NA DIRAMAKINI
APRILI Mosi, mwaka huu katika Ukumbi wa Ubungo Plaza uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam mitume na manabii kutoka pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliandika historia mpya na kuanza mwanzo mpya wa kuiendea mipango na malengo yao ya kulihubiri neno la Mungu wakiwa wamoja.
Ni kupitia Kongamano la Kitaifa la Mashangilio ambalo Mtumishi wa Mungu Mtume na Nabii wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji mjini Morogoro,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala aliwekwa wakfu na kukabidhiwa rasmi fimbo ya kuongoza Baraza la Mitume na Manabii Tanzania kwa nafasi ya urais.
Mashangilio hayo, mgeni rasmi alikuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mheshimiwa Omary Kumbilamoto akiambatana na Askofu Dkt.Dunstan Haule Maboya, Askofu Profesa Ndalima, Askofu Prof.Paul Shemsanga.
Wengine ni viongozi, maaskofu wa makanisa ya kitume na kinabii akiwemo Mchungaji Anthony Lusekelo (Mzee wa Upako),Mtume na Nabii, Boniface Mwamposa (Bulldozer),Mtume S.S. Rolinga, Nabii Bendera na wengineo wakiwemo watu mashuhuri nchini.
Kupitia hafla hiyo, watumishi wa Mungu wakongwe na walezi na waangalizi wa baraza hilo walimkabidhi, Rais Dkt.Nabiijoshua fimbo kama ishara ya kuongoza akifananishwa na Musa ambaye aliongoza kundi la wana wa Israel.
Rejea maandiko kupitia Biblia Takatifu,Hesabu 17:1-11...“Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake.
"Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao. Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi.
"Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung'uniko ya wana wa Israeli, wanung'unikiayo juu yenu. Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao.
"Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana katika hema ya kukutania. Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushahidi; na tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa malozi mabivu.
"Kisha Musa akazileta nje hizo fimbo zote kutoka hapo mbele za Bwana na kuziweka mbele ya wana wa Israeli wote; nao wakaangalia, na kila mtu akaitwaa fimbo yake. Kisha Bwana akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung'uniko yao waliyoninung'unikia, ili wasife. Basi Musa akafanya vivyo; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo alivyofanya.”
Mbali na Rais Dkt.Nabiijoshua, pia viongozi wengine wa baraza hilo waliwekwa wakfu kwa lengo la kusimamia na kuongoza baraza hilo katika nafasi mbalimbali za juu.
Aidha, kongamano hilo ambalo lilihudhuriwa na watumishi mbalimbali wa dini wakiwemo viongozi wa Serikali lilibeba ajenda kuu ya kushangilia, kumshukuru Mungu, kuhimiza na kuhamasisha watumishi wa Mungu kuwa na maadaili mema na kusimama katika kweli.
Kupitia tukio hilo ambalo watumishi wa Mungu walibubujikwa na machozi ya furaha wakati Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania, Dkt.Nabiijoshua akikabidhiwa fimbo hiyo, Mlezi wa Mitume na Manabii Askofu Dkt.Maboya alifanya maombi maalumu na kumuwekea mikono Dkt.Nabiijoshua huku akimweleza kuwa fimbo hiyo nni alama ya uongozi.
"Fimbo hii ni alama ya uongozxi, usiumize mtu wa ina yoyote, leo hii tukiwa pamoja na mtumishi wa Mungu na baraka zote ambazo umepata kutoka kwa Profesa na Nabii Paul Shemshanga,tunakabidhi fimbo hii kama alama ya uongozi, ukapate kuishi kama neno linavyosema, usiwe mnafiki, uwe mkweli.
"Ukae karibu na wazee katika masuala yote yaliyo magumu, usisikilize neno la mtu mmoja na kulifanyia kazi, wakati utakappona haulielewi jambo, tafuta washauri, Mungu akakusaidie, ni mzigo mkubwa. Kumbuka kuna bodi ambayo itakuongoza,usifanye maamuzi ya peke yako, unafanya maamuzi na kusimamia maamuzi ya kikao na jambo ambalo limezidi unaenda kwenye bodi,"amefafanua Mlezi wa Mitume na Manabii nchini, Askofu Dkt.Maboya.
