NA WILLIAM BOMBOM
Ilipoishia.. kikao kilitamatika kila mmoja akiwa na imani kuu kwa mtoto huyo, miujiza aliyoiona mbele ya macho yao ilikuwa mikubwa sana. Kamati ya ulinzi na usalama waliondoka huku wakiahidi kufika eneo hilo mara kwa mara.
Endelea
Muda wa kutawanyika ulipofika wanafunzi waliruhusiwa kurudi makwao. Kama kawaida mtoto THE BOMBOM alifuata njia ya kuelekea kwao, alipovuka barabara alitembea hatua chache akaufikia mti wa mkwaju.
Pale alijibadili na kuwa jibwa kubwa, lile jibwa liaendelea na safari ya kurudi nyumbani. Ilikuwa ni vigumu sana kwa mtu kutambua kuwa yule hakuwa mbwa bali binadamu aliyejibadili katika umbo hilo.
Mara nyingi wachawi huwa wanachukua maumbo ya wanyama mbalimbali kwa malengo maalumu, mtoto huyo alichukua umbo la mbwa kulingana na hisia alizokuwa nazo kichwani mwake.
Umbo la mbwa alilolichukua alikuwa amechanganya madawa mengine ya kuwakwepa mtu wa aina yeyote kumtambua.
Hapa niseme kidogo mara nyingi mchawi anapochukua umbo la mnyama mwingine, huwa hawawi mnyama huyo bali hupumbaza macho ya waangaliaji na kumuona kama mnyama.
Kimsingi hubakia katika maumbo yao, kujibadili huko huwa ni kwa watu wasio na madawa tu. Lakini akikutana na mchawi mwenzake humuona katika umbile la binadamu halisi.
Kwa upande wa mtoto huyo alijibadili na kuwa katika umbo la mbwa hata kwa wachawi wenzake. Hakuna mchawi wa aina yeyote ambaye angaweza kumbaini, alikuwa na uwezo mkubwa wa madawa.
Aliendelea kuifuata njia inayoelekea nyumbani kwao, kwa upande wa muda ilikuwa imetimia saa nane na ushee.
Alipokaribia uwanda unaotenganisha kitongoji cha nyumbani kwao na shuleni kwao aliona kundi kubwa la wachawi waliokuwa wamezagaa kwenye majaruba ya mpunga.
Yeye aliweza kuwabaini, lakini wao hawakuweza kumbaini, wachawi hao walikuwa wamejibadili katika umbo la ndege weupe wanaopenda kula wadudu majarubani.
Ndugu msomaji, njiani unapotembea huwa unakutana na mambo mengi ya ajabu. Kuna muda unaweza kuhisi umeingiliwa na vumbi machoni, tambua hiyo siyo vumbi ni kidole au umemwagiwa mchanga na wachawi.
Kuna muda unaweza kujikwaa na kudondoka chini ukadhani labda kuna gogo umejikwaa, la hasha ule unaweza ukawa mguu au tofali limewekwa kusudi wachawi wakuone.
Vitu vya namna hiyo kwao huwapa furaha sana. Basi tuendelee,lilikuwa ni kundi kubwa ambalo lilikuwa halifahamiki lilikotokea, hata hivyo kitendo cha kusubiri maeneo ya njia ambayo huitumia mtoto huyo kulionesha kuwa walikuwa wakimsubiria yeye.
Alipita eneo hilo pasipo wao kumbaini, waliamini kuwa yule alikuwa ni mbwa wa kawaida. Kulikuwa na maongezi baina yao, kila mmoja akijinasibu kumtia mtoto huyo mikononi mwake.
Kumbe kundi hilo lilikuwa ni la wachawi wa Zambia maeneo ya Ndola na Malawi ambao walikuwa wametumwa na wakuu wao.
Wao walitamani kumchukua mtoto huyo na kumpeleka huku kumlea kwa faida ya kambi zao za kichawi. Sifa mbalimbali za mtoto huyo kwenye unabii wa kuzaliwa kwake, zilizifanya kambi mbalimbali za kichawi kutamani kummiliki.
