Rais Dkt.Mwinyi atoa wito kwa wazazi kuhusu maadili

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewataka wazazi kurudi katika mstari wa malezi kwa watoto ili kulinusuru taifa dhidi ya majanga mbalimbali yanayojitokeza ambayo yamekuwa yakisababishwa na mmomonyoko wa maadili. 
“Nipende kuwasisitiza ndungu zangu suala la maadili mema ni kila Mtanzania na si suala la kitaasisi,lakini nimpongeze Sheikh Kapolo kwa kulea vijana wengi katika maadili mema na kwa kufanya kazi ya kumpendeza Mwenyezi Mungu,”amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi. 
 
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Aprili 16, 2023 katika kilele cha Mashindano ya Kimataifa ya Quran Tukufu katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Ameeleza kuwa,suala la kuzingatia maadili mema ni jukumu la kila Mtanzania. 

Pia amesema kuwepo kwa uvunjifu wa maadili katika jamii kunatokana na ukosefu wa malezi mema ya vijana na ukosefu wa elimu ya dini kwa baadhi yao.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran nchini, Sheikh Othman Ali Kapolo amesema, wamekuwa na mchango mkubwa wa malezi kwa Taifa kutokana na kuzalisha vijana wenye maadili mema kwa familia na Taifa kwa ujumla.
Amesema, mashindano yamekuwa na lengo la kukuza taaluma na kuendeleza maadili kwani tangu kuanzishwa kwa tunzo hiyo wameweza kuanzisha shule ya sekondari na msingi pia kituo cha afya huku akitoa rai kwa jamii kuunga mkono jitihada hizo. 

Naibu Mufti Sheikh Khamid Masoud Jongo kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania amesema, suala la maadili limekua janga kubwa, hivyo taasisi za dini zinapaswa kushirikiana kupiga vita janga hilo kwa kuhakikisha elimu ya dini inamfikia kila mtu.
Amesema, ili kuondoka na janga la mmomoyoko wa maadili jamii inapaswa kufanya kazi kwa bidii na kuepuka utegemezi, kwani umekuwa ukisababisha hasara kubwa kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, hivyo ili taifa lijitegemee linapaswa kuzalisha vijana wenye maadili na wachapakazi ili kuachana na utegemezi kwa wageni ambao wanaweza kuingiza mikataba itayoleta matatizo na kusababisha kuporomoka kwa maadili.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza vijana waumini wa dini ya Kiislamu kuisoma Quran na kushikamana kupitia mafunzo yake kwa kuleta tija kwa jamii na kuendelea kuyalinda maadili mema Kizazi cha sasa na kijacho. 

Mashindano hayo ya Tuzo za Kimataifa za Quran Mwaka 2023 yametimiza miaka 31 tangu kuanzishwa kwake yameshirikisha nchi zaidi ya kumi na tisa kutoka mabara tofauti na washiriki maalumu wa Adhana kutoka nchi tatu. 
Pia, Mheshimiwa Rais amemkabidhi zawadi kwa mshindi wa Kwanza Galal Saaed kutoka Yemen dola za Kimarekani elfu tano. 

Mshindi wa pili Abubaker Sharif kutoka Sweden dola za Kimarekani elfu nne. Mshindi wa tatu Abdul Biro kutoka Tanzania dola za Kimarekani elfu tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news