SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-11

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...rasmi Padri Samson Mcjohn akawa ametangazwa kuwa kiongozi mkuu wa wachawi kanda yote ya Magu na eneo dogo la Simiyu.

Endelea

Baada ya mtoto THE BOMBOM kuchukuliwa na kile kimbunga, usiku huo alipelekwa Kijiji cha Ihushi karibu na mji wa Kisesa.

Mji huu upo upande wa kulia mwa barabara, ukiwa unatokea Magu mjini. Ukivuka mji wa mikoroshini mbele yake utafika mji wa Isangejo kisha unapinda kulia kuiacha barabara iendayo Kisesa.

Kwa mwendo wa gari ni dakika kumi unafika kwenye kijiji hicho. Ndani ya kimbunga kilichonibeba kulikuwa na bibi wawili niliokuwa siwafahamu.

Wakati tunaelekea kwenye mji huo hatukufuata barabara, ndiyo maana tuliwahi kufika kijijini hapo. Zipo tofauti kubwa baina ya kimbunga cha kawaida na kile cha kutengeneza.

Kwa kawaida kimbunga cha kutengeneza hupeperusha takataka nyingi, kipenyo cha mduara wake ni mdogo sana kutegemea na ukubwa wa kigoda cha duara kilichowekwa.

Kimbunga cha kutengeneza huwa hakifuati njia za binadamu hata kidogo pia ni vigumu sana kupita katikati ya mji wa mtu labda kuwe na lengo fulani.

Kimbunga hicho kilikwenda kuishia kwenye kijimlima kilichopo kando ya mji huo wa Ihushi. Kwa macho ya kawaida mlima huo ulionekana ni wa kawaida, lakini haukuwa wa kawaida hata kidogo.

Ilikuwa ni makao makuu ya wachawi wa ukanda wa Kisesa, kulikuwa na majengo mazuri na ya kisasa. Ilikuwa ni kambi kubwa kiasi chake iliyokuwa na kila kitu cha kichawi.

Wale bibi vizee walimpeleka kwenye jengo fulani mtoto huyo, ndani ya jengo hilo aliwakuta wachawi wengine wa kike na kiume.

Walikuwa katika mkao wa kusubiri jambo, walipoingia chumbani humo alishangaa kuwaona wanasujudu mbele zake. Walimchukua na kumpeleka mbele ya kiongozi wao, yule kiongozi alisimama na kumsogelea karibu zaidi.

Mkononi alikuwa na kifaa kidogo mfano wa wembe, kifaa hicho kilikuwa na makali pande zote mbili. Kiongozi hiyo alimshika mkono mtoto THE BOMBOM na kumsogeza katikati ya chumba hicho.

Walipofika katikati ya chumba alimkalisha kitako, mtoto huyo alitii na kusubiri kuona kilichokuwa kikiendelea. Kiongozi huyo wa wachawi alimshika kichwani mtoto huyo kisha akamchanja utosini. Baada ya hapo na yeye alijichanja mkononi mwake kwa nyuma ya kiganja chake.

Damu ilipoanza kuchuruzika yule kiongozi aliiweka kwenye jeraha la mtoto THE BOMBOM. Kukawa na mwingiliano baina ya damu yake na ile ya mtoto, kitendo hicho kilimshangaza sana mtoto THE BOMBOM.

Baada ya muda mchache kiongozi huyo aliwaruhusu wachawi wengine kuendelea na utaratibu huo. Kila mchawi alijichanja kama alivyofanya kiongozi wao kisha akafanya upatanisho wa damu baina yake na mtoto.

Shughuli hiyo ilipomalizika walimchukua mtoto huyo na kumpandisha kwenye kiti cha utawala. Wachawi hao walishangilia sana kufanikisha jambo hilo, hapo ndipo mtoto huyo aligundua namna alivyokuwa akihitajika katika jamii ya kichawi.

Walimfanyia mazindiko ya kutosha ya kumlinda na balaa lolote, walipotosheka na madawa yao waliamua kumrudisha nyumbani kwao.

Alifikishwa nyumbani kwao muda wa saa tisa na nusu, mle chumbani alishangaa kuuona mwili wa bibi yake aliyeuawa kule shereheni.

Kwa kuwa kazi ya kichawi ilikuwa ni sehemu ya maisha yake alijikaza kisabuni. Ilipofika asubuhi yule maiti bibi wa mtoto THE BOMBOM alisimama na kutoka nje, pale nje alisalimiana na ndugu na jamaa kisha akawa anafanya kazi fulani.

Ghafla kichwa chake kilianza kumuuma, alimuita mmewe na kumuelezea namna alivyokuwa akijisikia. Kadri muda ulivyokwenda ndivyo maumivu yalivyokuwa yakiongezeka, ghafla alidondoka chini akawa anatokwa damu masikioni na puani.

