Nabii Dkt.Mjuni apasa sauti kuhusu ukatili wa kijinsia,mapenzi ya jinsia moja

NA DIRAMAKINI

MTUMISHI wa Mungu wa Huduma ya Yerusalemu Pomerini Ministry iliyopo mkoani Iringa, Nabii Dkt.Mjuni Kisha amesema, watumishi wa Mungu nchini wanapaswa kuunganisha nguvu kukemea ikiwemo kulaani vitendo vya ukatili wa kijinsia na mapenzi ya jinsia moja.
Dkt.Mjuni ameyasema hayo kupitia ibada kubwa iliyofanyika Yerusalemu Pomerini Ministry mkoani Iringa.

"Kamwe mkia hautikisi ng'ombe, tulioanzisha huduma tupige kazi,punguza vikao, maumivu huwaleta watu pamoja,katika kipindi hiki tunaumizwa na ushoga tuwe wamoja kupinga vitendo hivi vya ukatili kama Rais wetu alivyosisitiza ukatili wa kijinsia tuupinge.

"Hakuna mtu anaweza kuwabadilishia hisia zao mashoga kamba yetu iwe moja maombi ya toba na rehema,mwisho kila mnachokifanya fikiria kuipenda nchi yako kwani kuzaliwa Tanzania si kwa bahati mbaya,"amefafanua Nabii Dkt.Mjuni.

Amesema, ni jambo lisilokubalika mbele za Mungu na sheria za nchi kwa wanaume kujigeuza wanawake na wanawake kujigeuza wanaume.

"Tukatae kwa nguvu zote na viongozi wote wa dini tuwaunge mkono viongozi wetu kuwapinga mashoga na wasagaji, tusikubali kupokea maovu hayo kwa kigezo cha kupata misaada,kwani tukiacha vikaendelea siku moja tutakuja kushangaa mambo yakibadilika kabisa ndani ya jamii zetu," amesema Dkt.Mjuni.

Pia, Dkt.Mjuni ametoa wito kwa wazazi na walezi kuzingatia malezi bora kwa watoto wao ili kuandaa familia,jamii na Taifa lenye hofu ya Mungu.

"Si jambo la baraka watoto wetu kuachwa bila malezi, wazazi hawana muda nao wanajilea wenyewe.

"Baba unakuta hana muda na familia, wakati usiku mwingine anarudi amelewa nyumbani, mtoto naye utakuta usiku yupo tu mitaani anafanya ayajuayo yeye.

"Umefika wakati tuwalee watoto wetu katika uadilifu na tuliombee Taifa letu. Utandawazi hautaacha Taifa na Dunia salama,” amesema Dkt.Mjuni.

Aidha,ndoa ni muungano kati ya mwanamke na mwanamume kuishi pamoja kama mume na mke muda wote wa maisha yao kulingana na Kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.

Pia, sheria za nchi za mwaka 1971 ambazo Tanzania imeziridhia kutoka kwa Waingereza zinakataza ndoa za jinsia moja na kutamka kuwa linapofika suala la ndoa au mahusiano ya kimapenzi linahusisha watu wa jinsia tofauti.

“Wote tunajua msingi wa familia ni mume na mke ambao wanaweza kuzaa watoto...pia sheria ya makosa ya jinai inaeleza msimamo ndio huo, hivyo kwenda kinyume ni makosa ambayo mtu anaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka 30 jela."

Pia, kulingana na Kifungu cha 10 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kuna aina mbili za ndoa, mosi ni ndoa ya mke mmoja, hii ni ndoa ambapo mwanaume ana mke mmoja tu, mfano ndoa za Kikristo.

Pia, kuna ndoa ya wake wengi, hii ni ndoa ambayo mwanaume ana wake zaidi ya mmoja, mfano ndoa za Kiislamu na kimila.

Ndoa hizo zinaweza kufungwa kwa kufuata taratibu za kidini, kiserikali au kimila. Utaratibu huo utafuata au kuzingatia kama wanandoa ni waumini wa dhehebu au la. Kulingana na Kifungu cha 25 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kuna aina tatu za ufungaji wa ndoa.

Mosi,ndoa ya kidini, hii hufungwa kwa mujibu wa taratibu ya dini husika kama ni Kikristo, Kiislamu au dhehebu la wahusika katika ndoa. 

Jambo la msingi ni lazima masharti yote yatimizwe kisheria na taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe na ndoa ifungiwe mahali pa wazi panapokubalika kisheria na mfungishaji awe na mamlaka hayo kisheria.

