Rais Dkt.Mwinyi aahidi mema zaidi kwa taasisi zinazohudumia mahujaji

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi mbalimbali zinazowahudumia mahujaji wanaokwenda Makka, Saudi Arabia kutekeleza ibada ya hijja, baada ya kukamika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 22, 2023 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakati akihutubia Baraza la Eid -El- Fitr kwenye ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, Kikwajuni Mkoa wa Mjini Magharibi jijini Zanzibar.

Amesema, Serikali kupitia Kamisheni ya Wakhfu na Mali ya Amana itaendelea kufanya kazi kwa ushirikino na taasisi hizo ili kuzifanyia kazi changamoto zinazowasababishia usumbufu waumini wanaohitaji kwenda Hijjah.

Akizungumzaia suala la maadili wakati huu wa Sikukuu ya Eid el Fitr, Alhaj Dkt.Mwinyi ameihimiza jamii kuendeleza maadili ili kujiepusha na vitendo viovu vikiwemo uvunjifu wa amani, udhalilishaji, rushwa, ubadhirifu na dhuluma.

Pia amewaasa wananchi kuendelea kuheshimiana, kutii sheria za nchi, kuwa waadilifu, washirikiane pamoja na kuiendeleza amani iliyopo kwa umoja na mshikamano baina yao.

Alhaj Rais Dkt.Mwinyi amesema, kwa nyakati tofauti jamii zimekuwa zikikumbushwa kuhusu umuhimu wa kuendeleza maadili ili kupata mustakbali wa jamii njema.

Ameongeza kuwa, suala la kuporomaoka kwa maadili bado linaitesa jamii na kuchangia kuzorotesha juhudi za maendeleo kwenye ustawi wa jamii.

Vile vile, Alhaj Mwinyi aliisihi jamii kuendelea kupiga vita mambo yasiyoendana na maadili, mila, silka na tamaduni za Wazanzibari ili kupata kizazi kilichoongoka.

“Tuendelee kushirikiana katika kuyapiga vita mambo haya, hayaendani na maadili mema, silka na utamaduni ulioacha na wazee wetu,”amesisitiza Alhaj Mwinyi.

Akizungumzia suala la malezi, Alhaj Dkt.Mwinyi amewaasa wazazi, walezi na wazee kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto wao ili wawe waumini bora na raia wema wa kwa nchi yao pamoja na kuwasimamia kupata haki yao ya elimu ikiwemo elimu ya dini pamoja na kulinda usalama wao dhidi ya mambo yanayoweza kuwadhuru.

Sambamba na hayo amewahimiza wazazi na walezi kuzingatia usalama wa watoto wao hasa wakati huu wa sikukuu kwani ni wajibu wao kuwasimamia na kuhakikisha wapo salama dhidi ya mambo yote yanayoweza kuharibu furaha na amani yao pamoja na wazazi wao.

“Wajibu huu tuubebe sote kwa kuhakikisha watoto wetu wanatoka majumbani na wanarejea wakiwa salama,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi,.

Mapema asubuhi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alijumuika na waumini wa dini ya Kislam kwenye sala ya Iddi Fitri iliyosaliwa msikiti wa Masjid Zinjibar Kiembesamaki.

Pia alipata fursa ya kuzungumza na mashehe kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar waliofika Ikulu, Zanzibar kwa ajili ya kumtakia salamu ya heri ya Eid el Fitr.

Katika hafla hiyo, Alhaj Dkt.Mwinyi pia aliwaasa Mashehe hao kuendelea kuwaelekeza wananchi kuhusu masuala ya maadili, kuendeleza mashndano ya Qur’an.

Alisema, mambo yote yaliyokua yakifanywa kwEnye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan yaendelezwe kwenye miezi mingine inayoendelea pamoja na kuendelea kuhimiza amani ya nchi kwa waumini wote.

Kwenye hafla ya Baraza la Eid, viongozi mbalimbali wa Serikali na siasa walihudhuria wakiwemo Marais wastaafu wa Zanzibar Awamu ya Sita, Dkt.Amani Abeid Karume, Dkt.Ali Mohamed Shein, Rais wa Awamu ya Saba, Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah,

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shekh Saleh Omar Kabi, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Shaaban, Mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hafidh Ameir na Mawaziri na Manaibu mawaziri na viongozi wengine wastaafu wa Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news