Steven Nyerere
Katika kongamano hilo,mwigizaji maarufu wa filamu hapa nchini, Steven Nyerere akizungumza kama mdau wa injili, lakini muumini wa dini ya Kikristo alitoa ombi maalumu.
Maombi yake kwa wazee na watumishi wa Mungu wakongwe kwenye huduma ya injili hapa Tanzania ni kuwa wazidi kutolea macho sana juu ya misingi ya kimaadili na kweli katika imani.
Alisema, siku za karibuni jamii imeathirika sana na utitiri wa watumishi ambao wanapotosha watu kwa kutumia Neno la Mungu na imani za Kikristo hasa za wokovu.
Pia alisema yeye binafsi hawezi kutumia kipawa chake cha ucheshi na mzaa mbele za Mungu maana Mungu kuwa hadhihakiwi.
Akisisiza alisema, Mungu ndiye anayempa kibali na nafasi ya yeye kuwa pale alipo hivyo anaheshimu mno na kuitunza hofu yake kuu mbele za Mungu.
“Namuomba Baba yangu Askofu Maboya simameni, muwataje manabii ambao hawapo kichama, hamuungani sehemu yoyote na hamkutani, lakini tukikutana nao mtaani wanasema mimi nabii,”alisema.
Rais Dkt.Nabiijoshua
Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania,Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa licha ya changamoto mbalimbali zinazoendelea kuikabili Dunia kupitia nyanja tofauti tofauti ikiwemo za kijamii na kiuchumi.
"Nitakua sijatenda mema kama sitamshukuru kipekee sana mama yetu, Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Serikali yake anayoiongoza.
"Kwani,pamoja na changamoto nyingi ambazo taifa letu linapitia juu ya mambo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa,kwa mafanikio makubwa bado hekima, umoja na amani zimebakia kuwa ndiyo ngao kuu za ulinzi wa usalama na ustawi wa taifa letu.
"Bila kusahau undungu, mshikamano,mila na desturi zetu zinazoishangaza Dunia wakati wote.Asante sana Mhe.Rais na mama yetu, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuzienzi tunu hizi za utu na ubinadamu wetu walizotuachia waasisi wa Taifa letu hili jema la Tanzania,
"Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Abeid Amani Karume, ambayo wewe ndiye kiongozi wake mkuu wa kwanza mwanamke na mwenye moyo halisi wa mama Tanzania, Mungu akubariki sana mama yetu mwema sana,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.Katika hatua nyingine, Rais Dkt.Nabiijoshua amemshukuru Mungu kwa kuendelea kuwaunganisha mitume na manabii Tanzania kwa ajili ya kuujenga Mwili wa Kristo, kuhubiri na kueneza habari njema ya neno la Mungu mijini na vijijini.
"Mungu, amedhihirisha furaha yake kwetu kwa kutufanya wamoja kama tulivyo hivi leo.Nawashukuru wazee wetu kwa kuunga mkono jitihada hizi za Umoja wa Mitume na Manabii Tanzania, asanteni sana kwa upendo wenu huo.
"Mitume na manabii natambua kuwa tumefika hapa leo kwa sababu wote tumelipa gharama za umoja wetu huu. katika kulipa gharama hizo, wengi mmeumizwa sana kila mtu kwa namna yake nawasihi sameheni yote kwa maana sasa yamekuwa mapya.
"Ndugu zangu mitume na manabii, mashangilio haya hatutashangilia bure. Katika mfuko wangu wa kichungaji nimebeba nakala ya cheti cha usajili wa baraza ambalo ni chombo halali cha mitume na manabii wote Tanzania pamoja na makundi mengine madogo ya imani za kilokole walio nje ya TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania), CCT (Baraza la Jumuiya ya Kikristo Tanzania) na CPCT (Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania).
