NA CATHERINE SUNGURA
CHANJO huzuia takribani vifo milioni mbili hadi tatu kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani
Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof.Tumaini Nagu wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Kitaifa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati mkoani Manyara.
"Hapa nchini mafanikio ya chanjo ni dhahiri kwa mfano tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa ndui,magonjwa ya dondakoo,kifaduro,polio na pepopunda.Chanjo ni afua muhimu katika kutokomeza magonjwa na kupunguza vifo hususani vya watoto wa chini ya miaka mitano.
"Chanjo pia hupunguza gharama kubwa ambazo familia zetu kwa ujumla ingetumia katika kutibu maradhi yatokanayo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo,"ameongeza Prof.Nagu.
Aidha, amesema Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika utoaji wa chanjo kwa walengwa licha ya kuwa na changamoto ya uwepo wa mlipuko wa UVIKO-19 ambao kwa kiasi kikubwa uliathiri huduma za chanjo nchini.
"Nitoe msisitizo kuwa mtoto yeyote ambaye hajapata kabisa chanjo au hajakamilisha ratiba ya chanjo ni hatari sana kwa afya yake kwa sababu anaweza kuambukizwa magonjwa na pia ana hatari ya kuwaambukiza wengine kwa sababu hana kinga kamili ya mwili,"amesema.
Vile vile amesema wiki hii ni mahususi katika kuhimiza familia kuwapeleka watoto wote wanaostahili kupata chanjo katika vituo vinavyotoa huduma za afya vya Serikali na binafsi ili wapate chanjo
Hata hivyo amesema kuwa, Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kuhakikisha huduma za afya hususani za chanjo zinaendelea na zinaboreshwa ikiwemo ununuzi wa chanjo unafanyika kwa wakati ili kuwa na chanjo za kutosha muda wote na kuongeza majokofu ya kisasa yenye kuimarisha mnyororo baridi ili kuhakikisha kuwa chanjo zinatolewa zina kuwa katika ubora.
Naye, Mwakilishi wa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt.Boniface Makelemo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua thabiti zinazochukuliwa kupunguza athari za magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Amesema, WHO na jumuiya nzima ya Umoja wa Mataifa na washirika wao wote wa chanjo wanaunga mkono juhudi za Serikali na kujitolea rasilimali watu na fedha zinazohitajika ili kuinua kiwango cha chanjo kwa watu wote wanaostahili chanjo kwa rika zote.
"Kwa hiyo wiki hii ya chanjo tuhakikishe chanjo inaendelea kushikilia nafasi yake katika ajenda za maendeleona usalama Kitaifa".
Kwa upande wa Chanjo ya UVIKO-19, DktMakelemo ameongeza kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa katika utoaji wa chanjo hiyo ambapo asilimia 52 ya watu wamepata chanjo ya UVIKO-19 na kuipongeza Serikali kwa mafanikio hayo.