SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-16

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... wachawi hao wakiambatana na yule binti aliyeleta malalamiko. Walichukua bundi kisha wakaruka kwa mbawa zao, walikwenda kutua karibu na nyumbani kwa kijana huyo.

Endelea

Katika msafara huo mtoto THE BOMBOM ndiye aliyekuwa kiongozi wao, kazi kubwa waliyokuwa wametumwa ilikuwa kumshikisha adabu kijana huyo aliyekuwa akitarajia kufunga ndoa.

Kulikuwa na idadi kubwa ya watu katika mji huu usiku huo, hii yote ilichagizwa na mziki uliokuwa ukipigwa maeneo hayo kusherehesha furaha iliyokuwa mioyoni mwao.

Katika tamaduni za jamii ya Kisukuma ndoa imegawanyika katika hatua tatu, hatua ya kwanza huitwa bokwi ambayo ni sherehe ya utoaji wa mahari hufanyika mahali popote kulingana na makubaliano ya pande mbili.

Hatua ya pili huitwa bwenga au bokwelema, hii ni sherehe ambayo hufanyika kwao na mwanamke kwa ajili ya kumuaga binti yao.

Hatua ya mwisho huitwa bokombe, hii ndiyo sherehe ya mwisho hufanyika kwao na mwanaume. Katika sherehe hizo huwa hazihitaji ushiriki wa Padri, Mchungaji wala Shekhe.

Sherehe hii ilikuwa tofauti kabisa, haikuzingatia taratibu za kimila. Yote haya kwa kuwa baba wa kijana huyo alikuwa katikista wa dhehebu la RC kijijini hapo.

Ndoa ilitarajiwa kufungwa kesho yake kanisani, mfungishaji wa ndoa hiyo alikuwa Padri Samson Mcjohn kwa kuwa kijiji hicho kilikuwa ni kigango ndani ya parokia yake. Ndoa ilitegemea kufungwa asubuhi majira ya saa tatu kamili, katika kanisa la Moyo wa Yesu.

Hivyo shughuli zote za kimila zilizuiwa katika sherehe hiyo kwa kuwa ni dhambi, hivyo kitu pekee walichokiruhusu ni mziki ili kusherehesha.

Watu waliitika kwa fujo toka pande zote, vijana toka vijiji vya Galama, Bukala, Ng'wakelo, Kanyama, Kayenze, Busekwa na Igekemaja walikuwa wakishindana kulisakata rhumba.

Ghafla ukapigwa wimbo wa msanii wa kisukuma aitwaye Ng'wanakang'wa, wimbo huu ulikonga nyoyo za wasakata mziki hao. Vumbi likatimka kwa kiwango cha juu, kila mmoja alikuwa akicheza kwa staili yake kulingana na utamu wa mziki.

Wakati huo wale wachawi wote walikuwa bado kwenye umbo la bundi, huku wakiangazia macho yao kwa wasakata disko vumbi waliokuwa mbele yao.

Mtoto THE BOMBOM na wachawi watatu wengine, waliamua kuchukua umbo la paka, waliwaacha wenzao sita wakiwa juu ya mti katika umbo la bundi.

Kwa muda wote huo hawakumuona yule kijana yaani bwana harusi, wakajiaminisha kuwa kijana huyo alikuwa amepumzika chumbani kwake.

Walikisaka kwa udi na uvumba chumba chake hatimaye wakakibaini. Walifanya hila wakafanikiwa kuingia chumbani humo, wakamkuta akiwa kasinzia.

Walipoingia chumbani humo walimwaga dawa ya kuzuia mtu yeyete kutoingia chumbani humo, walipohakikisha kuwa wako salama kabisa walimuamsha kijana huyo.

Kijana alitoka usingizini na kuwakuta watu hao wanne wakiwa kwenye umbo la paka, ila vichwa vyao vilikuwa vya binadamu.

Walikuwa chumbani humo huku mlango ukiwa umefungwa, alijaribu kifikicha mboni za macho yake kwa kudhania labda alikuwa akiota.

Lakini kila alipotazama kwa makini hakukuwa na mabadiliko yeyote, wachawi wale walitaka kumpa hofu kwanza kabla ya kumshughulikia.

Alipojaribu kupiga kelele sauti yake ilizuiwa na wachawi hao, watu waliokuwa nje hawakusikia kelele ya aina yoyote toka chumba hicho.

Ghafla alichomoka kwa kasi kitandani hapo kama mshale wa mtemi Mirambo, alipofika mlangoni alishika kitasa na kunyonga kwa nguvu ili atoke nje, lakini mlango ukagoma kufunguka.

Yule mchawi binti alijibadili kutoka umbo la paka na kurudi kwenye umbo lake halisi. Akamsogelea kijana huyo huku akiwa na hasira, kijana huyo akapiga yowe la kuomba msaada, lakini haikumsaidia.

Yule binti alipomkaribia kijana huyo, akamnasa kibao cha nguvu shavuni kwake. Akaanguka chini mithili ya furushi la pamba, alipojaribu kusimama alikutana na kofi jingine lililomrudisha chini.

