SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-9

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...matokeo yake alikosa balansi akajikuta anadondoka chini. Palepale mtoto THE BOMBOM aliutumia muda huo kuiokota hirizi. Alifanikiwa kuiweka mikononi mwake, lakini kabla hajaiweka hirizi hiyo mdomoni. Alishangaa anapigwa na kitu kizito kichwani mwake akadondoka chini.

Endelea

Lilikuwa ni pigo takatifu ambalo lilimfanya aone nyota nyota machoni mwake. Pigo hilo la mpini lilituwa vyema kichwani mwake, toka kwa mwanamama Ng'wana Michembe lililokuwa limekusudia kukatisha uhai wa mtoto huyo.
Alidondoka chini mithili ya gunia la mahindi, kwa mbali akawa anaona ukungu ukipita machoni mwake.

Mbali ya shambulio hilo la nguvu bado mtoto THE BOMBOM aliendelea kujikaza kisabuni. Akiwa hapo chini alifumbua macho yake na kuangalia upande aliokuwa amedondoka bibi yake.

Bahati nzuri macho yao yalikutana, hali ya bibi haikuwa njema hata kidogo. Ingawa bibi yake hakuwa na uwezo wa kuzungumza, hata hivyo kupitia macho yake yalionekana kumuhimiza kufanya jambo.

Bibi yule hakuchukua muda akakata roho, mtoto THE BOMBOM alikuwa ameshatambua maana ya macho yaliyokuwa yametazamwa na bibi yake kabla ya kuaga dunia.

Alitazama upande wa kushoto wake akashangaa kuona yule Padri Samson Mcjohn na Ng'wana Michembe wakiwa kwenye mapambano makali.

Kila mmoja alitamani kuichukua hirizi hiyo kwa manufaa yake, kuimiliki hirizi hiyo ingesaidia kwa kiwango kikubwa kuongeza nguvu za kichawi.

Vilevile kuimiliki hirizi hiyo ilikuwa ni tiketi ya kuhamisha uchawi wa ukoo husika kwenda kwa mtu aliyeichuku.

Ghafla Ng'wana Michembe alitema mate, yale mate yakageuka kuwa wadudu wadogo wadogo wengi. Punde si punde wale wadudu walibadilika na kuwa nyuki waliokuwa wakiongezeka kila muda.

Sekunde chache tu wale nyuki walikuwa makumi elfu kwa makumi elfu, wakati huo mtoto THE BOMBOM alikuwa bado kalala chini.

Ng'wana Michembe alinuia kitu ghafla wale nyuki waliondoka kwa kasi wakimfuata Padri Samson Mcjohn.

Walipomfikia walianza kumng'ata kwa kasi ya ajabu, walimzingira mwili mzima huku wakiendelea kumng'ata.

Hakuna mtu aliyekuwa akiimiliki hirizi hiyo mpaka muda huo, si Padri si Ng'wana Michembe wala si mtoto THE BOMBOM.

Baada ya Padri kuzidiwa kwa maumivu makali ya nyuki alijibadili umbo na kuwa mti mkubwa. Wale nyuki walijaribu kuushambulia mti huo, lakini haukuteteleka, kwa kuwa Ng'wana Michembe alikuwa amekusudia kuchukua alama zote tatu toka kwa mpinzani wake alibadili njia ya kumshambulia adui yake.

Alitema mate kiganjani kwake kisha akanuia maneno fulani, mate hayo yalibadilika na kuwa chuma ndogo ambayo aliitupa chini.

Ndugu msomaji hii yote ilikuwa ni vita ya magwiji wa dawa, vita hiyo ililenga kumiliki hirizi iliyokuwa imetemwa na bibi yake mtoto THE BOMBOM.

Alipoitupa chini chuma hiyo ilibadilika na kuwa shoka kubwa. Ilikuwa ni shoka yenye makali yasiyomithilika, punde si punde shoka hiyo iliondoka kwa kasi toka chini hapo na kumfuata Padri aliyekuwa amejibadili kuwa mti.

