NA ADELADIUS MAKWEGA
HIVI karibuni Mwanakwetu alikutana na rafiki yake wa miaka mingi Yahane Lugendo, ndugu huyu wanafahamiana tangu miaka ya 1980 huku wakisoma masomo mbalimbali pamoja.
Ndugu Lugendo yeye ni mkazi wa Mbagala akiwa pia miongoni mwa Wakristo wa Waangalikana ambao mwanzoni hawakuna na Kanisa bali walikutana na kusali katika madarasa ya Shule ya Msingi Mbagalahuku kwa sasa wana makanisa mengi katika eneo lote la Mbagala.
Hivi sasa ndugu huyu ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni mojawapo ya ukandarasi wa umeme, ndugu Lugendo alimueleza Mwanakwetu namna kampuni anayoimiliki ilivyoingia katika shida katika miradi ya umeme wakati fulani na shauri hilo kupelekwa mahakamani. Mazungumzo haya yaliisha na kila mmoja kuchukua njia yake.
Mwanakwetu hapo sasa alikuwa yu Barabara ya Sita jijini Dodoma akatafuta sehemu ale chakula cha mchana, akapata mkahawa mmoja wa makabwela akaingia akawa anakula chakula chake mchana huo. Alipokuwa anakula Mwanakwetu akakumbuka kuna wakati wakiwa wadogo yeye na ndugu Lugendo walikwenda nyumbani kwa mama wa Mwanakwetu huko Mbagala Kizuiani jirani na nyumba ya Wageni ya Zimbwini hiyo ikiwa kati ya mwaka 1989-1990.
Walipofika hapo wakala chakula pamoja walipomaliza walitoka nje ambapo kulikuwa na duka la bidhaa, kando ya duka hilo walikutana na ndugu mmoja aitwaye Pandu wakifahamiana tangu utoto, ndugu Pandu na familia yake walikuwa wakimiliki nyumba kadhaa katika mtaa huo zikiwa nyumba za urithi baada ya baba yake kufariki dunia.
Baadhi ya nyumba hizo ziliuzwa na familia hii na wao kupata mitaji ya biashara, nyumba iliyokuwa kando ilinunuliwa na familia moja ambayo ilijulikana kwa majina ya watoto wao tu BabaTulo/Baba Agness, Mama Tulo /Mama Agness.
“Hapa tumepata wageni kutoka Temeke/Tandika, hawa si wageni wa Dar es Salaam bali ni wageni wa Mbagala.”
Mwanakwetu na Yohane Lugendo wakurudi Shule ya Msingi Mbagala lakini walifahamu kuwa nyumba hiyo ilishauzwa na akina Pandu huku akifanya biashara zake Mtaa wa Independence.
Kumbuka Mwanakwetu yu mkahawami anakula chakula Jijini Dodoma. Mwanakwetu akakumbuka kuwa aliendelea kwenda eneo hilo kwa sababu zingine kadhaa maana kulikuwa na rafiki zake aliokuwa akisoma nao Tambaza kama vile Rashidi Kazyoba, Harubu Harubu(Bakari Hamza), Yusufu Maulindi, Badi Ali, Hamisi Jangwa, Lastoni Katambala na wengineo.
Msomaji wangu Mwanakwetu yupo mkahawani vijiko vya wali vikiingia mdomo wake hapo alikumbuka kuwa Mbagala Kizuiani ilikuwa njia ya mkato kwenda Kanisani Parokiani Mbagala baada ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kuhamisha Parokia ya Mbagala kutoka Mbagala Misheni na kwenda Mbagala Zakhem.1987/1988. Kwa hiyo kila jumapili kupita njia hiyo ilikuwa ada huku akiona nyumba ya Baba Tulo/ Baba Agness.
Mwanakwetu anakula sasa sahani yake ya wali imekwisha akaagiza soda, ilipofika alipiga pafu moja la soda baridi hapo alikumbuka kuwa eneo la Mbagala Kizuiani lilikuwa pia na hudumu zote za kiserikali kama vile Shule, Zahananati, Mahakama, Ofisi za Kata na Soko Kubwa.
