NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imefafanua kuwa Serikali haioni haja ya kufanya marekebisho ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ili kurejesha kwa Wananchi eneo walilokuwa wanatumia kwa ufugaji wa nyuki na mifugo Wilayani Urambo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo Aprili 18, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Urambo, Mhe. Margaret Sitta aliyetaka kujua lini Serikali itafanya marekebisho ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla ili kurejesha kwa Wananchi eneo walilokuwa wanatumia kwa ufugaji wa nyuki na mifugo – Urambo.
Amesema kuwa Hifadhi ya Taifa Ugalla ni muhimu kiuhifadhi na ndani yake kuna vyanzo vya maji.
Amefafanua kuwa uwapo wa shughuli za kibinadamu katika eneo la hifadhi hiyo ilileta changamoto za kiuhifadhi ikiwemo uchomaji moto unaoathiri uoto wa asili na uchafuzi wa vyanzo vya maji hivyo, Serikali haioni haja ya kufanya marekebisho ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla.
Aidha, amesema kuwa Serikali itaangalia namna bora ya kupata eneo lingine kwa ajili ya shughuli za ufugaji nyuki.