Mtoto huyo kwa upande wa wachawi wa Afrika alionekana kuwa Tanzanite, walitamani kumpata ili aweze kuwasaidia katika taaluma za kichawi. Kwa upande wa uchawi wa watu weupe alikuwa ni mwiba, hawakutamani hata kidogo kumuona akiwa hai.
Aliwapita kimya kimya na kuelekea kwao, alipokaribia nyumbani kwao alijibadili katika umbo la binadamu. Alimkuta babu yake akiwa kajipumzisha chini ya mti wa muembe uliokuwa nyumbani hapo.
Alipoingia ndani alishangaa kukutana na wale bibi vizee waliomuokoa mikononi mwa Padri kule kwenye sherehe za kichawi.
Alitambua haraka ujio wao mchana huo, alitoka nje akamwaga dawa ya kuzuia watu wengine kuingia chumbani humo kisha akaingia.
Aliwakuta mabibi hao wakiwa wamekaa kwenye ngozi ndogo ya fisi, hawakuwa na furaha hata kidogo. Walipata taarifa ya wachawi wa Zambia na Malawi kumhitaji mtoto huyo, mabibi hao toka kambi ya Ihushi ndio waliokuwa wakimlea mtoto huyo kwa wakati huo.
Hawakutamani kumuachia kirahisi rahisi, kwani tayari walikuwa walishamwekea dawa za taarifa pindi anapokabiliwa na matatizo.
Walizungumza mambo mengi yanayohusiana na shughuli zao za kichawi, baada ya hapo walimpongeza kwa jambo alilofanya siku hiyo kule shuleni.
Walimsifu sana huku wakiamini muda si mrefu watafanya shughuli zao za kichawi kwa uhuru. Wakakubaliana kukutana mapema siku hiyo kule kambini, kwani kungefanyika kikao kinachohusu ustawi wa shughuli zao za kichawi.
Walipoondoka wachawi hao mtoto huyo aliendelea na shughuli za kawaida za nyumbani hapo huku akizungumza mambo mawili ama matatu na babu yake.
Aliutumia muda huo kumshauri babu yake kulima chakula cha kutosha kwa mwaka huo, alimsisitiza kuwa mwaka uliokuwa ukifuata ungelikuwa na njaa kali.
Ilipofika saa mbili kamili aliomba kujipumzisha, lengo lake alitaka kuona mienendo ya misukule aliokuwa kaachiwa na bibi yake.
Ndugu msomaji hapa nifafanue kidogo. Ukomo wa uhai wa binadamu kwa kawaida hapa duniani ni miaka sabini, lakini huwa tofauti kabisa na misukule.
Misukule huzeeka wanapofikisha miaka kuanzia mia tatu na kuendelea, ni rahisi msukule mmoja akalelewa na vizazi vya kichawi sita mpaka saba.
Yaani misukule waliochukuliwa na bibi, nitawalea mie mpaka nizeeke na kufa. Watachukuliwa na kizazi kingine nacho kitawalea mpaka kizeeke na kufa misukule hao bado wapo.
Mzunguko huo huendelea mpaka vizazi sita hadi saba hapo ndipo huzeeka. Siku zote msukule akizeeka hufanyiwa shughuli zingine, mfano wa shughuli hizo ni pamoja na kumpika ili kupata mafuta ya msukule kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Shughuli nyingine ambayo inaweza kutumika kwa msukule aliyezeeka ni kumuuza kwa ajili ya kumuua ili kupata kizimba cha kuchanganyia dawa.
Ndugu msomaji hapa duniani hakuna dawa kali isiyo na kizimba cha binadamu. Unaposikia kuwa mganga fulani au mchawi fulani ni bingwa utambue kuwa dawa zake zina vizimba vya kutosha vya binadamu.
Kwa namna hiyo anaweza akauliwa mtu husika kulingana na aina ya dawa au akauliwa msukule aliyezeeka. Msukule mzee pia anaweza kutumiwa kama mboga, hakuna mchawi ambaye hajawahi kula nyama ya binadamu.
Nyama hii ni tamu sana kuliko nyama ya aina yeyote, kwanza nyama yake huwa kwenye mfumo wa nyuzi nyuzi haitelezi kama ya ng'ombe.
Kuna muda wachawi wakikosa nyama huwapika hata hao misukule wazee. Kazi nyingine huwekwa kama mbadala wa msukule mpya wanapotaka kumchukua kwenye msiba.