Hapo Mwanakwetu akinywa soda aliona miaka ilivyokuwa inasonga na baadaye alikumbuka kuwa rafiki yake Pandu alifariki dunia. Huku alikumbuka namna akipita hapo nyakati za asubuhi au jioni aliona familia ta Baba Tulo /Baba Agness wakiendelea na maisha yao. Nazo nyumba zilizobaki za akina Pandu zikibakia na wapangaji wageni tu.
Taswira hii ilimjia Mwanakwetu,
“Asubuhi alimuona Baba Tulo anadamka kwenda kwenye shughuli zake, jioni anarudi na vifurushi vya familia yake huku Tulo na Agness wakimpokea Baba yao mizigo hiyo.”
Msomaji wangu Mwanakwetu mkahawani alikumbuka mwaka 1992 Tanzania ikaingia katika mfumo wa vyama vingi, huku majina maarufu kama James Mapalala yalitambulika mno.
Mwaka 1995 uchaguzi wa vyama vingi ukafanyika huku sasa wanasiasa wapya wa upinzani wakifahamika. Mwaka 1995 Mwanakwetu alikuwa Kilimanjaro kama mwanafunzi, aliporudi na kwenda kumsalimu mama alikumbuka kuwa aliambiwa juu ya Baba Tulo/Agness amegombea ubunge jimbo la Temeke.
Mwanakwetu aliuliza anatumia jina gani ? Aliambiwa kuwa anaitwa Tambwe Hiza. Hapo ndipo Mwanakwetu akaanza kumjua ndugu huyu mkazi wa Mbagala Kizuiani akiwa mwanachama wa NCCR-MAGEUZI. Baadaye vyombo vya habari vilipambwa na kesi ya Ubunge Jimbo la Temeke na mahakama kutengua ubunge wa Mheshimiwa Ramadhani Ally Kihiyo.
“Sasa hivi Baba Tulo / Agness atakuwa mbunge maana mbunge wa CCM alikuwa hana vyeti, alighushi vyeti vya DIT.”
Haya sasa yalikuwa maneno ya mtaani Mbagala Kizuiani. Mwanakwetu akakumbuka baada kuamuliwa hivyo na mahakama NCCR walimpitisha Augustine Mrema kugombea ubunge wa Temeke nayeye Tambwe Hiza akahamia CUF safari ya Tambwe Hiza kisiasa iliendelea. Sasa Mwanakwetu akakumbuka namna alivyokuwa Dar es Salaam wakati huo akihudhuria mikutano kadhaa ya vyama vyote.
“Jamani si mmemsikia Nyerere mwenyewe tangu mwaka 1995 alisema kuwa Mrema anafaha sana kuwa mbunge ili akaipe changamoto Serikali Bungeni. Sasa NCCR imempumzisha ndugu Tambwe Hiza na kumleta Mrema ndugu zetu wa Temeke amepitishwa ili akaifanye kazi hiyo vizuri si mlimuona alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi? Sasa kamilisheni hilo.”
Mikutano kadhaa iliyofanywa na NCCR MAGEUZI walinadi hilo wazi wazi, Mwanakwetu alikumbuka. Kumbuka soda ya Mwanakwetu mezani inaendelea kushambuliwa na koo lenye kiu ya joto kali ya Dodoma la mwezi Machi 2023 siku hiyo pia Mwanakwetu akayambuka maneno haya,
“Kampeni zilikuwa nzuri sana na zikivutia mno, majigambo ya kila aina, uwezo wa kujieleza kwa wagombea wote Abdul Cisco Mtiro akipewa nafasi ya kushinda na huku ikinadiwa kuwa yeye ndiye mgombea pekee mzaliwa na aliyesoma shule hapo Temeke, huku Tambwe Hiza akigombea kupitia CUF. Kura zikapigwa na matokeo kutangazwa Richard Tambwe Hiza alipata kura 3324, Mrema Augustine alipata Kura 54,850, huku Cisco Mtiro wa CCM alipata kura 33,113. Mrema akawa Mbunge wa Temeke.”