"Tumefikia hapa tulipo kwa sababu Mungu asiyedhihakiwa alimwandaa mzee wetu mtume na mpiganaji mkuu wa vita vya nyikani Profesa Paul Zemu Shemsanga, mlezi wetu mkuu na mtu shujaa asiyerudi nyuma kabla ya ushindi kupatikana Baba yetu Askofu Dkt.Dastan Haule Maboya, mzee wetu mlezi wa mkoa wa Kilimanjaro, Bishop Mwanga na wazee wengine waliokuwa mstari wa mbele katika kutusaidia kufanikisha chombo hiki kinacholetwa kwenu kwa utukufu wa Mungu wetu wa milele na milele.
"Kwa maumivu makubwa waliijenga safina ambayo sisi kuanzia leo tutakaa ndani yake wakati gharika ikiendelea huko nje,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.
Wakati huo huo, Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania, Dkt.Nabiijoshua ametoa wito kwa mitume na manabii kusimama imara kupiga vita hamasa ya mapenzi ya jinsia moja, vitendo ambavyo siku za karibuni vimeshika kasi duniani.
"Dunia yetu hivi sasa imekumbwa na wimbi la usodoma na gomora, watu wanausambaza ushoga na usagaji kwa gharama ya kununua Dunia yote iwe mali yao ya kishetani, pamoja na watu wote waishio humo. Hii ni dhambi kubwa mbele za Mungu kwa kawaida dhambi huwa haitosheki hadi izae mauti.
"Tusipochukua hatua za haraka na ukali unaohitajika kuiondoa hii dhambi katika nchi yetu, amin...amin nawaambia siku si nyingi vijana wetu watalazimishwa kuoana na wanyama na hawa ni wengine wa mwituni wa mapori ya dunia hii.
"Ndugu zangu mitume na manabii ili kushinda vita hii hatuna budi kumlilia Mungu, kufundisha, kuonya, kumea na kukaripia dhambi hii kwa nguvu zote.
"Natoa wito huu mkubwa kwenu, tukiiachia Serikali peke yake jambo hili ni zito litailemea kabisa. Ni wajibu wetu sote kusema basi na kuungana na madhehebu mengine ya dini nje ya imani zao kwa ajili ya taifa letu, wakiwemo waislamu ambao kwenye jambo hili haramu linalokosoa uumbaji wa Mwenyezi Mungu, wameonyesha kwa vitendo kwamba watalipa gharama za kulipinga kwa uwezo wao wote kabisa,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.
Ameendelea kufafanua kuwa, "Sasa naomba niwarudishie furaha yenu kwamba, baraza hili linalounganisha mitume na manabii wote Tanzania hadi sasa linamiliki vyuo vikuu viwili vya theolojia.
"Japan Bible Institute-Graduate School of Theology ambayo imeruhusiwa kuendesha mafunzo yake ya kidini na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Tume ya Vyuo Vikuu vya Kikristo Ulimwenguni.
"Chuo kinatoa certificate hadi PHD za elimu ya Kikristo. Jumla ya kozi ni 55, pia baraza limesimamia lugha mpya ya Kiungu ya TACHIL.
"Hivyo, naomba wenyeviti wote wa mikoa na wilaya zote muwe tayari kusimamia majukumu ya kiuongozi na kuwezesha mitume na manabii wote ili kuhakikisha wanajiunga na vyuo vyetu hivyo ili kujiongezea elimu, maarifa na ujuzi zaidi katika huduma zetu.
"Na sasa tuna uwezo wa kuwadhamini watumishi wa Mungu wenye huduma ambazo hazijasajiliwa, nitawalea hadi watakapopata usajili serikalini.
"Pia naomba niwashukuru vyombo vya habari na wamiliki wao ikiwemo TOPTV+ kwa kujitolea kwenu kurusha matangazo haya ili umma wa watanzania uweze kupata taarifa sahihi kuhusu mwili wa Kristo Tanzania. Asanteni sana,"amesisitiza Rais Dkt.Nabiijoshua.
HAKIKA INA PENDEZA SANA NIMEFURAHI SANA MIMI KAMA MOJA YA MANABII NIKIWA MWANZA NABII ELIYA KILAGULA WA KANISA LAPATMOS MINISTRIES FOR ALL NATIONS NIME FARIJIKA SANA AHSANTE RAISI WETU NABII JOSHUA MUNGU WA MBINGUNI AKUBARIKI SANA.
ReplyDelete