Kabla ya shoka hiyo kuufikia mti mambo ya ajabu yalijitokeza, yule Padri alijibadili na kuwa nguzo ya chuma mfano wa minara ya simu. Ile shoka ilipofika kwenye chuma kile ilipiga pigo moja ikajikunja mithili ya jembe lililokata kwenye mwamba imara.

Matokeo hayo yalimuudhi sana Ng'wana Michembe, hakuyatarajia hata kidogo. Muda mchache uliopita walikuwa marafiki wakisaidiana kumdhibiti bibi yake mtoto THE BOMBOM.

Lakini muda huu walikuwa wamegeuka na kuwa mahasimu wakubwa, endapo ungeliwaona mwanzoni walivyokuwa wakipanga mipango yao kwa pamoja usingeliamini kama wamekuwa maadui wa kiwango hicho. Namna shoka ilivyokuwa imejikunja isingeweza kutumika kwa namna yeyote.

Hasira iliongezeka kwa Ng'wana Michembe mara dufu, alijibadili na kuwa moto wenye uwezo wa kuyeyusha kile chuma. L

Lengo lake kubwa ilikuwa ni kummaliza Padri huyo mzungu, moto huo ulitembea kwa kazi kuelekea palipokuwa na ile nguzo.

Kabla moto huo haujafika kwenye ile nguzo, haraka sana nguzo hiyo ilijibadili na kuwa mto wa maji uliokuwa ukitiririsha maji mengi kuelekea katikati ya majengo ya shule ya Ng'watelesha.

Upana wa mto huo ulikuwa zaidi ya mita kumi, mto wenyewe uliambaa mpaka eneo ilipokuwa hirizi hivyo kuisomba kwa nguvu ya maji hayo yaliyokuwa yakienda kasi.

Mtoto THE BOMBOM alinyanyuka na kukimbilia hirizi hiyo iliyokuwa ikielea majini na kwenda kwa kasi upande mwingi lakini hakufanikiwa.

Moyo wake ulisita baada ya kuona magogo makubwa na majabali yaliyokuwa yalisukwasukwa kwa nguvu ya maji ya mto.

Alibaki amejishika kiuno huku akiwa amekata tamaa ya kuipata hirizi hiyo iliyokuwa ikiendelea kutoweka kwenye upeo wa macho yake.

Akiwa bado amesimama alishangaa kuuona ule moto ukizama ndani ya mto, moto huo ulipotelea ndani ya mto na kuliacha eneo hilo likiwa shwali.

Akiwa bado anashangaaa ghafla ndege mweusi alitokea kusikojulikana, ndege huyo aliinyakua ile hirizi toka kwenye ule mto kisha akapaa nayo hadi kwenye bati la shule msingi Ngw'atelesha.

Kuzama kwa moto huo ndani ya mto, ilikuwa ni kumaliza uhai wa Ng'wana Michembe. Maisha yake yalikuwa yameishia hapo alitamani kuchukua alama zote sita kama chama la wana Simba Sports Club kwa Vipers lakini alishindwa vibaya kama alivyoshindwa Mwananchi dhidi ya Al-Hilaly ya Sudan.

Maisha yake yaliishia mtoni hapo, kwa macho ya kawaida kwako ungeliona mto, lakini haukuwa mto bali ni aina fulani ya kiumbe ambaye hutengenezwa kwa mfano wa mto.

Ghafla mto ule ulipotea akatokea Padri Samson Mcjohn akiwa kwenye nguo zake za kichawi, alikuwa kavaa nguo zake nyeusi kufunika sehemu za siri huku sehemu zingine zikiwa tupu.

Hapa niseme kidogo, katika suala la mavazi wachawi tunatofautiana na waganga. Siku zote nguo ambazo hutumika katika shughuli za kichawi huwa ni nyeusi, rangi hii huwakilisha UKUU WA MWAFRIKA.

