SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-12

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...majibu yale hayakueleweka kwa watu waliokuwa kwenye kikao,lakini yalimkata maini mheshimiwa yule kutoka wilayani. Hakuamini kilichokuwa kikizungumzwa na mtoto huyo, macho yalimtoka.

Endelea

Mheshimiwa yule kutoka wilayani alijikaza kisabuni kutokana na majibu aliyopewa, hakutegemea kabisa kama angepata majibu ya namna hiyo toka kwa mtoto huyo.

Majibu ya mtoto huyo yalionesha kuwa alikuwa na uelewa mkubwa juu ya rushwa aliyokuwa kapewa na yule Padri. Majina aliyoyataja mtoto huyo yalisadifu habari nzima ya rushwa aliyopewa na mzungu yule, kengele ya hatari iligonga kichwani mwake.

Mwalimu mkuu, alishabaini hasira kali iliyokuwa machoni mwa mheshimiwa yule kutoka wilayani, mishipa yake ya shingo ilimsimama mithili mcheza mieleka.

Macho yake yalikuwa mekundu mfano wa kaa la moto, meno yake akawa anayasaga taratibu huku akijitahidi kuizuia hasira yake.

Mwalimu mkuu akarusha kete yake akiwa na lengo la kutuliza hali ya hewa maeneo hayo. "Waheshimiwa wakuu wangu, kwa niaba ya wanafunzi na walimu ninaomba radhi kwa majibu ya mtoto huyu.

"Pengine swali hakulielewa au amepitiwa tu, mtoto huyu ni miongoni mwa watoto waliotoa mchango mkubwa katika maendelea ya shule. Mtoto huyu ana kipawa alichojaliwa na Mwenyezi Mungu, hebu fikiri kwa umri wake wa miaka minne tu, lakini yupo darasa la sita.

"Ni mwanafunzi ambaye tumekuwa naye hapa shuleni kwa muda mfupi sana, lakini hata hivyo darasa la sita anaongoza kitaaluma. Chondechonde wakuu zangu, ninawaomba tushirikiane kumsaidia mtoto huyu, pengine anaweza kuwa msaada mkubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

"Kipawa kingine alichonacho mtoto huyu ni kutabiri mambo yajayo, wakuu zangu hamuwezi kuamini hata ujio wenu alituambia wiki nne kabla ya leo. Kwa hiyo tulijua kuwa leo tungekuwa na ugeni wenu, yote hiki ni kipawa alichopewa mtoto huyu na Mungu.

"Amekuwa msaada mkubwa kwa jamii na shule, amekuwa akitoa tiba kwa wanafunzi na walimu wagonjwa. Amekuwa akisaidia hata jamii kwa kuwatibu kwa maneno tu ya kutamka uponyaji unafanyika, nadiriki kusema yamkini ni miongoni mwa manabii wa Mungu,"Mwalimu mkuu alihitimisha maelezo yake yaliyokuwa yamejaa ukweli mtupu, hakika ilikuwa kweli tupu.

Wakati huo mtoto THE BOMBOM alikuwa katulia tuli mithili ya maji mtungini. Kwa upande wa mheshimiwa yule kutoka wilayani alikuwa kajawa na jakamoyo kifuani mwake, kila alipomtazama mtoto huyo gagasiko lilitamalaki moyoni mwake.

Lengo lake kuu ilikuwa ni kukamilisha adhima aliyokuwa katumwa na yule Padri, yaani kukwamisha mipango yote ya mtoto THE BOMBOM.

Alikuwa ameshazunguka mbuyu si kwa thamani ya vipande thelathini kama simulizi za Yuda kwa Yesu, bali alikuwa kajikusanyia kibindoni bilioni tatu.

Kamanda wa polisi wilaya alipata wasaa wa kuuliza swali, kamanda huyu alikuwa ni miongoni mwa askari polisi waungwana.

Alianza kwa kusema "Unaitwa nani mwanangu? Unaweza kutuelezea kwa kifupi historia ya maisha yako? Hizi habari zinazozungumzwa na jamii juu yako ni sahihi?" Yalikuwa ni maswali matatu ambayo ndani yake yangesaidia kumuelewa vyema mtoto huyo.

Mtoto THE BOMBOM alikohoa kidogo kusafisha koo lake, kisha akaanza kujieleza huku akiwa katulia. "Naitwa THE BOMBOM jina nililopewa na ukoo wangu baada ya kushindanishwa kwa majina mengi. Jina hili ni utambulisho kama yalivyo majina mengine, katika maisha yangu sikuwahi kumuona baba wala mama kwani baba aliuawa siku aliyombaka mama.