Walimchukua na kumpakiza kwenye mkokoteni unaovutwa na ng'ombe wampeleke hospitali, kabla hawajafika hospitali alifariki.

Kwa upande wa mtoto THE BOMBOM hakukuwa na jipya, kisa halisi cha kifo cha bibi yake alikuwa anakifahamu. Siku zote mtu akiuawa katika shughuli za kichawi, lazima atapewa uhai wa muda ili aonekane amekufa kihalali. Mara nyingi watu wa namna hii sababu za vifo vyao huwa ni kuumwa vichwa. Lengo lake ni kuipumbaza jamii ili iamini kuwa ndugu yao amekufa halali kumbe kuna nguvu za giza.

Maziko yalifanyika baada ya siku tatu pale nyumbani, kila siku wachawi wa maeneo mbalimbali waliokuwa karibu na bibi huyo walikuja.

Vikao mbalimbali vya kichawi vilifanyika nyumbani hapo wakati wa usiku, mtoto THE BOMBOM alihudhuria vikao hivyo kama mwanachama mwenzao.

Katika vikao hivyo hoja kubwa ilikuwa ni namna ya kulipa kisasi dhidi ya Padri huyo na kundi lake. Hoja mbalimbali zilizungumzwa juu yake, miongoni mwa makundi yaliyokuwa yakimpiga vita Padri huyo ni pamoja na kundi hilo la wachawi wa Ihushi.

Baada ya maziko maisha yaliendelea kama kawaida, kila siku usiku mtoto THE BOMBOM alikwenda kijiji cha Ihushi kujishughulisha na majukumu yake ya kichawi.

Kambi hiyo iliendelea kumlea mtoto huyo kimadawa siku baada ya siku, wakati wa masomo mtoto huyo aliendelea kuhudhuria kama kawaida.

Licha ya kuwa na umri wa miaka minne, lakini aliongoza darasani. Walimu na wanafunzi walimpenda sana, alikuwa ni mwanafunzi mpole asiye na makuu kwa wenzie.

Siku moja akiwa darasani mwanafunzi mwenzake alidondoka chini, damu zikawa zikimchuruzika puani na mdomoni. Wanafunzi wenzie walipiga kelele wakitaka msaada, mwalimu Nyambocha, Mhele, Tosiri na Lyatula walifika haraka darasani.

Walimchukua mtoto huyo na kumtoa nje ya darasa karibu na viunga vya shule. Damu ilikuwa ikiendelea kuchuruzika, aliitwa kaka mkuu akaulizwa chanzo cha tatizo hilo.

Katika maelezo yake alisema hakuwa na maelezo zaidi ya kumuona mtoto huyo akitiririkwa damu. Ndugu msomaji miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakimdharau mtoto THE BOMBOM alikuwa ni huyo, siku hiyo alikuwa kaamua kumshikisha adabu.

Hali ya mtoto huyo haikuwa nzuri hata kidogo, alianza kuharisha damu na kutapika pia. Hapa niseme kidogo, siku zote mchawi hawezi kukuloga pasipo sababu. Haijalishi sababu hiyo ni ndogo kiasi gani, yeye hupatia pa kukamilisha malengo yake.

Walimu waliamua kumuita mwalimu Sifan aje amuombee mwanafunzi huyo, mwalimu huyo alijulikana shuleni hapo kwa kuombea wagonjwa mbalimbali.

Alikuwa ni muamini wa kanisa la African Inland Church (AIC), sehemu zingine kanisa hili linajulikana kama kanisa la Wasukuma kwa kuwa idadi ya watu wanaosali ni kabila hilo.

Mwalimu aliomba mpaka akachoka, lakini hali ya mtoto iliendelea kuwa mbaya, walipiga simu kituo cha afya cha Ilungu kuomba msaada wa gari la wagonjwa.

Kabla gari la wagonjwa halijafika mtoto THE BOMBOM,alitoka nje akaelekea kwenye kiunga kilichokuwa amelazwa mgonjwa huyo.

Idadi ya walimu ilikuwa imeongezeka, walionekana kuumia sana kupitia ugonjwa waliokuwa wakiuona kwa mtoto huyo.

Hatimaye mtoto THE BOMBOM alifika eneo hilo, alimsogelea mwanafunzi huyo kisha akamshika kichwani. Alifumba macho akawa ananuia masuala ya kichawi ili kumponya mgonjwa, punde si punde ule ugonjwa ulikoma.
Hakukuwa na damu wala mwenzie na damu, yule mwanafunzi alisimama na kumshukuru mtoto THE BOMBOM. Walimu na wanafunzi walipigwa na butwaa kwa miujiza ya uponyaji uliyofanywa na mtoto huyo. Walilisifu jina la bwana kwa kufanya miujiza kupitia mtumishi wa bwana mtoto THE BOMBOM.

Walimu na wanafunzi walijenga imani kubwa kwa mtoto huyo, matatizo mbalimbali yaliyokuwa yakitokea shuleni hapo walimfuata mtoto huyo.

