Wakikuyu wapanda Mlima Kenya kushusha bendera ya mashoga na wasagaji, waipiga kiberiti

NA DIRAMAKINI

WAJUMBE kadhaa wa kimila kutoka kabila la Wakikuyu nchini Kenya wameharibu bendera inayodaiwa kuwakilisha jamii ya mashoga na wasagaji ambayo iliripotiwa kupandishwa kwenye kilele cha Mlima Kenya mwaka 2019.
Kwa mujibu wa runinga ya Citizen, kundi hilo, chini ya bendera ya Booi wa Kirira Kia Mugikuyu, iliyotafsiriwa kuwa ni 'mkusanyiko wa utamaduni wa Kikuyu', katika muda wa mwezi mmoja uliopita limekuwa likichangisha fedha kwa ajili ya kupanda mlima na kuondoa bendera inayodaiwa kuwakilisha jumuiya ya LGBTQ.

Timu ya wapanda mlima wapatao 10 walipanda mlima Aprili 7, na kurejea Aprili 9,2023 wakiwa na bendera inayodaiwa kuchomwa moto katika eneo la Naromoru, Kaunti Ndogo ya Kieni Mashariki, Kaunti ya Nyeri.

Tukio hilo lilifuatiwa na ibada za utakaso za wazee wa Kikuyu.Walisema majivu ya bendera iliyoungua yatatupwa kwenye mto unaoelekea Bahari ya Hindi.

Kundi hilo linasema kuwa, kupandisha bendera inayodaiwa kuwakilisha jumuiya ya LGBTQ kwenye Mlima Kenya kulikuwa na athari ya kunajisi mahali patakatifu pa Wakikuyu.

Kulingana na utamaduni wa Wakikuyu, Mlima Kenya ni makazi ya Mwenenyaga, mungu wao. Huwa Wakikuyu wakisali wanatazama mlima kwa ajili ya mapokeo ya baraka.

"Ni dharau kwa hali ya kiroho ya Gikuyu, kwa wanajumuiya hii kunajisi madhabahu yetu ya juu kwa kuinua bendera yao kwenye Kīrīnyaga (Mlima Kenya).Tulidhamiria kuishusha bendera na baada ya hapo kufanya ibada za utakaso na wahenga wetu," anasema Kimani Charagu, mwanachama mwanzilishi wa Booi wa Kirira.

Mjumbe mwingine wa kikundi hicho, Ngarau Njonjo, aliyekuwa katika timu iliyopanda mlima huo, alisema kung’oa bendera tajwa na kufanya sherehe za utakaso ni ujumbe mzito kwamba jamii haitatumika kama jalala la mgeni wa kila aina kufanya mazoea na mila zao.

Murugu wa Kimari, ambaye ni mweka hazina wa Booi wa Kirira, amesema wao ni njia ya kuhifadhi utakatifu wa Mlima Kenya pamoja na utamaduni wa Wakikuyu.

“Watu wetu wanapaswa kutulia na kujiuliza ni kwa nini mambo haya yote mabaya yanatokea katika jamii, ikiwa ni pamoja na mauaji yasiyoelezeka karibu kila siku,” alieleza Murugu, ambaye pia ameandika kitabu kuhusu utamaduni wa Wakikuyu. "Hii ni dalili tosha kwamba Mwenenyaga hajafurahishwa nasi,"ameongeza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news