NA JAMES MWANAMYOTO
KATIBU Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema ofisi yake haitosita kuwachukulia hatua za kinidhamu waajiri katika taasisi za umma watakaobainika kwenda kinyume na utaratibu kwa kuwakaimisha ukuu wa idara na vitengo watumishi wasio na sifa za kutumikia nafasi hizo, kwani kitendo hicho kimesababisha ofisi yake kulalamikiwa mara baada ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutoa ripoti inayoanisha uwepo wa watumishi wanaokaimu kwa muda mrefu bila kuwa sifa stahiki.
Bw. Mkomi amesema hayo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene, wakati akimuwakilisha waziri huyo kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, sehemu ya Tanzania (AAPAM Chapter-Tanzania).
“Mnaoshiriki kikao hiki ndio wenye jukumu la kusimamia rasilimaliwatu Serikalini hivyo mnapaswa kuwakumbusha waajiri kuzingatia taratibu za kumkamisha mtumishi nafasi ya ukuu wa idara au kitengo na kuongeza kuwa, yuko tayari kumchukulia hatua mwajiri yeyote atakayekiuka utaratibu kwa kukaimisha mtumishi asiye na sifa stahiki kwani ripoti ya CAG inaitaja ofisi yake wakati wanaosababisha changamoto hiyo ni waajiri,” Bw. Mkomi amesisitiza.
Bw. Mkomi ameongeza kuwa, wenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu katika baadhi ya taasisi za umma hawaishirikishi Ofisi ya Rais-UTUMISHI katika mchakato wa kuwakaimisha watumishi nafasi za uongozi na kusababisha watumishi hao kukaimu kwa muda mrefu bila kupata stahili za nafasi wanazokaimu, hivyo kuibua malalamiko yanayoepukika iwapo taratibu zingezingatiwa.
“Utaratibu wa mtumishi kukaimu si zaidi ya miezi sita lakini ninyi mnaosimamia rasilimaliwatu katika taasisi zetu hamzingatii taratibu na kusababisha ofisi yangu ilalamikiwe kwa kitendo cha uwepo watumishi wanaokaimu kwa muda mrefu kwasababu ya kukosa sifa za kuidhinishwa kukaimu nafasi walizopewa na waajiri,” Bw. Mkomi amefafanua.
Aidha, Bw. Mkomi amekemea kitendo cha baadhi ya waajiri wenye utamaduni wa kuwakaimisha watumishi wasio na sifa ili wapate muda wa kutosha wa kuwatafuta watu wao ambao wamedhamiria kuwapatia nafasi hizo kwa ajili ya maslahi yao binafsi na si ya ofisi.

Sanjari na hilo, Bi. Mavika amesema kuwa mkutano huo utawawezesha kubaini changamoto wanazokabiliana nazo katika eneo la usimamizi wa masuala ya utawala na rasilimaliwatu ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kuzitatua changamoto hizo kwa lengo la kuongeza ufanisi kiutendaji.
Bi. Mavika amesisitiza kuwa, taaluma ya usimamizi wa rasilimaliwatu na utawala ndio kiungo muhimu na msingi wa uendeshaji wa taasisi yoyote hivyo wao kama jumuia ya Wataalam wa Utawala na Rasilimaliwatu Afrika, sehemu ya Tanzania wanatumia fursa ya mkutano huo kuweka mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto ya uwepo wa malalamiko ya wananchi dhidi ya huduma zitotolewazo na baadhi ya taasisi za umma nchini.