Misukule alioachiwa mtoto huyo walikuwa wengi sana, pale nyumbani misukule hao walikuwa wamegawanywa katika makundi mawili.
Kundi la kwanza walikaa ndani, hawa ni wale waliokuwa wamejifungua au kunyonyesha. Kundi la pili walikaa nje ya nyumba palepale nyumbani, kulikuwa na wigo uliojengwa maalumu kwa ajili ya kuwatunza.
Wigo huo uligawika mara mbili ambapo sehemu ya kwanza walikaa misukule watoto upande mwingine walikaa misukule wakubwa.
Jambo usilolijua misukule huwa na wake, watoto na koo zao, ndani ya mabanda yao huishi kwa upendo huku wakizungumza mambo mbalimbali.
Hawana uwezo wa kukumbuka maeneo waliyozaliwa au kuishi kabla ya kuchukuliwa, labda wakati anachukuliwa kuna hatua fulani ilirukwa kurahisisha kumchukua.
Ilipofika saa nne kamili mtoto THE BOMBOM alichukua ungo wake, alipanda kisha akapaa. Hapa nifafanue kidogo, kifaa hiki kinaitwa ungo kwa kuwa muundo wake kwa juu huonekana kama ungo.
Siyo ungo kama ulivyo ungo wa kupepetea mchele, umbo lake liko mfano wa ungo huo. Malighafi zinazotumika kutengeneza kifaa hicho hutofautiana toka jamii moja kwenda nyingine.
Nyungo zote hutumia mafuta ya binadamu kuweza kupaa. Ni sawa na pikipiki haiwezi kutumia mafuta ya taa kutembea, lazima kuwepo na Petrol ndipo iweze kuondoka.
Jambo jingine ni juu ya uwezo wa kubeba abiria, ukubwa wake hutofautiana kulingana na malighafi iliyotumika. Upo ungo wa kubeba abiria watatu, wanne, saba hadi kumi na tano.
Usafiri huo huwa wa gharama sana, wapo wachawi ambao hawana kabisa usafiri huo. Hii hutoa mwanya kwa wamiliki wa nyungo kufanya biashara za kuwasafirisha, hasa kwenye sherehe za kichawi au wamekwenda sehemu fulani.
Masharti ya usafiri huo ni kufumba macho wakati wa safari, ukijichanganya ukafumbua macho lazima upate ajali. Ndiyo hao wachawi mnaosikia wameanguka walikuwa wanakwenda eneo fulani, kuna taratibu hawakuzitimiza wakati wa kusafiri.
Ukubwa wa ungo huo ni sawa na kiganja cha mtu mzima, lakini hupanuka kulingana na namna utakavyoelezwa na mmiliki kufikia idadi yake kamili.
Mfano kama uwezo wake wa kusafirisha ni watu kumi na tano, wakati huo mpo sita. Basi atanuia nafasi ya watu sita tu ndipo utapanuka nafasi za kutosha watu hao. Siku zote nyungo hutua kwenye viwanja vya shule, makanisa, misikitini, maeneo ya wazi ya jamii na makaburini au kambini kwa wachawi.
Mtoto huyo aliondoka kwa kasi ya ajabu, alikuwa ni dereva mzuri kwenye usafiri huo. Alitamani kufika mapema kambini hapo ili wakaendelee na ratiba zilizokuwepo siku hiyo.
Sekunde chache alikuwa ameshapavuka Nyanguge, mwendo wake ulikuwa zaidi ya upepo. Alivuka Bukandwe, Mikoroshini, Isangijo hatimaye alifika kitongoji cha Bukala.
Punde si punde aliwasili kijiji cha Ihushi, akiwa bado hewani alishangaa kuona kambi yao ikiungua. Alipokodoa zaidi kuangalia eneo hilo alishangaa kuwaona majoka wakubwa waliokuwa wamezunguka kambi hiyo huku wakitema moto uliokuwa ukiunguza kambi.
Ndugu msomaji, unadhani mtoto THE BOMBOM atachukua hatua gani kuinusuru kambi hiyo? Endelea kufuatilia simulizi hii ya kusisimua.
NAHENE BABA