SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-8

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...sherehe hiyo iliambatana na kubadilishana misukule. zipo sababu mbalimbali ambazo hupelekea wachawi kubadilishana misukule. Mojawapo ya sababu hizo ni pamoja na: uzee wa msukule, nguvu za misukule, usumbufu wake, vizimba nk.

Endelea

Saa nne kamili usiku mtoto THE BOMBOM pamoja na bibi yake walikuwa wameshafika eneo la sherehe.

Wachawi kibao walikuwa wakishuka uwanjani hapo wakitumia usafiri wa aina mbalimbali. Wapo waliokuja kwa vijiko, miko, fagio na vyombo vingine.

Wengine walikuja kwa usafiri wa ungo, ngozi, ndege kiumbe pamoja na upepo. Wale wa karibu walikuja kwa usafiri wa wanyama kama vile panya, paka, mbwa na fisi.

Wengine walikuja kwa mbweha, punda, popo na mbu. Huu wote ni usafiri ambao hutumiwa na wachawi kutegemea na uwezo wa mchawi mwenyewe.

Kwa upande wa bibi na mtoto THE BOMBOM wao walitumia usafiri wa upepo. Walifanya hivyo kwa kuwa kutoka Ilungu kwenda Gw'atelesha haikuwa mbali sana. Kwa mara ya kwanza mtoto THE BOMBOM akawa amehudhuria sherehe kubwa ya kichawi.

Katika sherehe hiyo mipango mbalimbali ya kichawi ilifanyika, walipanga njia bora za namna ya kuua watu.

Walibadilishana uzoefu wa madawa mbalimbali huku wakifundishana majina ya miti ya uchawi, namna ya kuchimba dawa pamoja na vionjo vyake.

Kwa kawaida katika sherehe hizo huwa kuna mazindiko ya kila aina. Wachawi hufanya hivi ili kuwazuia mahasimu wao kuleta dhoruba.

Mbali na mazindiko waliyokuwa wameyafanya mahali hapo, bado kuna watu walikuwa wamevamia kwenye sherehe hiyo kimya kimya.

Kulikuwa na makundi ya wachawi wengine waliokuja eneo hilo, Padri Samson Mcjohn na kundi lake nao walifika eneo hilo.

Bibi na kundi lake walizidiwa ujanja hawakuweza kuwaona hasimu wao. Mahasimu hao walifika mapema eneo hilo na kumwaga dawa zilizowafumba macho bibi na kundi lake kuona.

Pia kulikuwa na kundi jingine ambalo lilikuwa linatokea eneo la Ilongo ambalo lilikuwa halielewani kabisa na kundi la bibi.

Mahasimu hao walikuwa na nia ovu dhidi ya kundi la kichawi la bibi, muda mwingi walitamani kupata upenyo wa kufanya maovu, lakini walishindwa.

Hatimaye leo kwa kusaidiana na kundi la Padri Samson Mcjohn walikuwa wamefanikiwa. Wachawi hao walifanikiwa kumwaga dawa kwenye chakula kilichokuwa kimeandaliwa shereheni.

Dawa hiyo ilikuwa ni sumu iliyokuwa imekusudiwa kuwamaliza wote pindi watakapokula chakula hicho. Sherehe iliendelea kama kawaida huku wachawi husika wakiwa kwenye furaha ya hali ya juu.

Hawakujua hata kidogo kama siku hiyo walikuwa wameingia kwenye mtego wa mahasimu wao. Hatimaye ukafika muda wa kula na kunywa vinywaji vilivyokuwa vimeandaliwa.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji miongoni mwa watu wanaopenda starehe ni wachawi. Hupendelea pombe na mapochopocho kwenye sherehe, hula nyama kwa wingi kuliko kitu chochote.

Sherehe iliendelea huku wachawi wa kundi la bibi wakila sumu iliyokuwa imetegwa. Ghafla walianza kudondoka mmoja baada ya mwingine, sumu iliyokuwa imewekwa kwenye chakula na vinywaji ilianza kuchukua uhai wao mmoja baada ya mwingine.

Kitendo hicho kilimshituwa bibi kutoka kwenye lindo la kilevi alilokuwa katopea. Ndani ya muda mfupi alishuhudia wachawi wenzake wakidondoka chini na kukata roho mithili ya siafu mbele ya moto.

Kabla hajachukua hatua yeyote alishangaa akikamatwa na watu aliokuwa hawaoni. Mara watu hao walijitokeza mbele ya upeo wa macho yake, hakuamini kilichokuwa kikiendelea mbele yake.

Alikuwa ni hasimu wake mkuu Ng'wana Michembe akiwa na kundi la wachawi wengine. Mwanamke huyu alikuwa ni hasimu mkuu wa bibi yake na mtoto THE BOMBOM wa muda mrefu.

Uhasama huo ni wa vizazi na vizazi baina yao, kuanzia kwa babu wa babu wa mababu zao. Familia hizo hazikuwahi kuelewana hata kidogo, bahati nzuri familia zote zilikuwa zimetopea kwenye taaluma ya uchawi.

Hata hivyo baina yao familia ya bibi ilikuwa na nguvu kubwa ya kichawi kuliko mahasimu wao. Japo familia ya Ng'wana Michembe ilinyanyasika kwa muda mrefu, lakini hawakukata tamaa waliendelea kupambana hadi tone la mwisho.

