Somo la mali kwa wanandoa kwa kilichotokea kwa Achraf Hakimi na mkewe

NA WAKIL BASHIR YAKUB
+255714047241

MKE wa ACHRAF HAKIMI ameshindwa kupewa mali yoyote baada ya ndoa yao kuvunjika kwa sababu Hakimi aliziandika mali zote jina la mama yake mzazi.
Je jambo hili linawezekana kwa Sheria za Tanzania?. Ndio linawezekana, ni hivi :- Kwa wanandoa kuna mali za aina 2;-

1. Mali zilizopatikana kabla ya ndoa.

2. Mali zilizopatikana wakati wa ndoa.

MALI ZILIZOPATIKANA KABLA YA NDOA

Hizi ni mali ambazo mtu anakuwa nazo kabla hajaoa ama kuolewa. Yumkini akiingia kwenye ndoa anaingia nazo.

Hata hivyo Sheria ya ndoa inasema mali hizi zinahesabika si za ndoa kwa maana ya kuwa huyo mwenye nazo ni zake peke yake bila mwenza wake. Ndoa ikivunjika haziwezi kugawiwa.

Pamoja na hayo, mali hizo pia zinaweza kubadilika na kuwa za ndoa ikiwa mambo mawili yatafanyika. KWANZA, ikiwa mwenza mwenye hizo mali ataingia makubaliano na mwenza wake kuwa ziwe za ndoa basi zitakuwa za ndoa na itakapovunjika basi zitagawiwa.

PILI, iwapo mali umeingia nayo kwenye ndoa lakini kipindi cha ndoa imeendelezwa. Mfano, Umeingia kwenye ndoa na kiwanja chako lakini kipindi cha ndoa ndo kimejengwa, AU kilikuwa kimejengwa lakini ni pagala tu, kipindi cha ndoa ndo mmemalizia na kuwa nyumba kamili.

Hapa ndoa ikivunjika mtagawana na hautasema alinikuta na Pagala langu au kiwanja changu. Kitendo cha kuendeleza mkiwa wote kinampa haki mwingine na kuwa mali ya wote.

Lakini kama mali ameingia nayo kwenye ndoa na hakuna maendelezo yoyote yaliyofanyika kipindi cha ndoa basi hiyo mali haiwezi kugawiwa ndoa ikivunjika na inabaki mali ya mwenza huyo pekee.

MALI ZILIZOPATIKANA WAKATI WA NDOA

Hizi huhesabika moja kwa moja kuwa ni za wanandoa wote mpaka isemwe vinginevyo.Na haijalishi zipo kwenye jina la mke au mme, madhali zilipatikana kipindi cha ndoa basi zinahesabika ni za wanandoa na zinastahili kugawiwa ndoa inapovunjika.

Hata hivyo, ili ziweze kugawiwa ni lazima kila mwanandoa athibitishe mchango wake katika upatikanaji wa hizo mali.

Tafsiri ya mchango ni pamoja na pesa, vifaa, lakini hata kazi za nyumban nao ni mchango katika kupatikana kwa mali.

Mke au mme anayebaki nyumbani kwa ajili ya shughuli za nyumbani anahesabika amechangia kwa kile kinachopatikana kutoka kwa yule aliyeingia mtaani kutafuta.Kwa hiyo wakati wa kuthibitisha mchango hayo yote yanazingatiwa.

JE MGAWANYO WA MALI NI NUSU KWA NUSU

Hapana, mgawanyo mali za ndoa inapovunjika sio lazima kuwa nusu kwa nusu. Inaweza kuwa 20%/80%, 70%/30%, 90%/10%, nk nk. Kwa ufupi hakuna kiwango maalum, hata kukosa kabisa kupo.

Kikubwa ni kuwa utapata fungu lako kutokana kiwango cha mchango wako kama tulivyoona hapo juu. Na kama huna mchango kabisa basi waweza kutoka kapa pia.