Asilimia kubwa ya matatizo hayo yalisababishwa na mtoto mwenyewe, ndiyo maana aliweza kuyatatua kirahisi kila alipoitwa.

Shuleni wanafunzi wenzake walianza kumuita nabii wa Mungu, baadhi ya watu walianza kupindisha mistari iliyoko kwenye Bibilia na Quran.

Kwa kuwa mtoto huyo alikuwa kajijengea umaarufu mkubwa baadhi ya watu hawakumpenda. Miongoni mwa watu waliokuwa wakimchukia ni mmoja wa waheshimiwa wilayani Magu.

Baada ya habari za kushangaza za mtoto huyo kuenea, wagonjwa mbalimbali walikuwa wakiletwa shuleni hapo kupewa uponyaji.

Walimu waliletewa maelekezo toka ofisi ya elimu wilaya. Maelekezo hayo yalikuwa yakipinga wagonjwa hao kuja shuleni hapo kupokea upako toka kwa mtoto huyo.

Kwa kuwa jamii kubwa imeghubikwa na matatizo walipuuza katazo hilo wakawa wanamsubiri mtoto huyo karibu na bohari la pamba la Ilongo jineri.

Siku moja asubuhi na mapema mheshimiwa huyo alifika shuleni hapo, aliambatana kamati yake. Ulikuwa ni msafara mkubwa wenye viongozi wakubwa wa wilaya, walifika shuleni hapo saa moja kamili.

Hawakutoa taarifa kwa afisa elimu kata wala kwa mwalimu mkuu, juu ya ujio wao shuleni hapo. Hata mtendaji wa kata au kijiji hakuwa na taarifa ya ugeni huo.

Mbali ya kutotoa taarifa juu ya ujio huo, mtoto THE BOMBOM alitambua ujio huo mapema na akamuelezea Mwalimu Mkuu.

Mwalimu huyo aliwataarifu walimu wake kisha wakafanya maandalizi ya ugeni huo kiutendaji. Kwa hiyo siku hiyo walimu hawakuwa na shaka juu ya ugeni huo, kilifanyika kikao cha walimu na kamati hiyo.

Walimu wote walielezea umuhimu wa mtoto huyo kuwepo shuleni hapo, walifafanua kwa mapana msaada uliokuwa ukitolewa na mtoto huyo shuleni hapo.

Hatimaye, mkuu huyo aliagiza kuletwa mtoto THE BOMBOM kikaoni hapo, baada ya kuletwa kikao kiliendelea. Katika hali ya kawaida ilikuwa ni vigumu kuamini mambo yaliyokuwa yakizungumzwa ukilinganisha na umri wa mtoto huyo.

Mheshimiwa huyo hakumpenda hata kidogo mtoto huyo, alitamani kumfuta hata shule, lakini miongozo ya elimu haikumruhusu.

Alitamani kumpiga risasi mtoto huyo, lakini alishindwa kulingana na uwepo wa watu maana hakuwa juu ya sheria. Ndugu msomaji chuki za mheshimiwa huyo zilikuwa na mizizi yake toka kwa Padri Samson Mcjohn.

Baada ya mtoto huyo kutoroshwa mikononi mwa Padri huyo kwenye uwanja wa shule ya msingi Gw'atelesha. Alifanya mawasiliano na taasisi za kichawi nchini kwake Urusi, walipoangalia kwenye njia zao za madawa waliona kuwa nabii wa kichawi aliyetabiriwa vizazi na vizazi alikuwa ni mtoto THE BOMBOM.

Kuzaliwa kwake, kulelewa kwake hadi kusoma kwake na miujiza mingine ilikuwa ndiyo yenyewe. Hivyo njia pekee ya kuzima ndoto hiyo ilikuwa ni kumuua, fedha mbalimbali zilitumwa kwa Padri huyo ili kufanikisha jambo hilo. 

Padri aliamua kumhonga mheshimiwa huyo kiasi kikubwa cha fedha ili kiukamilisha hitaji hilo, walimtangulizia fedha za awali, zikasalia zingine. Yote haya mtoto THE BOMBOM alikuwa akiyafahamu kwa kina na mapama.

Yule mheshimiwa alimtupia swali mtoto huyo. Unaitwa nani? Yule mtoto alikaa kimya kwa muda kitambo kisha akajibu " Naitwa Bilioni tatu baba yangu ni bilioni mbili na babu yangu ni bilioni tano kwa upande wa mama yangu anaitwa Rushwa Mzungu.

Majibu yale hayakueleweka kwa watu waliokuwa kwenye kikao, lakini yalimkata maini mheshimiwa. Hakuamini kilichouwa kikizungumzwa na mtoto huyo, macho yalimtoka.

Ndugu msomaji mambo yameiva, unadhani nini kitampata mheshimiwa huyo. Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua.

LYANGOSHA

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news