Rais Dkt.Samia atunukiwa Tuzo ya Heshima Sekta ya Elimu

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amepatiwa Tuzo maalum kwa ajili ya kuleta Mapinduzi katika Sekta ya Elimu nchini Tanzania.
Hafla ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanyika jana jijini Mwanza ambapo Umoja wa Maafisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri (REDEOA) wamemtunuku Tuzo hiyo maalum ambayo imepokelewa na Mhe. Angellah Kairuki, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEM kwa kutambua mchango wake mkubwa wa kusimamia, kuipaisha na kupelekea mapinduzi makuwa ya elimu nchini.

Katika hafla hiyo Waziri Kairuki amewataka Viongozi wa elimu nchini kutokuchoka kusimamia na kuyasemea masuala ya elimu kwani wao ndio waliopewa dhamana na Watanzania.

Kairuki amesema njia pekee ya kumsaidia Mheshiwa Rais Dkt. Samia Hassan ni kusimamia kwa weledi Sekta ya Elimu ambapo amewataka Viongozi hao kudumisha ushirikiano na wananchi pamoja na kuwawajibisha Viongozi wa elimu wanaoshindwa kutimiza wajibu wao.

“kila Afisa Elimu Mkoa na Halmashauri ahakikishe anadumisha ushirikiano na wananchi na Wadau wa elimu, anasimamia ufundishaji na ujifunzaji, wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaendelea kusaidiwa kwa ukaribu na kusimamia Miradi ya Maendeleo katika Sekta ya Elimu na Viongozi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao wanachukuliwa hatua bila kuwaonea na bila kuchelewa” amesema Kairuki.

Katika Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Sekta ya Elimu chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI imefanikiwa kwa kuandikisha wanafunzi wa awali 1,500,227 (109%), darasa la kwanza 1,767,586 (108%) na wanafunzi wa kidato cha kwanza walioripoti walikuwa 1,002,093 (93%).

Kwa mujibu wa Waziri Kairuki mafanikio mengine ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa 8,000 vilivyojengwa kwa shilingi Bilioni 160 ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi 1,076,402 waliofaulu na wote kuchaguliwa kwenda shuleni.

Aidha, kupitia Mradi wa GPE LANES mabweni 20 yamejengwa kwa shilingi Bilioni 2, mabweni 50 shilingi Bilioni 4 kwa mradi wa TCRP 5441 na mabweni 9 yamejengwa kwa shilingi milioni 960 kwa fedha za Uhuru mwaka 2022.

Naye Mwenyekiti wa REDEOA Germana Mng’ao ameishukuru Serikali kwa kurahisisha ufuatiliaji na usimamizi wa elimu nchini baada ya kupokea magari kwa ajili ya Mikoa na Halmashauri, pikipiki za Maafisa Elimu Kata na vishikwambi kwa walimu wote nchini.

Katika hafla hiyo mada mbalimbali ziliwasilishwa na pia Tuzo nyingine zilitolewa kwa Mheshimiwa Angellah Kairuki Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kusimamia Sekta ya Elimu Vizuri, Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Msonde, Mkurugenzi wa Elimu Ofisi ya Rais TAMISEMI Vicent Kayombo, Mwenyekiti wa REDEOA Germana Mng’ao na Afisa Elimu wa Mkoa wa Pwani Sarah Mlaki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news