NA DIRAMAKINI
MTUMISHI wa Mungu wa Huduma ya Yerusalemu Pomerini Ministry iliyopo Kilolo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa, Nabii Dkt.Mjuni Kisha amelitaka kanisa la Tanzania na barani Afrika kuyaonesha matatizo yanayoikabili jamii na kumuomba Mungu ili atoe majibu namna ya kuyapatia ufumbuzi.
Nabii Dkt.Mjuni ambaye amekuwa balozi mwema katika kuyaibua matatizo na changamoto zinazoikabili jamii ikiwemo mahitaji ya msingi na kuyapatia ufumbuzi kwa kadri Mungu anavyomjalia amekuwa akisisitiza kuwa, watumishi wa Mungu wana mchango mkubwa katika kuisaidia jamii mahitaji ya kiroho na kimwili.
"Kanisa la Afrika linapaswa kuonesha matatizo ya kijamii yanayohusiana na chakula,ulinzi, afya na uhuru wa mtu na tunapofanya hivyo tusisahau wala kupuuza masuala ya kiroho,tusipofanya hivyo baadae tutaona vitu katika muonekano mbaya kama kioo,"amefafanua Nabii Dkt.Mjuni.
Pia, amesema makanisa hujenga ushirika na kushiriki kwa vitendo ndani ya jamii na kufanya kazi kutetea haki,amani na upatanisho kwa ustawi bora wa jamii,Taifa na Dunia kwa ujumla.
"Hivyo, sisi watumishi wa Mungu kupitia huduma tunazoongoza tuna jukumu kubwa kuhakikisha kanisa linashiriki katika shughuli zinazoonekana, na wakati mwingine kanisa linashuhudia kwa sauti kubwa kwa njia ya huduma kwa majirani wenye uhitaji na ikiwezekana kufanikisha mahitaji muhimu kwa wahitaji,"ameongeza.