Mwanakwetu alitoka hapo mkahawani na kwenda kuchimba dawa kidogo alafu akarudi. Akiwa ameketi alikumbuka hawa NCCR wakavurugana hilo likasababisha Mrema kwenda TLP na kupoteza ubunge wa Temeke.
Ukafanyika uchaguzi tena wa Jimbo la Temeke John Kibaso ambaye awali alikuwa diwani wa Kurasini wa CCM alipata kura 27,090 Abbas Mtemvu huyu ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam alipata kura 14,701 na Tambwe Hiza alipata kura 25,742. Mbunge wa Temeke akawa Mheshimiwa John Kibaso wa CCM. Baada ya hapo Tambwe Hiza aligombea sana kupitia CUF lakini hakufua dafu.
Maisha ya kisiasa ya yalibadilika Tambwe Hiza alirudi CCM, Mwanakwetu aliyekuwa mtoto mwaka 1988 sasa akakutana kwenye siasa na Tambwe Hiza. Mwanakwetu yu mkahawani alikumbuka kuwa kura za maoni CCM kwa mwaka 2015.
“Jamani mimi sina pesa ya kuwahonga wana CCM wezangu, lakini kuweza kuwafanyia kazi kama Mbunge ninaweza sana. Ndiyo maana chama chenu wao wenyewe wamenipa kazi kubwa ya kubwa. Shauri ni lenu mambo yawe yaleyale au mnichague mimi Tambwe Richard Hiza nikaiwakilishe Mbagala Bungeni.”
Wanachama wa CCM katika Mkutano uliofanyika kata ya Chamazi wakawa wanacheka. Mwanakwetu alikumbuka walipofika Kata ya Mbagala ambapo mkutano ulifanyika katika ukumbi mmoja Jirani na Mbagala Moringe jirani na makazi ya Tambwe Hiza hapo ndugu Mwanakwetu alitoka ndani ya basi na kwenda dukani kununua soda, jamaa wa dukani akasema maneno haya,
“Kuna baadhi ya wazazi, watoto wao wanateseka mno pale kunapotokea migogoro ya ndoa na mara nyingi mama ndiye anayebaki na watoto, Jambo hilo linasumbua familia nyingi. Baba anatakiwa kuwa makini kunapotokea shida kama hizo. Hapo kunahitajika umakini mkubwa na uvumilivu wa hali ya juu, wazazi tusiwe watu wa kulipizana kisasi baada ya magomvi ya ndoa.Tambwe Hiza nimemuona karudi CCM na anagombea, hilo ni jambo zuri sana kama ningekuwa nina kadi ya CCM ningempigia kura yeye maana ni mtu mwenye kujali watu , kujali watoto wake na siyo mtu wa kisasi.”
Mwanakwetu yu mkahawani alikumbuka habari hii ya muuza duka alipokwenda kununua soda siku ya Kura za Maoni CCM 2015. Mwanakwetu kimoyomoyo akasema yale maneno ni ya kweli maana akimfahamu Tambwe Hiza kitambo. Wakiwa katika basi la Watia Nia wa CCM kwenda kuomba kura Kata ya Mtoni KIjichi ndani ya basi hilo kuliibuka mjadala juu ya mgombea Urais wa CCM wakati huo marehemu John Pombe Magufuli, Swali lililoibuka Je ni kweli CCM walijipanga kumchagua Magufuli kuwa mgombea wao mwaka 2015? Kuliibuka upande mmoja uliomeza watu wote isipokuwa Mwanakwetu , Dereva na Kijana wa Chama aliyepangwa na CCM wilaya kusimamia nidhamu za wagombea ndani ya basi.WEngi wakisema ushindi wake ndani ya chama uliibuka tu baada ya baadhi ya kambi kuondolewa katika mchakato huo.
“CCM walikuwa wanajua sana kama Mgombea wao wa Rais mwaka wa 2015 ni John Pombe Magufuli kwa kuwa vikao vingi vilivyotangulia vya CCM vikubwa vikubwa ambayo John Pombe Magufuli hakuwa mjumbe halali alialikwa huku Mwenyekiti wa CCM akisema mengi ya kumpamba na akipewa nafasi ya kuelezea mambo mbalimbali.Mimi kama mwanasiasa nililishitukia mapema.”
