Rais Dkt.Samia, Kagame wakubaliana mema zaidi

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Rwanda zimekubaliana kufanya mageuzi katika sekta ya usafirishaji,kuimarisha biashara na uwekezaji katika nchi hizo mbili wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ustawi bora wa pande zote.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mhe.Paul Kagame wakati akimsindikiza Aprili 27, 2023 mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam.(Picha na Ikulu).

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Aprili 27, 2023 katika mkutano wa pamoja uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Rwanda,Mheshimiwa Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema biashara kati ya pande mbili haziakisi rasilimali nyingi zilizopo katika nchi hizo mbili, hivyo kuna haja ya kutumia miundombinu kukabiliana na changamoto hiyo.

Kuhusu suala hilo, amesema, lazima kuwe na mageuzi katika sekta hiyo ili nchi hizo mbili ziwe katika nafasi ya kunufaika na rasilimali zilizopo.

“Sasa tunaendelea kuimarisha bandari zetu, hasa Dar es Salaam na Tanga zinazotumiwa na Rwanda. Pia tumejadili jinsi ya kuimarisha njia nyingine za mawasiliano ili Tanzania iweze kutoa huduma bora kwa Rwanda na nchi nyingine zinazotuzunguka,"amesema.

Akitoa taarifa ya Mradi wa Umeme wa Rusumo uliopo kwenye mpaka wa pamoja wa Rwanda na Tanzania kwenye Mto Kagera unaoendelea,Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, unaendelea vizuri na wote wamekubaliana kuuzindua kwa pamoja. 
 
"Pia tumekubaliana vyombo vyetu vya usalama viendelee kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha usalama katika nchi zetu na ukanda wetu wa Afrika Mashariki,"amesema.

Mrejesho huo ambao umetolewa na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia akiwa na mgeni wake Rais wa Rwanda, Paul Kagame baada ya kufanya mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es Salaam pia amesema,ziara hiyo fupi ni muhimu zaidi.

“Tumepata ziara ambayo tulikuwa tukiisubiri kwa siku nyingi, Kagame anasema ziara fupi, lakini bora nimekuja kuliko nisingekuja, ni ziara fupi lakini yenye mafanikio, ziara imetupa muda mzuri wa kutathmini masuala ya ushirikiano.

"Katika mazungumzo yetu kuna mambo tumeyafanyia kazi, lakini hatujamaliza kwa hiyo tumekubaliana nchi zote mbili zikafanyie kazi kila moja na upande wake halafu watalaamu wetu wakutane na watuambie wamefikia wapi.

Naye Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame amesema kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mshirika mkuu wa Rwanda hasa kuhusiana na usafirishaji na uunganishaji wa biashara.

“Asante Dada yangu Samia Suluhu Hassan (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) kwa kuniwezesha kufika kwa ajili ya ziara hii ambayo ni fupi, mambo muhimu umeyasema Mimi nitazungumza kwa ufupi sana.

"Naomba uniruhusu nitumie Kiingereza, ingawa najitahidi kuzungumza Kiswahili kizuri ningependa kuzungumza Kiswahili kizuri kama chako, lakini bado kazi inahitajika.

"Mimi na Rais Samia tulikuwa na mazungumzo na tumekubaliana kudumisha uhusiano zaidi wa kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kihistoria, Tanzania na Rwanda zina mzizi mzuri wa ushirikiano wa muda mrefu.

"Tanzania ni mshirika mkubwa wa Rwanda hususani kwenye upande wa biashara, tunaheshimu kitendo cha Tanzania kukubali kudumisha zaidi ushirikiano huu kwa faida za mataifa yote mawili ili kuruhusu watu wetu kupata maendeleo ya haraka na kampuni zetu kushindana vizuri kwenye masoko ya Kimataifa.

"Mwisho Mheshimiwa Rais Samia nakushukuru kwa uongozi wako katika kutafuta suluhisho ya kudumu kwenye mgogoro ambao upo kwenye kanda yetu ya Afrika Mashariki hususani mgogoro tunaoshughulika nao Mashariki ya Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) ukishirikiana na viongozi wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

"Kujenga amani ya kudumu na usalama kwenye ukanda wetu tunahitaji kujitoa na kuwa na msimamo imara kwetu sote ikiwemo wale ambao wameathirika moja kwa moja na mgogoro huu.

"Amani na utulivu ni hitaji muhimu sana kwa ajili ya maendeleo na umoja wa Afrika, Mheshimiwa Rais kwa mara nyingine tena nakushukuru kwa mapokezi mazuri yanayotufanya tujisikie tuko nyumbani, asanteni sana,”amefafanua Mheshimiwa Rais Paul Kagame ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news