NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameizungumzia Wiki ya Ubunifu kama sehemu ya mkakati wa Serikali katika kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Waziri Mkenda amezungumza hayo jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa wahabari kuhusu wiki hiyo itakayoanza Aprili 24 – 28, 2023 katika viwanja vya Jamhuri jijini humo ambapo amesema kukiwa na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu itaharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amsema tayari bunifu 38 zimeshaingia sokoni ambazo zimetokana na mashindano ya MAKISATU ambayo tangu mwaka 2019 Wizara kwa kushirikiana wadau imekuwa ikiyaendesha kwa lengo la kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini.
“Labda niwaambie tu juhudi hizi zimetusaidia kuwa na bunifu ambazo tayari zimeanza kuingia sokoni moja wapo maarufu sana ni ile ya mita ya maji ambayo inafanyiwa majaribio sasa imeanza kubihasharishwa,”ameongeza Prof. Mkenda.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa wiki hiyo itatoa fursa kwa wabunifu, wagunduzi, watafiti watunga sera, wadau wa maendeleo na washirika wengine kukutana na kujadili sera kanuni na miongozo mbalimbali kuhusu maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema, wiki hiyo itatanguliwa na maadhimisho katika ngazi ya mikoa na halmashauri ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Iringa, Morogoro, Tanga, Arusha, Mwanza, Kigoma, Kagera, Mara, Ifakara, Njombe, Mtwara, Kilimanjaro, Songwe na Unguja Magharib kupitia kumbi mbalimbali za ubunifu.
Waziri Mkenda ametumia fursa hiyo kuwaalika Taasisi, Mashirika, Wizara za kisekta na wananchi wote kushiriki katika maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu Tanzania yenye kauli mbiu Ubunifu kwa Uchumi Shindani.
Maadhimisho ya wiki ya ubunifu yatahusisha maonesho ya ubunifu na teknolojia kutoka taasisi za elimu ya juu, Taasisi za utafiti na Maendeleo, mashirika na makampuni ya umma na binafsi, mamlaka ya Elimu na mafunzo ya ufundi stadi VETA, shule za Sekondari na Msingi na wabunifu walioendelezwa katika program ya MAKISATU.