NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini waendelee kupiga vita vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa jamii ili kulifanya Taifa kuwa mahali salama kwa watoto na Watanzania kwa ujumla.
Ametoa wito huo leo Ijumaa Aprili, 14, 2023 alipofungua msikiti wa ‘Masjid Ali Bin Saif’ uliopo Vingnguti jijini Dar es Salaam. Msikiti huo umejengwa na familia ya Sheikh Seif Ali Seif.
Amesema kuwa, moja kati ya msisitizo mkubwa wa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto, mmomonyoko wa maadili.
“Tukiachia mmomonyoko wa maadili, tunaweza kutengeneza Taifa ambalo halitakuwa na manufaa mbeleni, Viongozi wa dini mmekuwa mstari wa mbele katika kukemea ukatili dhidi ya watoto.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ni budi kwa Watanzania kuhakikisha wanapiga vita matendo yote yanayoharibu utamaduni, mila na desturi ya mtanzania “Tunayoyasikia huko duniani tuombe yasije hapa nchini na kama yapo tuyapige vita, Taifa hili leo tupo hapa na viongozi walioongoza nchi hii walisimamia kwenye mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka waumini wa dini ya kiislam kuutumia mwezi mtukufu wa ramadhan kuliombea taifa ili mwenyezi Mungu aendelee kuilinda na kudumisha amani, kuikinga dhidi ya maradhi na majanga mengine.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema amesema amevutiwa na ubora na uzuri wa msikiti huo. “Msikiti wa Ali bin Saif umejengwa kwa viwango vya juu sana hadi natamani na mimi pia ningekuwa mkazi wa Vingunguti ili na mimi nipate raha ya kusali kwenye Msikiti huu.”