Watoto wenye matatizo ya macho wawahishwe hospitali mapema-Dkt.Mshangila

NA MWANDISHI WAF

WAZAZI wametakiwa kuwapeleka watoto wenye matatizo ya mtoto wa jicho wanayozaliwa nayo au yaliyotokana na majeraha ili kupata matibabu sahihi na kumuwezesha ubongo kukua vizuri na kuona vizuri.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari Bingwa wa Macho kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH),Dkt. Barnabas Mshangila kwenye kambi ya upasuaji wa mtoto wa jicho inayoendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali ambayo inaratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Hellen Killer International la hapa nchini.
 
Dkt. Mshangila amesema kawaida mtoto anapokua anatakiwa macho yake yaone vizuri ili ubongo na wenyewe uweze kukua hivyo mtoto anapoumia akiwa chini ya miaka (7) na asipopelekwa hospitali kufanyiwa upasuaji husababisha kutokuona vizuri ukubwani.
“Mtoto asipofanyiwa matibabu kwa wakati na anapofanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho akiwa mtu mzima, jicho huwa halioni vizuri kwani mwanga unakuwa haujaingia wa kutosha na kufanya ubongo nao usikue, ushauri wangu ni vyema wazazi kuwapeleka kwenye vituo vya afya watoto kwa ajili ya uchunguzi pale mtoto anapopata majeraha kwani anaweweza asisikie maumivu,"amesema Dkt. Mshangila.

Kwa upande wa waliofanyiwa upasuaji Dkt. Mshangila amesema ni vyema wakafuata masharti wanayopatiwa ikiwemo kutokufanya kazi ngumu na kutokukaa sehemu yenye moshi pamoja na vumbi pia kuhudhuria kliniki na kuonana na wataalamu kwa tarehe walizopangiwa.
Aidha, amesema mtu aliyefanyiwa upasuaji wa mtoto wa jicho tatizo hilo haliwezi kujirudia mara baada ya upasuaji ila wapo baadhi ya watu huwa inaweka ukungu kwenye sehemu ambayo inaachwa wakati wanaweka lenzi ya mwanzo.

"Kuna wachache inaweka ukungu kwa kuona jicho linafifia tena lakini inakua sio kama mtoto wa jicho la mwanzo na huwa labda baada ya miaka mitatu, akija hospitali upasuaji wake huwa sio mkubwa na hurudi kuona tena,"amesema.
Hata hivyo amewatoa hofu baada ya watu ambao wana matatizo ya mtoto wa jicho ambao hudhani akifanyiwa upasuaji hawawezi kuona tena na kuwasihi kujitokeza kwa wingi ili kuweza kupatiwa huduma hizo ambazo zimesogezwa karibu na makazi yao.

Dkt. Mshangila ameongeza kuwa yapo matatizo mengine yanayosababisha upofu ambao hautibiki hivyo kama wataalamu kabla ya upasuaji wa mtoto wa jicho huwafanyia uchunguzi kama kuna shida nyingine kama presha ya macho, huwashauri wajue endapo watafanyiwa upasuaji hawatoona vizuri.
Mtoto wa jicho ni tatizo linalosababisha ukungu kwenye kioo (lenzi) ambapo mboni ya jicho hubadilika na kuwa jeupe na hivyo upasuaji hufanyika ili kutoa lenzi yenye ukungu na kuweka lenzi isiyo na ukungu na visababishi vyake ni mabadiliko ya mwili yanayoambatana na umri.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news