Serikali yasisitiza mradi wa maji Mugango na Tegeruka ukamilike, Prof.Muhongo na wananchi wamshukuru Rais Dkt.Samia

NA FRESHA KINASA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maji imemtaka mkandarasi kampuni ya Kiure Engineering Ltd kukamilisha kazi ya mradi wa maji wa Mayani-Tegeruka-Kataryo utakaonufaisha wananchi wa Kata ya Mugango na Tegeruka kwa kuzingatia muda wa mkataba ili kuhakikisha wananchi wananufaika na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yao.

Mradi huo ni mwendelezo wa mradi mkubwa wa maji wa Mugango-Kiabakari Butiama. Wito huo umetolewa leo Aprili 13, 2023 baada ya kusainiwa kwa mkataba wa kiasi cha shilingi bilioni 4.7 kati ya mkandarasi huyo na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MUWASA) ambao ndio wasimamizi wa mradi ili kuvifikia vijiji sita vya kata hizo vinufaike na huduma hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kusainiwa mkataba huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema, hakuna sababu za kuongeza muda nje ya mkataba katika utekelezaji wa mradi kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha mkataba huo unatekelezwa kwa muda uliopangwa.

Amebainisha kuwa, mkataba ni miezi sita ili mradi ukamilike na sio vinginevyo katika kuhakikisha dhamira na shabaha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan inazidi kuendelea kutekelezeka kwa vitendo ya kumtua mama ndoo kichwani. 
Ameongeza kuwa, fedha zipo ndio sababu mkataba umesainiwa, hivyo hakuna sababu za kucheleweshwa kwa mradi huo ambao unasubiriwa kwa hamu na wananchi.

Amebainisha kuwa, Wizara ya Maji imejipanga vizuri kuwawezesha wataalamu wake kusudi wawe na madhubuti wa usimamizi mzuri wa miradi.

"Muwasa mmeona wamesaini mkataba leo na Wizara inawaamini katika usimamizi wa miradi na hata huu watamsimamia vizuri mkandarasi ili aweze kutekeleza kwa wakati,"amesema.

Aidha, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo kwa ufuatiliaji wa mradi katika kuhakikisha wananchi waliomchagua wananufaika na kuondokana na tatizo la maji kwani maji ni muhimu kwa maendeleo. 
Naye Mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amemshukuru Rais Dkt.Samia Hassan na Serikali kwa ujumla kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya mradi huo ambapo amesema wananchi wanapokea kwa mikono miwili na kwa moyo wa upendo kutoka kwa Rais Samia ambaye tangu aingie madarakani ameonesha ushupavu, upendo na kuwajali kwa dhati Watanzania na wana-Musoma Vijijini kupitia fedha ambazo amekuwa akitoa za miradi ya maji na miradi mingine. 

Prof. Muhongo amesema, kwa sasa katika vijiji vyote 68 ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini ipo miradi ya maji ambayo inaendelea na mingine imekamilika na wananchi wanapata hudima ya maji. 

Catherine Peter mkazi wa Kata ya Mugango ametoa pongezi kwa Rais Dkt.Samia na Mbunge Prof.Muhongo kwa kuwajali wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini ambapo amesema miradi ya maji inayotekelezwa jimboni humo inamanufaa makubwa hasa kwa kina mama ambao ndio hupoteza muda mwingi wakitafuta maji na kushindwa kufanya kazi za maendeleo.
"Huu ni ni upendo mkubwa wa Rais wetu Dkt.Samia pamoja na Mbunge Prof. Muhongo kwa wananchi, lazima tushukuru kuona neema hii miradi ya maji ikifanyika wanawake huko nyuma tulipata mateso sana kutembea na ndoo usiku kucha tukitafuta maji, lakini tangu Rais aingie madarakani tunaona miradi ya maji kupitia RUWASA mingine tayari inahudumia wananchi, na mradi mkubwa kabisa wa Mugango-Kiabakari-Butima pamoja na mradi huu Mungu awabariki sana,"amesema Catherine Peter.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news