Vinara dawa za kulevya wadakwa mkoani Mara

NA GODFREY NNKO

ZAIDI ya watuhumiwa 39 ambao wanatajwa kuwa ni vinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya na uuzaji wa pombe haramu ya gongo wamekamatwa mkoani Mara.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi wa Polisi Longinus Tibishubwamu wakati akizungumzia kuhusu kushikiliwa kwa watu hao kwa makosa ya usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya aina ya bangi ikiwemo mirungi.

Amesema, watuhumiwa hao wamekamatwa kwa vipindi tofauti ndani ya mwezi Machi, mwaka huu kutokana na oparesheni inayoendelea mkoani humo.
Kamishna Msaidizi wa Polisi Longinus Tibishubwamu amesema,miongoni mwa watuhumiwa hao wapo waliokamatwa kwa makosa ya uuzaji wa pombe ya gongo (moshi) ambapo jumla ya lita 384 pamoja na mitambo miwili ya kutengeneza pombe hiyo vimekamatwa.

Pia katika oparesheni hiyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limekamata kila 87 za dawa za kulevya aina ya bangi ikiwemo misokoto 34.
Wakati huo huo, Kamanda Tibishubwamu amewataka wakazi wa Mkoa wa Mara kuacha mara moja kujishughulisha na biashara hiyo haramu na badala yake kueukia fursa zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Mara ikiwemo uvuvi, uchimbaji madini na kilimo.

Bangi ni nini?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), bangi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Cannabis sativa” ambao hustawi na hutumika kwa wingi hapa nchini na duniani kote. 
Bangi huathiri ubongo na kubadili jinsi tunavyotafsiri uhalisia wa vitu. Majani na maua ya mmea huo hukaushwa na hutumiwa kama kilevi peke yake au kwa kuchanganywa na dawa zingine. 

Mara nyingi bangi imekuwa ni kati ya dawa ya awali kutumiwa, ambapo watumiaji wengi huanza matumizi wakiwa na umri mdogo hivyo kuwa katika hatari zaidi kiafya, kijamii na kiuchumi. 

Aidha, watumiaji wengi wa bangi huishia kutumia dawa nyingine hapo baadae kama heroin na cocaine. Hivyo, bangi hutumika kama njia ya kuingia katika matumizi ya dawa nyingine za kulevya. 

Majina mengine ya bangi yanayotumika mitaani ni kama msuba, dope, nyasi, majani, mche, kitu, blanti, mboga, sigara kubwa, ndumu, msokoto, ganja na mengineyo.

Sheria inasemaje?

Kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95, kilimo na biashara ya bangi katika Taifa letu ni kosa la jinai. 

Kwa hiyo, kujihusisha kwa namna yoyote na bangi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia, kuichakata, nk) ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha jela.

Mirungi Je?

Kwa mujibu wa DCEA, mirungi ni aina ya dawa ya kulevya inayotokana na mmea unaoitwa “Catha edulis”. Mmea huo una kemikali za cathinone na cathine ambazo huongeza kasi ya utendaji wa mfumo wa fahamu. 

Mirungi ilikuwa inatumika tangu enzi za mababu kwenye nchi za pembe ya Afrika hususani Ethiopia, Eritrea, Kenya, Somalia pamoja na Rasi ya Arabuni nchini Yemen. 

Aidha, mirungi hutumika zaidi kwenye mikusanyiko ambayo hujumuisha zaidi wanaume ingawa katika miaka ya karibuni wanawake wamejiingiza katika matumizi. 
Nchini kwetu mirungi hustawi na hupatikana kwa wingi katika mikoa ya Kilimanjaro huko Same, Tanga huko Lushoto na Arusha huko Mlima Meru. 

Kiasi kingi cha mirungi huingizwa nchini isivyo halali kutoka nchi jirani ya Kenya ambako ni zao halali la biashara. Mirungi hufahamika kwa majina ya gomba, veve, miraa, kangeta, mkokaa, colombo, asili, mbaga, alenle na nyinginezo.

Sheria inasemaje?

Kwa mujibu wa DCEA, mirungi katika taifa letu ni haramu.Kujihusisha kwa namna yoyote na mirungi (kulima, kuuza, kuhifadhi, kutumia) ni kosa la jinai na adhabu yake inafikia hadi kifungo cha maisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news