NA FRESHA KINASA
JIMBO la Musoma Vijijini lililopo katika Mkoa wa Mara limeamua kujidhatiti kujenga maabara tatu za masomo ya sayansi kwenye kila sekondari ya kata.
Maabara hizo ni za Physics, Chemistry na Biology hatua ambayo inalenga kuwaandaa wasomi wa sayansi watakaoleta mageuzi chanya kwa uchumi wa kisasa nchini.
Hayo yamebainishwa Aprili 24, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo. Ambapo taarifa hiyo imeeleza kuwa,jimbo hilo lenye kata 21 lina sekondari za kata 25 na za binafsi mbili. Ambapo sekondari tatu tu kati ya 25 ndizo zina maabara tatu, zingine zinazo mbili au moja.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Sayansi ni muhimu sana katika kuchagiza maendeleo ya taifa lolote na ikaeleza kuwa yapo mataifa ulimwenguni ikiwemo China, India na Brazil yanaendana na uwekezaji mkubwa kwenye Sayansi.
"Sekondari mpya zinazoendelea kujengwa na wanavijiji lazima ziwe na maabara hizo.Kwa hiyo, fedha zote za Mfuko wa Jimbo, zinatumika kwenye ujenzi wa maabara hizo.
"Mtiro Sekondari Sekondari ya Kata ya Bukumi yenye vijiji vinne vya Buira, Bukumi, Buraga na Busekera. Ilifunguliwa mwaka 2006, haina maabara hata moja.
"Wanafunzi wa Mtiro Sekondari jumla ni 681,Jumla ya Walimu wa ajira ya Serikali ni 13, na wanne ni walimu wa muda (kujitolea) wanaopewa posho kutoka kwa wazazi wenye watoto shuleni hapo.
"Mwitikio wa masomo ya sayansi, walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi ni wanne, walimu wanaofundisha Hisabati ni wawili. Jumla ya Wanafunzi wa kidato cha III ni 110 ambapo 14 wanasoma Physics, 17 wanasoma Chemistry, 110 wanasoma Biolojia kwa kulazimika.
"Jumla ya wanafunzi wa kidato cha IV ni 123, 21 wanasoma Physics, 26 wanasoma Chemistry, 123 wanasoma Biology kwa kulazimika,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.
FAIDA ZA MAABARA
Takwimu hizo hapo juu zinaonesha mwitikio mdogo sana wa wanafunzi wetu kupenda kusoma masomo ya Sayansi.Kuwepo kwa Maabara za Masomo ya Sayansi ni muhimu kwa kufundishia na kwa kujifunza, hasa kwa vitendo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mtiro Sekondari wanajenga maabara tatu za masmo ya sayansi ambapo Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof.Sospeter Muhongo, alipiga harambee ya ujenzi wa maabara tatu za masomo ya sayansi, na matokeo ni michango ifuatayo:
"Wanavijiji wa vijiji vinne michango inaendelea kutolewa ikiwemo nguvukazi ya kuchimba misingi,mchanga tripu 27, kokoto tripu mbili,saruji mifuko nane,fedha taslimu shilingi 1,508,000 huku wazaliwa wa Kata ya Bukumi na wadau wengine wakitoa shilingi 1,500,000,"imeongeza taarifa hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Muhongo ametoa saruji mifuko 150 ambapo ameanza kwa kutoa mifuko 75 na Mfuko wa Jimbo ambaye Mwenyekiti ni Mbunge wa Jimbo saruji mifuko 200, na nondo 49.
MAOMBI
Halmashauri ya Musoma DC ianze kuchangia ujenzi wa maabara za Masomo ya Sayasi kwenye Sekondari zake za kata, isisubiri kufanya kazi ya kuratibu fedha zinazotolewa na Serikali Kuu.
"Wazaliwa wa Musoma Vijijini waanze au waendelee kuchangia sekondari za kata za kwao kwenye ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi na maktaba.
"Sayansi ni kila kitu.Uchumi wa kisasa unahitaji Sayansi na mafanikio makubwa ya kiuchumi ya China, India na Brazil yanaendana na uwekezaji mkubwa kwenye Sayansi," imeeleza taarifa hiyo.