Rais Dkt.Mwinyi:Serikali itaendelea kuboresha maabara kupata matokeo sahihi ya vipimo

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuziboresha Maabara kwa lengo la kupata matokeo sahihi ya vipimo na tafiti za maabara nchini.

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika mkutano wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Maabara Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar.
Amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeamua kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika kuimarisha maabara kwa kuzipatia mashine na vifaa vya kisasa hali ambayo imesaidia kupunguza kupeleka sampuli kuchunguzwa nje ya nchi.

Mhe. Dkt. Mwinyi amesema, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuzishirikisha taasisi na kampuni binafsi katika utoaji wa huduma za Maabara za Afya katika Hospitali kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za maabara pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji.

Aidha, ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Maadhimisho ya Wiki ya Maabara Zanzibar kutapelekea kuwa na Jukwaa litakalowaunganisha wataalamu wa Maabara ndani na nje ya Nchi hatua ambayo itatoa fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu katika kufanya vipimo na majaribio mbali mbali ya tafiti.


Pia, ameeleza kuwa kuanzishwa na kuendelezwa Maadhimisho ya Wiki ya Maabara Duniani hapa Zanzibar kutapelekea kuimarika kwa vitengo na Jumuiya za Wataalamu wa Maabara za Afya nchini.

Akigusia suala la ajira kwa wataalamu wa Maabara, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa , Serikali itaendelea kuajira wataalamu hao kwa mujibu wa uhitaji na kueleza kuwa Hospital zilizopo na zinazoendelea kujengwa zinahitaji wataalamu hao ili wananchi wapate huduma bora, zenye urahisi na haraka.

Sambamba na hayo Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali kwa kutambua Afya za wananchi wake imeandaa mpango wa kuziboresha huduma za Maabara kwenye vituo vya mifugo na uvuvi ili ziweze kutoa nyama, maziwa na samaki wenye usalama kwa afya za binadamu.

Aidha, amewashauri Wataalamu wa Maabara za kilimo,mifugo na uvuvi kuandaa mipango mikakati ili kuleta mapendekezo ya kuziboresha maabara ili kuenda sambamba na dunia inayozungumza mkakati wa Sera ya afya moja.

Pamoja na hayo Rais Dkt. Mwinyi amewahakikisha wataalamu hao wa maabara kuwa Serikali italinda na kusmiamia maslahi yao ili kuendeleza kada hiyo pamoja na kuimarisha mazingira yao ya kazi.

Kwa upande wake Kaimu Waziri wa Afya Mhe. Riziki Pembe Juma ambae ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na watoto ameeleza kuwa kada ya Maabara ni muhimu kwa kuwa inatoa mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa Jamii kwa kuwahakikishia usalama wa Afya za wananchi.

Aidha, amewataka wataalamu hao kushirikiana na Wataalamu wengine kwa kutumia matokeo ya tafiti za Wataalamu hao ili kukuza ustawi wa Wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wataalamu wa Maabara Zanzibar (ZAMELSO), Hamad Bakar Magarawa ameeleza kuwa Zanzibar kwa mara ya kwanza imeungana na Nchi nyengine kwa kuadhimisha wiki hiyo ambapo itaweza kusaidia kukuza Kada hiyo nchini.

Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitembelea mabanda ya maonesho ya kazi za Maabara na kujionea juhudi mbali mbali zinazofanywa na wataalamu hao na kusifu hatua zilizofukiwa kupitia kada hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news