Simba SC yakabidhiwa milioni 5/- za motisha kutoka kwa Rais Dkt.Samia

NA DIRAMAKINI

KLABU ya Simba ya jijini Dar es Salaam imeendelea kujichotea fedha za ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kununua kila bao la klabu hiyo katika michuano inayoendelea ya Kimataifa.

Leo Aprili 22, 2023 baada ya ushindi wa bao moja waliopata dhidi ya Wydad Casablanca katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika wamekabidhiwa shilingi 5,000,000 ikiwa ni sehemu hiyo ya motisha kutoka kwa Rais Dkt.Samia.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amekuwa akitoa kiasi hicho cha fedha kwa kila bao wanalofunga kwenye michuano hii ili kuongeza morali kwa timu za Tanzania kufanya vizuri.

Fedha za leo amekabidhiwa nahodha, John Bocco na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Tulia Akson ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mchezo wetu.

Katika mchezo uliopita wa nyumbani dhidi ya Horoya kutoka Guinea, Simba SC walikabidhiwa shilingi milioni 35 baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0.

Katika mchezo huo uliopigwa leo katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Simba SC iliwazidi ujanja wageni wao.

Mchezo ulianza kwa kasi, ambapo pande zote zilionekana kushambuliana kwa zamu huku mpira ukichezwa zaidi katikati ya uwanja na timu zikionekana kucheza kwa tahadhari.

Jean Baleke aliwapatia Simba SC bao hilo pekee dakika ya 31 akimalizia pasi ya Kibu Denis kufuatia shuti la mpira wa adhabu uliopigwa na Saido Ntibazonkiza kuzuiwa na walinzi wa Wydad.

Kipindi cha pili,Simba SC walirudi kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Wydad, lakini mabingwa hao wa Afrika walikuwa watulivu zaidi kwenye eneo lao la ulinzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news