Hata kwa upande wa waganga nguo nyeusi hutumika kwa maana hiyo, wanapotumia rangi nyekundu humaanisha umwagaji wa damu ndiyo maana watu wekundu wana roho za kikatili sana japo huhadaa na kujiita wao ni weupe.

Padri aliangaza huku na huku kuitafuta hirizi ile, lakini hakuiona, hatimaye alimuona yule ndege akiwa ameibeba mdomoni mwake juu ya paa la shule.

Kitendo hicho kilimkera sana Padri huyo, haraka alijibadili na kuwa bundi kisha aliruka kwa mataho kuelekea juu ya paa la shule.

Kabla hajatua batini hapo, yule ndege mwenye hirizi aliruka na kuhamia upande wa alipokuwa amesimama mtoto THE BOMBOM.

Bila kuchelewa alitua karibu ya mdomo wa mtoto THE BOMBOM kisha akamlisha ile hirizi mfano wa njiwa afanyavyo, kisha ndege huyo akaondoka. Mtoto huyo alijitahidi kuimeza haraka kabla hajazidiwa ujanja na yule Padri Mzungu.

Kitendo hicho kilimkera sana Padri huyo, alijaribu kumkimbiza yule ndege mweusi ili amuwajibishe, lakini haikuwezekana ndege huyo alipotea kimiujiza.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji mara nyingi umekuwa ukikutana na viumbe katika maumbo fulani na unaamini kuwa viumbe hao ndiyo halisi.

Hapa huwa unajidanganya kuna muda wachawi huchukua maumbo ya viumbe kwa malengo fulani. Unapokutana na paka mweusi tii au mweupe pee kisha mwili wako ukawa unasisimuka tambua huyo siyo paka bali ni mtu.

Dalili nyingine ya kugundua huyo siyo mnyama halisia ni kusimama kwa nywele zako. Unapokutana na mchawi katika umbo la kiumbe kingine ni lazima nywele zako zisimame.

Hii ni kwa sababu ya dawa ya mchanganyo ya mti wa lotonda, dalili zingine ni kujiamini sana kwa kiumbe huyo kupitiliza kuliko uhalisia wa kiumbe husika. Hapo tambua kiumbe huyo ni binadamu aliyevaa umbo la kiumbe mwingine kwa shughuli maalumu.

Yamkini hata ndege mweusi aliyeiokota hirizi hiyo hakuwa ndege halisia bali alikuwa ni binadamu. Kulingana na hali halisi ya mazingira mtoto THE BOMBOM hakuweza kumbaini ndege huyo.

Baada ya Padri huyo kumkosa yule ndege alijibadili na kuwa upepo kisha akarudi kwa mtoto THE BOMBOM.

Hasira ilikuwa wazi machoni mwake, alitua pembeni mwa mtoto huyo kisha akajibadili kuwa joka kubwa.

Alikuwa joka mkubwa mwenye unene na urefu wa nguzo ya umeme, alimrukia mtoto huyo na kumkamata kisha kumuangusha chini.

Alijizungusha mwilini mwa mtoto huyo kisha akaanza kumlamba mwili wake. Padri alitamani kummeza mtoto huyo ili ile hirizi aliyomeza mtoto huyo iingie tumboni mwake.

Yaani mtoto na hirizi zote ziingie kwa mzungu huyo. Aliendelea kumlamba kwa kasi huku mtoto akiwa kabanwa hana uwezo wa kuchomoka. Mate ya joka hilo yalikuwa yanateleza mithili ya mlenda wa Kinyamwezi..

Ndugu msomaji tayari mtoto THE BOMBOM ameshaingia kwenye kumi na nane ya Padri Samson Mcjohn. Unadhani nini kitampata mtoto huyu? Je,KANISA LA KICHAWI linahusika vipi na Padri na mtoto THE BOMBOM.

GW'ANAGW'ISE MHOLA?

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news