NA ADELADIUS MAKWEGA
CHUO cha Maendeleo ya Michezo Malya Mkoani Mwanza kimezindua Dawati lake la Jinsia na kufanya mdahalo maalumu juu ya kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili katika jamii ya Tanzania leo Aprili 25, 2023, huku jamiii ya Watanzania ikiaswa kila mzazi au mlezi kutunza familia yake ipasavyo na kwa kufanya hivyo kunaweza kusaidia kupunguza mimomonyoko ya maadili katika jamiii.
Akizungumza katika tukio hilo Makamu Mkuu wa Chuo hicho kinachotoa kozi mbalimbali za michezo nchini, ndugu Alex Mkenyenge amesema kuwa, wanachuo wake ambao ni wanamichezo na walimu wa michezo wanatakiwa kuwa na maadili zaidi kuliko mtu yoyote maana michezo inahitaji nidhamu ya hali juu ili kuupata ushindi.
“Nyinyi kama wanamichezo, wazazi au walezi na vijana wa Kitanzania mna wajibu wa kuhimiza kila mlipo watu watimize wajibu wao,”amesema.
Akizungumza katika mdahalo huo uliwakutanisha wakurufunzi zaidi ya 150, wakufunzi na watumishi zaidi ya 20 na wakaazi kadhaa wa Kijiji cha Malya, Mwenyekiti wa Kijiji cha Malya mheshimiwa Leonardi Mayunga alikishukuru sana chuo hiki kwa kumualika katika shughuli hiyo akisema hayo ndiyo mahusiano mema baina ya taasisi za umma na wanakijiji.
"Kwa kuwa watu wengi wanatazama utamaduni wa kimagharibi kama mwongozo wao, kumbe utamaduni huo unaipotosha dunia yetu. Yapo mambo mazuri kama vile tekinolojia zao lakini ndani yake hata hiyo tekinolojia ni balaa linakuja mathalani simu hizi za mikononi.”
Mwenyekiti huyo wa kijiji hiki kilichopo katika Wilaya ya Kwimba amesema kuwa hata kijiji chao kinapata shida hiyo na ndiyo maana wamepitisha sheria ndogo kwa kila yule anayekamatwa akivaa nguo fupi anapigwa faini ya shilingi 10,000. Huku akiwaomba wanachuo hao wasiingie katika mkumbo huo.
Wakichangia mawazo yao wakufunzi wote kwa pamoja walikubaliana kuwepo kwa shida ya mmomonyoko wa maadili huku wakipishana namna ya kuielekea changamoto hiyo tu, lakini kwa kauli moja wanaungama kuwa kwa hali ilivyo inahitaji kupambana nayo bila kusita kwa kila mmoja wetu.
Akitoa neno la shukrani katika hitimisho la mdahalo huo Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia, Bi.Hapifania Mugaga amesema kuwa, kazi za dawati la jinsia zimeanza na jukumu la kila mmoja wao kutoa ushirikiano kwa kamati yake punde mtu yoyote anapohitajika.