Haya yalikuwa maneno yake mwenyewe Richard Hiza Tambwe katika Coaster hiyo iliyokodiwa na CCM Wilaya ya Temeke kwa shughuli za kuomba kura za wana CCM katika kata zake za jimbo la Mbagala. Hapo Tambwe Hiza alipata kura chache mno ndipo akaenda CHADEMA
Kumbuka msomaji wangu hayo juu anayakumbuka tu namna ilivyokuwa mwaka 2015 akawa amemaliza kunywa soda yake akalipa pesa na kutoka zake hapo kuelekea Makole kupanda basi za Chamwino-Ikulu. Alipofika Makole akapanda basi za Chamwino Ikulu na kuianza safari. Mwanakwetu akawasha simu yake kufungua na kutazama baadhi ya video za mikutano ya aliyofanya Tambwe Hiza mara alipohamia CHADEMA.
“Nilikuwa pale CCM makao makuu, Katibu Msaidizi wa Chama, Mkuu wa Prapaganda. Mama yangu Agness yupo huko, ameshakufa, mimi nimekwenda kujificha CCM nikamuonea aibu nikatoka…”
Mwanakwetu akakumbuka kuwa CCM ilishinda uchaguzi huo 2015 akiwa ndani ya basi hilo alipitiwa na usingizi kidogo kama dakika45 hivi na gafla alishtuka baada ya simu yake kuanguka chini na abiria mwanzake kuiokota na kumpa.Alipopewa simu hiyo Aliona ile video bado ipo katika sura ya simu yake na akaitoa na kuona habari za msiba wa Richard Tambwe Hiza ambao ulitokea Februari 8, 2018.
Mwanakwetu akakumbuka siku ya msiba ya msiba huo alishiriki akitokea Lushoto Tanga akafika nyumba kwa Tambwe Hiza Mbagala Kizuiani. Huku akikutana na wana CCM wachache mno labda wakubwa wakubwa walikuwa ni Mzee Mkali ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam zamani na Mzee Mbonde ambaye aliwahi kuwa Katikbu wa CCM wa wilaya mbalimbali zamani.
Mwanakwetu akauliza ,
“Mzee Mkali kumbe mtu akiondoka chama chetu kwenda upinzani ndivyo tunavyotakiwa kufanya? Hatushiriki kumzika ndugu huyo?”
Mzee Mkali alisikitika mno, akasema huo siyo utaratibu wa chama chetu na siyo CCM tu hata TANU hatukuwa hivyo.
“Nyinyi vijana mtambue kuwa kupishana ki kimtazamu, kiitikadi ndiyo siasa yenyewe na hiyo siyo vita. Kama mimi ningefariki kabla yake(Tambwe Hiza) nina hakika ndugu yangu huyu angekuja kwangu kunizika.”
Mwanakwetu ibada ya mazishi ilipoisha waombolezaji walitoka nyumbani kwa Tambwe Hiza Mbagala Kizuiani na baadaye mazishi kufanyika makaburi ya Maduka Mawili Wilaya Temeke Dar es Salaam.
Mwanakwetu akiwa ndani ya basi la Chawmino Ikulu alibani kuwa Februari 8, 2023 mwaka huu ilikuwa ni miaka mitano baada ya kifo cha Tambwe Hiza. Mwanakwetu alifika kwake na kuendelea na shughuli zake akaamua tafakari hiyo ya Richardi Tambwe Hiza ya tangu mwaka 1988 hadi 2018 yaani miaka 30 aiweke katika simulizi hii maana alikuwa ni mkazi mwenzake wa Mbagala, alikuwa jirani wa mzazi wake, alikuwa mwanaCCM mwenzake na alikuwa Mkuu wa Propaganda wa CCM Taifa.
Mwanakwetu upo?
Tafakari hii siku ya leo ina anuani hii,
“Tuna Wajibu wa Kuzikana Hata Kama Tukitafautiana Kisiasa.”
Nakutakia Pasaka Njema.
makwadeladius@gmail.com 0717649257