya 24 zimeathirika sana.
"Tathmini inaendelea kufanywa.Wakati taathimini ya uharibifu uliotokana na mafuriko hayo ikiendelea kufanywa, Mbunge huyo amebaini yafuatayo,
"Baadhi ya nyumba zimebomoka na kuanguka baadhi ya nyumba zimepasuka hazifai kutumika,
"Baadhi ya kaya, chakula chao kilichotunzwa majumbani kimeharibika na kingine kimesombwa na maji.
"Kuku na bata wamesombwa na maji huku tope nyingi sehemu za makazi ya watu.
"Tunategemewa kupata tathmini kamili ndani ya wiki hii.Kilichosababisha maafa haya. Wananchi, kwa uzoefu wao, wamebaini sababu kuu mbili ambazo ni
ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita 5, haukuzingatia uwekaji wa njia za kutosha kupitisha maji kwenda ziwani (Ziwa Victoria).
"Wakulima wa mpunga, n.k. walioko sehemu ya juu ya Kijiji cha Kusenyi wameweka miundombinu yao ya kilimo inayozuia maji kutitirika kwenye mikondo inayoelekea ziwani."
OMBI KUTOKA KIJIJINI KUSENYI
"Waathirika wa mafuriko ya Kijijini Kusenyi wanaomba tuwasaidie chakula, vifaa vya ujenzi (tathmini itaainisha idadi),
"Ujenzi wa miundombinu mikubwa ya kutiririsha maji ziwani. Ambapo Michango ipelekewe kwa DC Wilaya ya Musoma +255 756 088 624."
Picha za hapa zinaonesha matukio mbalimbali ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo akiwa na waathirika wa mafuriko Kijijini Kusenyi, Kata ya Suguti
Na viongozi 3 kutoka Kijijini Kusenyi wakipokea magunia 25 ya mahindi (@kilo 108), na gunia 1 la maharage la kilo 100.
"Tafadhali sana tujitokeze kuwasaidia waathirika wa mafuriko ya kijijini Kusenyi." imeeleza taarifa hiyo.
DIRAMAKINI imezungumza na Naomy Ally ni Mkazi wa Kusenyi amemshukuru Prof. Muhongo kwa kutoa msaada huo ambapo amesema kitendo cha kuwajali Wananchi hao ni alama ya upendo wa dhati kwa Wananchi wa Jimbo hilo.
Naye Esta Peter, amesema hatua ya Prof. Muhongo kuwatembelea Wananchi hao na kuwapa msaada ameonesha uungwana mkubwa kwani amecha majukumu mengi na kuwatembelea kuwatia moyo na kuwapa faraja.
"Tunamshukuru Prof. Muhongo kuja haraka kutuona na kutoa msaada kama kiongozi wetu tunamshukuru Sana kufika kwa wakati, Mungu azidi kumbariki Sana alipotoa kujali Wananchi hawa." amesema Joachim Shabani.