Pili,ndoa ya kiserikali,hii hufungwa mbele ya mkuu wa wilaya ambaye ndiye Msajili wa Ndoa na wanandoa wanaokusudia kuwa na ndoa ya kiserikali. Ndoa itafungiwa katika Ofisi ya Msajili (mara nyingi hufungwa bomani kwa mkuu wa wilaya) au mahali pengine popote palipotajwa katika leseni yake ya kufungisha ndoa.

Tatu ni ndoa ya kimila,hii inaweza kufungwa kimila iwapo mmoja wa wafunga ndoa au wote wawili wanafuata sheria za mila za kabila fulani. 

Aidha, mwandishi wa ndoa za kimila ni Katibu Tarafa (Afisa Tarafa) wa eneo husika ambako ndoa ya kimila inakwenda kufungishwa. 

Ndoa ya kimila hufungishwa na mtu anayetambulika kimila kuwa ana uwezo huo. Ni muhimu sana Katibu Tarafa kuhudhuria kwenye ufungishaji huo wa ndoa, kwani ndiye atakayehusika na kupeleka vyeti vya ndoa kutoka kwa msajili.

Wakati huo huo, ukipitia katika Sheria ya Ndoa mwaka 1971 kifungu cha 9.Wanaooana wawe wamekubaliana pasipo kulazimishwa na mtu. Ndoa ni ya mwanamke na mwanamume, ni ndoa ya kudumu maishani.

Vivyo hivyo, mpango na utaratibu wa Mungu kwa wanandoa umewekwa wazi, rejea Biblia Takatifu kitabu cha Mwanzo 2:18, " “Bwana Mungu akasema si vema mtu huyu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufafana naye”. 

Pia, rejea Mathayo 19:3-6...3-"Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?.

4-Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, 5-akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?.

6-Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe."

Biblia inasisitiza kila mara kwamba ushoga ni dhambi,rejea Mmwanzo 19:1-13; Mambo ya Walawi 18: 22; Warumi 1:26-27; 1Wakorintho 6:9. 

Vile vile,Warumi 1:26-27 inatufundisha kwamba ushoga ni njia mojawapo ya kumkana na kutomtii Mungu. 1Wakorintho 6:9 inasema kuwa mashoga hawataurithi ufalme wa Mungu.

Walawi 18:22, 24-25 “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo. Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote; na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa”.

Mwanzo 19:1-13 “ Basi, wale malaika wawili wakaja Sodoma jioni; na Lutu alikuwa amekaa mlangoni pa Sodoma. Lutu akawaona akaondoka akaenda kuwalaki, akainama kifudifudi. 

Akasema, Bwana zangu, karibuni nawasihi mwingie nyumbani mwa mtumwa wenu, mkalale, mkanawe miguu yenu, hata asubuhi mwondoke na mapema mkaende zenu. Wakasema, Sivyo, lakini tutakaa uwanjani usiku kucha. 

Akawasihi sana, nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate isiyochachwa nao wakala. Hata kabla hawajalala, watu wa mji, wenyeji wa Sodoma, wakaizunguka nyumba, vijana kwa wazee, watu wote waliotoka pande zote. 

Wakamwita Lutu, wakamwambia, Wa wapi wale watu waliokuja kwako usiku huu? Uwatoe kwetu, tupate kuwajua. Lutu akawatokea mlangoni, akafunga mlango nyuma yake. Akasema, Basi, nawasihi, ndugu zangu, msitende vibaya hivi. 

Tazama, ninao binti wawili ambao hawajajua mtu mume, nawasihi nitawatolea kwenu mkawafanyie vilivyo vyema machoni penu, ila watu hawa msiwatende neno, kwa kuwa wamekuja chini ya dari yangu. Wakasema Ondoka hapa! Kisha wakanena, Mtu huyu mmoja amekuja kwetu kuketi hali ya ugeni; naye kumbe, anataka kuhukumu! Basi tutakutenda wewe vibaya kuliko hawa. 

Wakamsonga sana huyo mtu, huyo Lutu, wakakaribia wauvunje mlango. Lakini wale watu wakanyosha mikono yao, wakamwingiza Lutu kwao nyumbani, wakaufunga mlango. Kisha wakawapiga hao watu walioko mlangoni kwa upofu, wadogo kwa wakubwa, hata wakachoka kwa kuutafuta mlango. 

Basi wale watu wakamwambia Lutu, Je! Unaye mtu hapa zaidi? Mkwe, wanao, na binti zako, na wo wote ulio nao katika mji, uwatoe katika mahali hapa; maana tutapaharibu sisi mahali hapa, kwa kuwa kilio chake kimezidi mbele za BWANA; naye BWANA ametupeleka tupaharibu.”

Hivi karibuni, Nabii Mjuni ametunukiwa Udaktari wa Heshima kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuwahudumia Watanzania kupitia neno la Mungu na kuwapatia mahitaji mbalimbali huko vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news