Polisi watangaza msako dhidi ya mtandao unaofukua makaburi kishirikina Singida

NA DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Singida limekamata watuhumiwa saba waliofanya mauaji na kufukuwa makaburi kwa imani za kishirikina huko wilayani Manyoni.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi makao makuu ya Polisi jijini Dodoma,SACP David A.Misime.

"Tumeona kwenye mitando ya kijamii taarifa ya kufukuliwa kaburi la mzee mmoja huko wilayani Manyoni na kudaiwa kuchukuliwa baadhi ya viungo. Taarifa hizo zimeonesha wananchi wanahoji polisi wameshindwa kudhibiti uhalifu huo?.

"Kaburi lililofukuliwa hivi karibuni na wahalifu, uchunguzi umebaini kilichochukuliwa ni nguo, cheni, saa, pete na viatu vya marehemu na hakuna kiungo kilichochukuliwa.

"Matukio haya ya kishirikina huko wilayani Manyoni kwa uchunguzi uliofanyika, umebaini yanaongozwa na imani potofu za kishirikina ambazo ni aibu na pia ni uhalifu.

"Tangu matukio haya yaanze kutokea wilayani humo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limefanya jitihada kubwa na kufanikiwa kukamata watuhumiwa saba waliofanya mauaji na kufukuwa makaburi kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo alivyotoa taarifa kwa waandishi wa habari Machi 28, 2023. Watuhumiwa hao saba walifikishwa mahakamani Aprili 4, 2023,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kutoka Jeshi la Polisi makao makuu, mtandao huo wa watu wenye imani hizo potofu za kuua na kufukua makaburi kwa lengo la kupata viungo na mali nyingine za marehemu unaonesha bado upo. "Na Jeshi la Polisi muda si mrefu litaumaliza na wahusika watafikishwa mahakamani,"imeongeza taarifa hiyo.

"Jeshi la Polisi lingependa kutoa wito, pamoja na jitihada zinafanywa na polisi za kukamata wahalifu hao na kutoa elimu kwa jamii ili kuondokana na fikra hizo potofu, kikubwa ni kwa wananchi kukubali kubadilika na kuachana na imani hizo mbaya.

"Kwani ni kosa la jinai kufukuwa makaburi, lakini pia ni aibu kwa dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia kuendeleza imani hizo potofu,"imeongeza na kufafanua taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news