NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kasim Majaliwa amewataka viongozi wa dini nchini kuhakikisha wasimamia haki na kuienzi na kusimamia amani kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.


Mheshimiwa Majaliwa amesema hayo leo Aprili 16, 2023 katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula wakati wa Ibada ya Harambee ya Ujenzi wa Shule ya Kanisa la Kiinjili la Kikutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki Ziwa Victoria-Mwanza iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Imani wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Kupitia harambee hiyo ya ujenzi wa Shule ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria-Mwanza kanisa hilo limefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 119,563,000 zikiwemo fedha taslimu, ahadi na vifaa.
Aidha, kupitia hotuba yake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka viongozi wa dini nchini kutochoka kufundisha na kulea vijana katika maadili mema na kuthamini kufanya kazi halali.

"Katika nyakati hizi ni ukweli ulio wazi kuwa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii yetu, vitendo viovu na mambo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu yanazidi kuongezeka, mambo ambayo siku za nyuma yalikuwa nadra sana kutokea au kusikia, lakini sasa yanakuwa habari za kila siku na wakati mwingine huonekana eti ya kawaida,"amesema Waziri Mkuu Majialiwa kupitia hotuba yake.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kushuka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya kwa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo kunachangia sana na kurudisha nyuma juhudi za kujiletea maendeleo na kuifanya kazi ya kuondoa umaskini kuwa ngumu.
Amesema, anaamini kwa dhati kuwa viongozi wa serikali, dini na vyama vya siasa wakishika mafundisho ya dini na kuwa na hofu ya Mungu, maovu mengi yatapungua na nchi kuoongozwa vizuri.
"Naendelea kuwaomba kwa niaba ya Serikali, viongozi wa dini zetu zote tusaidiane kulea taifa letu kimaadili na tuweke mkazo zaidi kwa vijana kwa sababu kwanza wao ndiyo wahanga wakuu wa maovu yanayotendeka, lakini pia wao ni taifa la leo na viongozi wa kesho,"amesema.

Kupitia hotuba yake hiyo, Majaliwa amesisitizia pia suala la elimu na kueleza kuwa elimu ni muhimu kwa maendeleo ya taifa lolote na kutaka viongozi wa dini kusaidia kuzungumza na wazazi na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kusomesha watoto.
Pia amelipongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria-Mwanza na waumini kwa ujumla kwa kujitoa kwa hali na mali kwa kufanya kazi ya Mungu kwa kuhakikisha jengo linakamilikia hasa ikizingatiwa fedha zote ni michango ya waumini na kubainisha kuwa, kitendo kilichofanyika ni chema na kinaleta baraka zote.



Katika harambee hiyo ya ujenzi wa shule Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alichangia shilingi milioni 5 ili kutumika kukamilisha kazi ya ujenzi wa shule huku Dkt.Mabula akichangia shilingi milioni 2 katika ujenzi huo.