Wale wachawi watatu nao walijibadili maumbo yao na kuwa binadamu wa kawaida, walimsogelea pale chini kijana huyo na kuanza kumhoji maswali kadha wa kadha.

Kijana alilia kwa uchungu huku akiomba msamaha kwa makosa yake, aliendelea kuomba nafasi nyingine ili asawazishe makosa yake. Wachawi wale hawakuwa na muda wa kutoa msamaha, kazi kubwa iliyokuwa imewapeleka ni kumshikisha adabu.

Walimshika kwa nguvu kisha wakamkalisha chini, wakachukua msumari mmoja wa nchi sita wakaushindilia kichwani mwa kijana huyo. Lilikuwa pigo moja la nyundo lilililoushindilia msumari huo na kuishilizia kichwani.

Wakaongeza msumari mwingine wakaushindilia kwa nyundo nao, walitaka kutoa fundisho kwa vijana wengi ambao hupenda kuchezea watoto wa watu.

Yule kijana alidondoka chini akawa anarukaruka mithili ya kuku aliyechinjwa kwa kisu kisha akaachiwa. Aliendelea kurukaruka kwa muda wa dakika chache kisha akatulia, yule binti alikuwa amefarijika kwa kitendo hicho.

Baada ya hapo mtoto THE BOMBOM alichukua dawa fulani akampaka maiti huyo kisha wakaondoka wakiwa kwenye umbo la paka.

Kule nje waliwakuta watu wakiendelea na muziki wao. Wale wachawi waliamua kutoa zindiko, hii ni kawaida kwa wachawi wanapoamua kumuua mtu kwa kifo cha namna hii.

Hupiga kelele sana wakiwa kwenye umbo la paka, kwa mtu asiyejua anaweza kudhani paka hao wanapandana au wanagombana kumbe wanatoa zindiko.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji mara nyingi kuna watu huuawa kwa vifo vya namna hii. Vifo vya namna hii hospitali hawana vipimo vya kuvijua, wao hukimbilia kusema shinikizo la damu.

Vifo hivi huwa ni vya visasi itategemea na kosa ulilomfanyia mchawi, mhusika aliyekosea hukamatwa kwa nguvu mahali popote watakapomwinda na kumkamata. Mara nyingi vifo vya namna hii hutokea usiku, wanaweza kukukamata njiani, chooni, ndani au mahali popote pale.

Wakikukamatata wanaweza kukunyonga kwa kamba, wanaweza kukupiga panga au mkuki, wanaweza kukupiga mpini au chochote na kukuua.

Kumtambua mtu aliyeuwawa kwa namna hii ni rahisi sana, kwanza kabisa enapokufa mtu huyo ni lazima paka walie sana kwa muda mrefu maeneo hayo. Pili maiti huwa na rangi nyeusi ya kuiva hasa kwenye mashavu na eneo la tumbo.

Walipomaliza kazi yao walijibadili na kuwa bundi kisha wakaruka kwa mbawa zao mpaka mtini palipokuwa na wenzao.

Walijadiliana mambo kadhaa mtini hapo kisha wakakubaliana kwenda kanisani ambako kulitakiwa kufungishwa kwa harusi hiyo.

Pale kanisani waliwakuta wachawi wengine wakiendelea na shughuli zao. Ilikuwa muda wa saa nane na dakika ushee hivi, haikuwashangaza sana kwa kuwa maeneo hayo hutumiwa sana na wachawi katika shughuli zao. Kulikuwa na wachawi wa kiwango cha chini, pengine wengine ndiyo walikuwa wakijifunza taaluma hii.

Waliingia kanisani humo na kukuta wachawi wengine wakiendelea na shughuli zao, kulingana na nguvu za dawa walizokuwa wamejipaka wale wachawi wasingeweza kuwaona.

Walielekea kwenye altari ya kanisa hilo, walipofika kwenye kiti ambacho hukitumia Paroko wakati wa ibada wakamwanga dawa.

Baada ya hapo walikwenda kwenye sekastia, kisha wakaifungua na kutoa ekaristi na kuichanganya na dawa.Walifanya hili wakiwa wamedhamiria kumkomesha Padri huyo.

Kulikuwa na kundi kubwa la wachawi waliokuwa hawaelewani na Padri huyo. Walimgundua mapema kuwa hakuwa mtumishi wa Mungu bali ni mchawi mwenzao.

Kuna majaribio mengi yalifanyika ya kumuua, lakini aliyakwepa, baada ya hapo waliachana naye kila mmoja akawa anafanya shughuli zake. Siku hiyo walitaka kumjaribu tena nguvu zake, mtoto THE BOMBOM ndiye aliyeongoza kazi hiyo.

Walipokamilisha kazi yao, walirudi kambini kwao katika umbo la bundi. Walitoa maelezo kwa kina juu ya kazi waliyoifanya, hata hivyo walielezea kazi ya ziada waliyoifanya kule kanisani.

Mambo yanasonga mbele, ndugu msomaji unadhani nini kitampata Padri huyo? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua sehemu inayofuata.

WABEJA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news