NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amezindua Mpango Mkakati wa mwaka 2022-2027 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (wa pili kulia) akionesha vitabu kuashiria uzinduzi wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) jijini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama, Mhe. Simbachawene amesema Mpango Mkakati huo unaotarajiwa kutumia Dola za Marekani milioni 363 unalenga kuboresha masuala mbalimbali yakiwemo kuimarisha utekelezaji wa mikakati ya kukabiliana na maafa kabla hayajatokea.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa Mpango huo utawezesha Utekelezaji wa Mpango wa Lishe kwa jamii na mpango wa chakula shuleni na Kukuza jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na urejeshaji hali wa mazingira.
“Utekelezwaji wa Mpango Mkakati huu ni wazi utasaidia kuwainua wakulima wadogo ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuwawezesha kupata masoko ya mazao. Katika eneo hili WFP itawasaidia wakulima kuwa na utaratibu bora wa kutunza mazao kabla kuyafikisha sokoni (Post Harvest strategies) na kutoa elimu kwa wakulima kuhusu,”amesema Mhe. Simbachawene.
Vile vile amezitaka Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zitakazonufaika na utekelezaji wa Mkakati huo kushirikiana WFP ili kuhakikisha shughuli zilizopangwa zinatekelezwa na kuchangia katika kuboresha hali za maisha ya watu.
“Uzinduzi huo unafuatia kukamilika kwa Mpango Mkakati wa WFP uliotekelezwa kwa kushirikiana na Serikali kuanzia mwaka 2017-2021 na Serikali inatambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau katika kuchangia maendeleo ya Nchi,” amebainisha Mhe. Simbachawene.
Katika hatua nyingine Waziri Simbachawene ameeleza kwamba Mkakati huo utawezesha nchi kufikia malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 ambayo yamejikita katika kupunguza umasikini na kuleta ustawi wa maisha ya watu.
Aidha Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bi. Sarah Gordon-Gibson ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa usaidizi, uaminifu na ushirikiano wake huku akiahidi kuwa WFP itahakikisha Tanzania inakuwa nchi endelevu na yenye uwezo wa kustahimili maisha bora kwa Watanzania wote.