NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama amewataka wataalam kushirikiana na wakandarasi ili kuhakikisha ujenzi wa Mnara wa Mashujaa unakamilika katika viwango vyenye ubora.
Mbunifu Majengo kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bwa. Noel Gustav akiwasilisha muonekano wa ramani ya Mnara wa Mashujaa wakati wa kikao cha kumpitisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Hayupo pichani) utakaojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).
Mhe. Mhagama ameyasema hayo wakati wa kikao chake na Wataalam, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo Mbalimbali katika Ofisi hiyo waliokutana kwa lengo la kumpitisha katika ramani ya ujenzi wa Mnara huo katika kikao kilichofanyika Ukumbi wa Ofisi hiyo Jijini Dodoma.
Mhe. Mhagama amesema ujenzi wa Mnara huo kwa Awamu ya Kwanza unatarajiwa kugharimu shilingi Bilioni Moja ukitarajiwa kukamilika mapema kabla ya maadhimisho ya Mashujaa mwaka 2023.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza wakati wa kikao chake na Wataalam, Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo Mbalimbali katika Ofisi hiyo kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi hiyo jijini Dodoma.
“Kukamilika kwa Mnara huu itakuwa ni hatua kubwa sana kwa Serikali kama sehemu ya kuwakumbuka mashujaa wetu jinsi walivyoipigania Nchi yetu na utakuwa wa kipekee sana na nembo kubwa kwa Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma. Watanzania watapata fursa ya kutembelea hapo na kujifunza yaliyofanywa na Mashujaa wetu,”amesema Mhe. Mhagama.
Baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) wakifuatilia kikao hicho.
Vilevile Mhe. Mhagama amesisitiza matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali kukamilisha ujenzi huo kuhakikisha zinatumika kama ilivyopangwa ambapo kukamilika kwake kutafungua fursa nyingi za kiuchumi kutokana na miundo mbinu rafiki na huduma muhimu zitakazowekwa katika mnara huo.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.Batholomeo Jungu akifafanua jambo katika kikao cha kumpitisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) katika ramani ya ujenzi wa Mnara wa Mashujaa utakaojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.
Aidha, amebainisha kwamba ujenzi wa Mnara huo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa maadhimisho ya siku ya Mashujaa yaliyofanyika mwezi Julai mwaka 2022 ambapo aliagiza kujengwa kwa Mnara wenye ubora na hadhi ya makao makuu ya nchi Dodoma.