"Mama yangu alikuwa na tatizo la afya ya akili yaani alikuwa kichaa, baada ya kubakwa utungisho ulifanyika siku hiyo. Kama ilivyoada baada ya miezi tisa nilizaliwa, kama vitabu mbalimbali vilivyotabili mama alikufa siku hiyo. Baada ya hapo nimekulia kwenye malezi ya babu na bibi kizaa mama, miezi michache iliyopita nimempoteza bibi yangu kipenzi na kubakia na babu,ko! ko! ko! (alikohoa kidogo kisha akaendelea).

"Kitu pekee mlichokuwa hamkifahamu ni juu ya uwezo ulioko mwilini mwangu, ndugu zangu mimi ni nabii wa bwana.

"Vitabu mbalimbali vya wenye akili vilitabiri kuzaliwa kwangu, wenye akili kutoka mataifa ya watu mbalimbali wanasubiri kuzaliwa kwangu.

"Vitabu hivyo vilitabiri kuwa Afrika itapata nabii atakayekuwa msaada mkubwa kwa dunia nzima, utabiri huu umekuwepo miaka milioni tano iliyopita.

"Mababu zetu walilitambua hilo hata watu weupe walilijua hilo kabla ya kuharibiwa kwa mji mtakatifu wa Kemet. Vitabu mbalimbali vilivyotabiri kuzaliwa kwa nabii wa bwana vilipotezwa na wakoloni.

"Walichoma moto nyaraka yoyote iliyoonekana kuzungumzia kuzaliwa kwake. Baada ya hapo walileta elimu ya kwao ili kuupindisha ukweli, walibadili hata historia ya mji mtakatifu wa Kemet na kusifia miji yao ya uongo. Waliwaeleza watoto wao ukweli juu ya utabiri wa kuzaliwa kwa nabii mwingine Afrika, wakawasisitiza kumuua nabii huyo pindi watakapombaini."

Ndugu msomaji, maelezo ya mtoto huyo yalikuwa yakisisimua kamati nzima, waheshimiwa kutoka wilayani walikuwa makini zaidi wakifuatilia neno kwa neno.

Kwa muda huo mfupi mtoto huyo alikuwa kafanikiwa kuwateka baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, maelezo yake yalikuwa yamenyooka, kwani hakuna mtoto mwenye umri wa namna hiyo ambaye angeweza kuelezea mambo mazito kiasi hicho.

Mtoto huyo aliendelea, " kwa kulitambua hilo walibuni njia mbadala ambazo zingeweza kuwasaidia kuingia na kusambaa Afrika kirahisi ili kupeleleza unabii huo.

"Walianzisha makanisa nchini kwao ambayo waliyasambaza hadi Afrika, ndani ya makani yao waliingiza wapelelezi wao ambao hutoa taarifa mbalimbali juu ya Afrika.

"Baada ya kuzaliwa kwangu haikuchukuwa muda kwa wao kunitambua, walinitambua kuwa mimi ndiye nabii aliyetabiriwa kupitia wakala wao Padri Samson Mcjohn.

"Ndugu zangu kibali cha Padri huyu nchini kwetu ni kueneza masuala ya Mungu wao, lakini ndani yake kuna nia mbili ovu. Nia ya kwanza ni kufuatilia taarifa muhimu juu ya kuzaliwa kwa nabii aliyetabiriwa, walilishwa yamini ya kuhakikisha wanamuua haraka nabii huyo.

"Nia ya pili ni kujifunza sayansi ya kiafrika yaani uchawi ili wakawafundishe nyumbani kwao kwa jina la teknolojia, hili wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa maana ukienda pale BUJORA MUSEUM Kisesa utawakuta na sehemu zingine za namna hiyo.

"Muda si mrefu mtegemee kuona kundi kubwa la wazungu katika wilaya ya Magu, watu hawa wanakuja kwa kisingizio cha kueneza neno la Mungu, lakini ni wachawi walio na lengo ovu juu ya unabii wangu.

"Tayari fedha nyingi zimeshatumwa kwenye akaunti ya Padri huyo, pesa hizo kazi yake ni kuteketeza maisha yangu ili kuuondoa unabii. Kupitia nguvu za fedha baadhi ya viongozi wamelipwa kwa ajili ya kuanda mazingira ya kuuawa kwangu.

"Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na huyu mheshimiwa (anamyooshea kidole). Yeye aliomba bilioni tano kama ujira wa kufanikisha kuuwawa kwangu, mpaka sasa ameshapewa bilioni tatu zimesalia bilioni mbili.

"Hii ni rushwa kwa kiongozi huyu kwa kufanikisha mipango ovu ya watu hao," alipofika hapo alitulia kidogo, yule mheshimiwa macho yakamtoka kodo, alijipapasa mfukoni mwake haraka haraka. Lengo lake lilikuwa ni kutoa bastola, alikuwa amedhamiria kumshindilia risasi za kichwa mtoto huyo afilie mbali.

Ndugu msomaji unadhani nini kitampata mtoto THE BOMBOM mbele ya mheshimiwa huyo mwenye bastola? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

BONONU BWINGE!!!

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news