Rais Dkt.Samia awapa kongole Simba SC, Yanga asema ahadi ya kila goli ipo pale pale

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amezipongeza klabu za Simba na Yanga za jijini Dar es Salaam kwa kuendelea kuiwakilisha vema Tanzania katika michezo ya Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo ikiwa ni saa chache baada ya Klabu ya Yanga ikiwa ugenini huko nchini Nigeria kuishushia kipigo cha mabao 2-0 klabu ya Rivers United Football Club.

Ni katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao umepigwa Aprili 23, 2023 katika Uwanja wa Venue Godswill Akpabio International mjini Uyo, Nigeria.

Ushindi huo ulitanguliwa na ule wa watani zao Simba SC ambao wakiwa nyumbani katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Aprili 22, 2023 waliichapa Wydad Athletic Club (Wydad Casablanca) kutoka nchini Morocco bao 1-0.

"Hongereni watani wa jadi Simba na Yanga kwa ushindi katika michezo yenu ya CAF (Klabu Bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho) wikiendi hii. Ahadi ya hamasa kwa kila goli bado iko pale pale. Endeleeni kutuwakilisha vyema. Nawatakia kheri,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Samia katika mitandao yake ya kijamii.

Ushindi wa Yanga SC, ulitokana na mabao mawili ya Fiston Mayele katika kipindi cha pili cha mchezo huo. Mayele alifunga bao la kwanza dakika ya 73, ingawa ilibidi refa Abongile Tom wa Afrika Kusini akajiridhishe kwenye VAR na la pili dakika ya 81 mara zote akimalizia pasi ya beki na nahodha, Bakari Nondo Mwamnyeto.

Aidha,kwa upande wa Simba SC dhidi ya Wydad Cassablanca katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, Jean Baleke aliwapatia Simba SC bao hilo pekee dakika ya 31 akimalizia pasi ya Kibu Denis kufuatia shuti la mpira wa adhabu uliopigwa na Saido Ntibazonkiza kuzuiwa na walinzi wa Wydad.

Aidha, kwa matokeo hayo, Simba SC wanasubiria mechi ya marudiano ambayo itapigwa nchini Morocco hivi karibuni huku Yanga SC nao wakitarajiwa kuumana na River United katika Dimba la
Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news