Serikali yaahidi kuendelea kuiwezesha TAZARA

NA DIRAMAKINI

NAIBU Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete amesema Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuwekeza kwenye Shirika la Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuhakikisha shirika hilo linapata faida na kuweza kujiendesha.
Akizungumza katika tukio maalum la kuwakumbuka wahandisi na watumishi mbalimbali waliofariki wakati wa ujenzi wa reli hiyo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri Mwakibete amesema, mchango walioutoa katika ujenzi wa reli unathaminiwa hivyo Serikali itaendelea kuutambua kwa kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa kutimizwa kiutendaji yanafikiwa.

“Reli hii iliasisiwa na viongozi wetu Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Dkt. Kenneth Kaunda aliyekuwa Rais wa Zambia kwa kushirikiana na China, hivyo njozi yao ya uanzishwaji wa reli hii hatutaiacha iende hivi kwa kuangalia shirika hili likijiendesha kwa hasara wakati wao walihakikisha shirika linakuwepo na linakuwa na malengo ya kusafirisha mzigo na abiria kwa Tanzania na Nchi Jirani zinazotuzunguka,"amesema Naibu Waziri Mwakibete.

Naibu Waziri Mwakibete amesema Serikali za Tanzania na Zambia kwa kushirikiana na Serikali ya China wako katika hatua mbalimbali za kutatua changamoto zilizopo kwa sasa ili kuhakikisha uwekezaji unaowekwa kwa pamoja unakuwa na tija kwenye miundombinu na mtaji.

Naye Mshauri wa Waziri kutoka Ubalozi wa China Nchini, Suo Peng amemuhakikishia Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, kuwa nchi hiyo iko tayari wakati wote kuhakikisha shirika hilo linaboreshwa kwani lilidhamiria kusaidia kwenye ujenzi hivyo hakuna sababu ya kushindwa kulisaidia kwenye kipindi hiki cha maboresho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAZARA, Mhandisi Bruno Ching’ amesema TAZARA inatekeleza mpango wake wa muda mrefu na mfupi ambapo kwa sasa tayari kuna kampuni ambazo zinashirikiana nazo ili kuhakikisha uwekezaji unaoendelea kuwekwa unakuwa na faida.

Siku ya kuwakumbuka watendaji mbalimbali walipopoteza maisha katika ujenzi wa reli ya TAZARA huadhimishwa Aprili Mosi ya kila mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news