NAIROBI- Serikali ya Jamhuri ya Kenya imebainisha kuwa, uwekezaji mkubwa katika umwagiliaji endelevu utasaidia kukabiliana na tatizo la chakula nchini.
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, William Ruto amesema Serikali imetanguliza ujenzi na upanuzi wa mabwawa ili kuinua upya sekta ya kilimo.
Amebainisha kuwa, mabwawa yana nguvu kubwa ya kuchochea uzalishaji wa chakula, kwani yanapunguza utegemezi zaidi wa kilimo cha kutegemea mvua.
"Ikiwa tutazalisha chakula zaidi, inamaanisha mapato zaidi kwa wakulima wetu na ajira zaidi kwa vijana wetu," alisema Rais.
Mheshimiwa Rais Dkt.Ruto aliyasema hayo hivi karibuni huko Fulugani, Kaunti ya Kwale, wakati wa uwekaji msingi wa ujenzi wa Bwawa la Mwache.
Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, Waziri wa Maji Alice Wahome, Waziri wa Utumishi wa Umma,Aisha Jumwa, Waziri wa Madini, Uchumi wa Bluu na Masuala ya Bahari, Salim Mvurya, Magavana Fatuma Achani (Kwale), Abdullswamad Nassir (Mombasa) na Andrew Mwadime (Taita Taveta) ni miongoni mwa viongozi walioshiriki hafla hiyo.
Ukitarajiwa kukamilika Agosti 2026, mradi huo wa shilingi Bilioni 18 za Kenya utatoa maji ya kumwagilia angalau ekari 7,000 za ardhi huko Kwale, na kuzalisha chakula cha thamani ya shilingi Bilioni 1.3 kwa mwaka.
Rais Ruto alisema bwawa hilo litatoa zaidi ya lita milioni 230 za maji kwa siku kwa umwagiliaji na matumizi ya nyumbani.
"Hii itafanufaisha angalau watu milioni 1.6 katika Kaunti za Kwale na Mombasa." Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka hadi milioni 2 ifikapo 2030.
Serikali ina mpango wa kujenga mabwawa makubwa 100 na madogo 1,000, na hivyo kuongeza ekari zinazochimbwa na umwagiliaji kutoka 670,000 za sasa hadi milioni tatu."Umwagiliaji ni hatua ya mageuzi zaidi tunayoweza kufanya katika kilimo."
Kwa upande wake Gavana wa Kwale, Fatuma Achan alisema wamelenga kutimiza ahadi zao za kabla ya uchaguzi. "Hatutashiriki katika maonyesho ya kando kama maandamano ya hivi majuzi, hayaongezi thamani yoyote katika maisha ya watu,"alibainisha.