NA JAMES MWANAMYOTO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wametoa wito kwa watumishi wa umma nchini kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, ubunifu na ushirikiano ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza azma yake ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akifurahia jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama kabla ya Mawaziri hao kukabidhiana ofisi jijini Dodoma.
Mhe. Simbachawene na Mhe. Jenista wametoa wito huo kwa watumishi wa umma, wakati wa hafla ya makabidhiano ya ofisi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) jijini Dodoma ikiwa ni siku chache tangu wateuliwe na kuapishwa tarehe 2 Aprili, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa walizonazo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ya ofisi, Mhe. Simbachawene amewataka watumishi wa umma kuendelea kuchapa kazi ili kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za umma.
Mhe. Simbachawene amesema, ili taifa lipate maendeleo ni lazima kila Mtanzania anayepata nafasi kuhakikisha anaitendea haki kwa kuwa mbunifu na kuchapa kazi ili kufikia maono ya viongozi wakuu wa nchi ambao wamedhamiria kuliletea taifa maendeleo.
“Viongozi wetu wakuu wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wanabeba maono yenye ndoto za mafanikio, hivyo tunapaswa kutafsiri na kuziishi ndoto zao kwa matendo ili mwisho wa siku tutoe huduma bora kwa Watanzania pamoja na kutoa mchango katika maendeleo ya taifa,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Aidha, Mhe. Simbachawene ameahidi kumpa ushirikiano wa kiutendaji Mhe. Jenista Mhagama ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwataka kumsaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kuongeza kuwa, ana deni kubwa la kuitendea haki nafasi aliyopewa ili kumsaidia Mhe. Rais kutimiza malengo yake.
Mhe. Jenista amesema, kwa yeyote aliyepata heshima ya kuaminiwa na Mheshimiwa Rais kwa hakika ana kila sababu ya kuchapa kazi ili kuacha alama ya mchango alioutoa katika kufikia malengo ambayo Mheshimiwa Rais ameyakusudia.
“Ni lazima kujiwekea mkakati wa utendaji kazi ambao utajielekeza katika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa muda mfupi na mrefu pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na kuongeza kuwa nyaraka hizo muhimu ndio hasa zinahitaji uwepo wa watumishi wa umma kuzitekeleza,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama na viongozi wengine, mara baada ya kumalizika kwa hafla ya makabidhiano ya ofisi za Mawaziri hao iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) jijini Dodoma.
Sanjari na hilo, Mhe. Jenista amewataka watumishi wa umma nchini kuwa tayari kulitumikia taifa mahali popote watakapopangiwa kuwatumikia wananchi kama ambavyo yeye na Mhe. Simbachawene walivyo tayari kulitumikia taifa katika nafasi walizoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.