MALI AMBAZO ZIKO KWENYE MAJINA YA WATOTO

Mali hizi hamuwezi kuzigawa ndoa inapovunjika. Hii ni kwasababu kitendo cha kuandika majina ya watoto ni sawa na kuwa mlikubaliana kuwapa zawadi watoto.

Ukitoa zawadi maana yake maslahi(ownership interest) yenu katika hiyo mali yalishahama kwenda kwa watoto kwa njia ya zawadi nanyi hamna maslahi tena katika hiyo mali.

MALI ZILIZOANDIKWA MAJINA YA WATU WENGINE

Mali ambayo haina jina la mke au mme sio rahisi kuigawa ndoa inapovunjika. Huyu HACHRAF HAKIMI aliandika majina ya mama yake. Mali ya namna hii ni vigumu kuigawa kama mali ya ndoa kwasababu inaonekana inamilikiwa na mtu mwingine.

Kwa msingi huu huwezi kugawa mali ambayo haihusiki. Wengine huandika majina ya ndugu zao, marafiki nk.

Ndio, akifanya hivi basi ni vigumu hiyo mali kuigawa ndoa ikivunjika hata kama una uhakika wa 100% kuwa ni yenu.

Hii ni kwasababu ushahidi wa nani mmiliki wa mali ni nyaraka au usajili. Nyaraka na usajili unaonesha mtu mwingine ni vigumu useme hii mali ni yetu.

MALI INAYOBADILISHWA UMILIKI

Kama mali imeanza ikiwa ni ya ndoa halaf ikabadilishwa majina hiyo unaweza kuidai na ikagawiwa. Wapo wanandoa wakiona mambo yameanza kubadilika basi ama huanza kubadili majina ya mali au huuza.

Ikiwa tarehe zitaonesha mali ilibadilishwa au kuuzwa kipindi cha ndoa na ni mali ya wanandoa,na mwenza hakuwa ameridhia, basi ubadilishwaji huo ama uuzaji huo ni batili na hiyo mali itarudishwa kwenye mali za wanandoa ili igawiwe.

WANANDOA WANAWEZA KUFANYA NINI KUHUSU MALI

KWANZA, yafaa ikiwa mtakubaliana basi mali iwe na majina ya wote mke na mme. Iwe ni gari, kiwanja, nyumba,akaunti benki, nk. Sheria inaruhusu.Hii husaidia sana hata kipindi cha kifo ambapo mjane au mgane hawezi kusumbuliwa.

PILI, mnaweza kuwa na makubaliano kuhusu kila mali,kuanzia zile ambazo mlikuwa nazo kabla hamjaoana, mpaka zile mtakazopata wakati wa ndoa. Mtakubaliana ipi iwe ya pamoja na ipi iwe ya mmoja.Japo hili ni gumu kwa maisha yetu sababu ukilianzisha hili utaambiwa HUNA MAPENZI YA KWELI.

TATU, muwe na utaratibu wa kucheki mara kwa mara hadhi(status ) ya mali. Pitia pitia huko Ardhi, TRA, Serikali ya mtaa ujue. Msilale sana.Huenda ukagundua kitu mapema kabla mambo hayajaharibika.

NNE, msajili/andika mali kwa majina ya watoto, maana yake muwape zawadi watoto. Hata kama mnatumia nyie lakini ikijulikana ni za watoto. Ila lazima iwe imesajiliwa na sio kusema tu kwa mdomo kuwa hizi ni mali ni za watoto.

Ukisema mali ni za watoto na hakuna usajili rasmi hiyo hukataliwa sababu watoto hawana mali bali mali ni za wazazi na majina zitakuwa zinasoma wazazi.

TANO, kama hamuwezi kufanya lolote mapema kati ya hayo manne juu basi mmoja awe tayari kupoteza au msubiri mahakama iwaamue.

REJEA ya maandiko haya ni :-

Sheria ya ndoa R:E 2019 hasa vifungu vya 58,59,,60, na114.

NA

Shauri la Bi Hawa Mohammed vs Ally Sefu(Rufaa Na.9/1983) TZCA 12.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news