Hatimaye siku hiyo walikuwa wamefanikiwa kuwaweka mikononi mwao. Bibi huyo alianza kumshikisha adabu bibi wa mtoto THE BOMBOM, alianza kwa kumpiga makofi ya mashavuni.

Baada ya hapo alichukua upanga wake akaanza kumtenganisha kiungo kimoja baada ya kingine. Wakati huo mtoto THE BOMBOM alikuwa akishuhudia kwa macho yake mambo aliyokuwa akifanyiwa bibi yake.

Walianza kumtenganisha vidole vya miguu kimoja kimoja, maumivu aliyokuwa akiyahisi bibi wa mtoto THE BOMBOM yalikuwa makali kuliko kawaida.

Kila alipojaribu kugusa chale zake ili awatoroke maadui hao hakufanikiwa. Alikuwa kadhalilishwa kwa kiwango cha juu, yeye na kundi lake hawaku na namna ya kukwepa tena. Wakati huo Padri Samson Mcjohn na kundi lake walikuwa wakiendelea kuwamalizia kuwaua wachawi waliokuwa hawajaathiriwa sana na ile sumu.

Walichukua msumari wa nchi tano kisha wakauweka kichwani mwa bibi yake mtoto THE BOMBOM, msumari huo alikuwa nao Padri Samson Mcjohn wenye sumu.

Baada ya hapo waliushindilia kichwani mwake kwa pigo moja takatifu la nyundo iliyopigwa kwa nguvu na Ng'wana Michembe.

Msumari huo ukazama wote pasipo mawaa, kundi hilo lilishangilia kitendo hicho cha kinyama walichokuwa wakikifanya.

Wahenga walisema "damu ni nzito kuliko maji" kitendo hicho kilimuumiza sana mtoto THE BOMBOM. Katika umri huo alikuwa akimuhitaji sana bibi yake, mambo aliyokuwa akifanyiwa bibi yake na mahasimu wake yalimuumiza sana.

Alijaribu kukimbia ili akamsaidie bibi yake, lakini hakuweza, kabla hajamfikia bibi yake alitegwa ngwala akadondoka chini mithili ya furushi la nguo chafu.

Akiwa pale chini alianza kushambuliwa kwa mabuti na mikoma ya madawa waliyokuwa nayo wachawi hayo.

Damu zikawa zikimchuruzika puani na mdomoni. Wakati huo bibi yake alikuwa akimalizia kukata roho, msumari ulioingia kichwani mwake ulichukua uhai wake. Lakini kabla ya kufa bibi huyo alitema hirizi ya uchawi.

Hapa niseme kidogo, kwa utaratibu wa kawaida hirizi hiyo alipaswa kulishwa mtoto THE BOMBOM ili kuendeleza uchawi wa ukoo wao.

Ng'wana Michembe na Padri Samson Mcjohn walifurahia sana kuiona hirizi hiyo. Waliichukua wakawa wanajadili jambo fulani pembeni ya sehemu alipokuwa ameangushwa mtoto THE BOMBOM.

Kwa kuwa mtoto huyo alikuwa ni mchawi, alikuwa akifahamu umuhimu wa hirizi iliyokuwa imetapikwa na bibi yake. Mara kwa mara bibi yake alikuwa akimsimulia umuhimu wa kuitunza hirizi hiyo na kuirithisha kizazi na kizazi.

Akiwa chini hapo alishuhudia kuanzia mwanzo hadi mwisho ilivyochukuliwa hirizi hiyo. Alijitutumua kwa kukusanya nguvu zake za kitoto, kisha alichomoka toka hapo chini kama mshale na kufanikiwa kumpokonya Padri Samson Mcjohn hirizi hiyo mikononi mwake.

Kilikuwa ni kitendo cha haraka sana kwani hawakutegemea. Alipoitia mikononi mwake mtoto THE BOMBOM hakupoteza muda aliitia kinywani mwake.

Lakini kabla hajaimeza alipigwa ngumi nzito upande wa shavu lake la kushoto. Ngumi hiyo ilitoka kwa Padri Samson Mcjohn ili kumzuia mtoto huyo kuimeza.

Maumivu yalikuwa makali yasiyo mfano, kulingana na uzito wa ngumi hiyo mtoto huyo aliitema hirizi pamoja na jino moja.

Ng'wana Michembe akautumia muda huo kuiokota, kabla hajaichukua alipigwa mueleka mzito toka kwa Padri Samson Mcjohn.

Akadondoka chini na kuikosa hirizi hiyo, Padri aliinama kuichukua hirizi lakini alikamatwa miguu yake kwa nyuma na Ng'wana Michembe.

Matokeo yake alikosa balansi akajikuta anadondoka chini, palepele mtoto THE BOMBOM aliutumia muda huo kuiokota hirizi. Kabla hajaiweka mdomoni alishangaa anapigwa na kitu kizito kichwani akadondoka chini..

Ndugu msomaji mambo yameanza kuiva, mtoto THE BOMBOM anapambania kuchukua hirizi ya bibi yake. Je, atafanikiwa? Endelea kufuatilia kisa hiki cha kusisimua.

BALOGI MATWENEGI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news