NA BENNY MWAIPAJA-WFM
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Dunia, Bw. David Malpass, na kujadiliana masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Serikali na benki hiyo, yatakayoiwezesha nchi kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Aidha, Bw. Malpass alihamasisha juhudi zaidi katika kulinda uwekezaji wa sekta binafsi kwa kuwa ni nguzo katika kukuza uchumi na kushauri Sekta binafsi kupewa kipaumbele katika kusukuma ajenda ya maendeleo jambo ambalo litachochea uzalishaji, kuongeza ajira pamoja na kuboresha Maisha ya watu.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Rais Malpass, kwa kuisaidia Tanzania kutimiza agenja zake mbalimbali za Maendeleo katika kipindi chake cha uongozi kama Rais wa Benki ya Dunia.

Alisema katika kipindi chake cha uongozi, Bw. Malpass ameimarisha ushirikiano wa Benki ya Dunia na Tanzania na kumfahamisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki ya Dunia, Tanzania imepata fedha za mkopo nafuu na misaada mbalimbali iliyosaidia kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kimkakati.
