NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Jamhuri ya Kenya chini ya uongozi wa Rais Dkt.William Ruto imejitolea kushughulikia changamoto zote zinazowakabili Wakenya. Mheshimiwa Rais Dkt.Ruto amesema, Serikali kwa sasa inaangazia masuala yatakayobadilisha maisha ya watu wa kawaida.
Ameyasema hayo hivi karibuni katika kaunti za Narok na Kiambu ambako alizindua miradi ya maji na barabara, ambapo Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa, umoja na mshikamano ni msingi utakaowezesha nchi kusonga mbele.
Pia amewataka viongozi kuzingatia mabadiliko ya nchi na kuacha siasa. “Niko tayari kufanya kazi na viongozi wote kubadilisha Kenya. Nitafanya kazi na kiongozi yeyote anayetaka kuboresha maisha ya Wakenya,”alisema Mheshimiwa Rais Dkt.Ruto.
Rais alizindua mradi wa shilingi bilioni 1.5 za Kenya, Mradi wa Majitaka wa Narok Town akishirikiana na Magavana Patrick Ole Ntutu (Narok) na Joseph Ole Lenku (Kajiado), wabunge pia ni miongoni mwa viongozi walioshiriki katika hafla hiyo.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Dkt.Ruto alizindua Mradi wa Maji wa Shilingi Milioni 73 huko Suswa ambao utasambaza lita milioni tano za maji kwa siku kwa zaidi ya kaya 40,000 za eneo hilo.
Rais alisema, Serikali imetenga shilingi milioni 350 kwa ajili ya maji katika kaunti hiyo. "Tunajenga mabwawa na mifumo ya kusambaza maji kwa matumizi ya nyumbani na umwagiliaji ili tuweze kutokomeza njaa nchini Kenya," alielezea.
Baadaye, Rais Ruto akiwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua,Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Moses Kuria, Gavana wa Kiambu, Mheshimiwa Kimani Wamatangi, Kiongozi wa Wengi katika Bunge, Kimani Ichung'wa na wabunge walizindua uboreshaji wa kiwango cha lami cha kilomita 90 za barabara huko Gachie,Limuru katika Kaunti ya Kiambu.
Alibainisha kuwa, barabara hizo zitarahisisha usafirishaji wa mazao ya shambani na bidhaa sokoni.
“Hii itafungua fursa za kiuchumi kwa watu wa eneo hilo. Huu ndio mwelekeo wa Ajenda yetu ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya Chini kwenda Juu."
Rais Dkt.Ruto alisema Serikali inafanya kazi usiku kucha ili kuhakikisha inapunguza kupanda kwa gharama za maisha.