NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amewataka wananchi wanaokabidhiwa hati milki za ardhi kuhakikisha wanazingatia masharti yaliyopo kwenye hati sambamba na kufuata mipango kabambe ya maeneo husika.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na wananchi katika eneo la Shibula Manispaa ya Ilemela Mkoa wa Mwanza wakati wa zoezi la kutoa hati Aprili 17, 2023. Kulia ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza, Happy Mtutwa.
Mheshimiwa Dkt.Mabula amesema hayo Aprili 17, 2023 katika eneo la Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza wakati wa zoezi la kutoa Hati Milki za Ardhi kwa wananchi wa eneo hilo. Jumla ya hati 570 ziliandaliwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa eneo hilo.
"Huwezi kupata hati leo, kesho unaenda kuomba kubadili matumzi mwisho wake miji inaonekana haina maana na haipendezi na sisi tunataka Jiji la Mwanza na Ilemela ikiwemo liwe mfano, tunapima viwanja vingi kwa ajili ya uwekezaji tuzingaite kilichopo kwenye Master Plan,’’amesema Dkt.Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula akimkabidhi hati mmoja wa Milki ya Ardhi waliopatiwa hati katika eneo la Shibula Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mkoa wa Mwanza tarehe 17 Aprili, 2023. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala.
Pia amewaonya wanaopata hati milki za ardhi kutobadili matumizi na kuwaagiza watendaji wa sekta ya ardhi na uongozi wa Wilaya ya Ilemela kuhakikisha hakuna kubadili matumizi na badala yake wamiliki wazingatie masharti ya hati na yale matumizi yaliyopo kwenye mpango kabambe.
Akigeukia suala la utoaji Hati Milki za Ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Dkt.Mabula ameshangazwa na idadi ndogo ya wamiliki waliojitokeza kuchukua hati ambao ni 50 kati ya 570 walioandaliwa kuchukua hati.
Baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Ilemela Mkoa wa Mwanza waliojitokeza kupatiwa hati milki za ardhi wakati wa zoezi la utoaji hati lililofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula katika eneo la Shibula.
"Watu wana tabia ya kulalamika hati hazitoki, tuna hati 570 hapa waliojitokeza ni 50 tu, hao wengine wako wapi ni kitu ambacho hakieleweki, hati zinaandaliwa, lakini hamji kuchukua, hizo zinazobaki naomba muangalie namna mtakavyotoa,"amesema Dkt.Mabula.
Ametaka wamiliki wa ardhi walioshindwa kuchukua hati kuandaliwa utaratibu maalum wa kupatiwa hati hizo huku akieleza kuwa, idara ya ardhi katika Halmashauri ya Ilemela kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mwanza kuchagua sehemu moja na kutumia wiki mbili kutoa hati kwa wahusika ili ziweze kuisha na kuendelea na hati nyingine ambazo ziko katika mchakato.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mkoa wa Mwanza, Hassan Masala akizungumza katika zoezi la utoaji hati milki za ardhi lililofanyika eneo la Shibula Manispaa ya Ilemela.
Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameeleza kuwa, wizara yake iko katika mageuzi makubwa ya kubadilisha mifumo yake lengo likiwa kuweka taarifa za ardhi sawa, kuondoa migogoro ya ardhi pamoja na kuwezesha serikali kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.
"Mifumo inaboreshwa na taarifa za sekta ya ardhi zinaenda kukaa vizuri na sasa taarifa ya kudaiwa kodi ya ardhi utaipata kupitia simu yako ya kiganjani na unapopata ujumbe nenda kalipe maana huhitaji kwenda ofisini,’’amesema Dkt.Mabula.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akifurahia jambo na mwananchi ambaye ni shabiki wa timu ya Simba baada ya kumkabidhi hati katika eneo la Shibula Manispaa ya Ilemela Mkoa wa Mwanza ikiwa ni siku moja baada ya Simba kuifunga Yanga mabao 2-0.
Kufuatia hatua hiyo, Dkt Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kutimiza majukumu yao na kusisitiza kuwa asingependa watanzania wenye shida kwenda ofisi za ardhi na kuelezwa njoo kesho na kuweka bayana kuwa kama suala haliwezekani ni bora kuelezwa ukweli.
Amesema, maboresho makubwa yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt samia Suluhu Hassan,kwa wizara yake kupatiwa fedha nyingi hasa ikizingatiwa Wizara ya Ardhi ni wezeshi na isipowawezesha wananchi itamuangusha Mhe.Rais na yeye asingependa kumuangusha.
Mmoja wa wananchi wa Ilemela akikabidhiwa hati na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula wakati wa zoezi la kutoa hati kwa wananchi wa Halmashauri ya Ilemela. (Picha na WANMM).
Vile vile, Dkt.Mabula amewataka wamiliki wa ardhi waliowekewa alama za mipaka (Beacons) katika maeneo yao kuhakikisha wanakamilisha taratibu za umilikishwaji ili waweze kupatiwa hati milki za maeneo yao kwa lengo la kuziweka ardhi zao salama.
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni moja ya halmashauri nchini zilizonufaika na mkopo usio na riba kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ambapo katika awamu ya pili halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha shilingi bilioni 3.589.