NA MUNIR SHEMWETA-WANMM
WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewafuturisha watumishi wake waliopo wizarani na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma.
Akizungumza wakati wa futari hiyo, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula aliwaeleza watumishi kuwa, uamuzi wa kuandaliwa futari ya pamoja unalenga kuwaweka pamoja watumishi wa wizara hususani kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwaresma.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda alishukuru uamuzi wa wizara kukutanisha pamoja watumishi kuanzia ngazi ya chini hadi juu jambo alilolieleza kuwa ni nadra sana kutokea watumishi kukutana kwa wakati mmoja kuanzia kada ya chini hadi juu.
Kamishna wa Ardhi nchini, Nathaniel Methew Nhonge akitoa neno la shukrani wakati wa futari ya pamoja ya watumishi wa Wizara ya Ardhi jijini Dodoma.(Picha na WANMM).
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anthony Sanga alihimiza watumishi wa sekta ya ardhi kuwa na umoja wakati wote wa utendaji kazi.
Hii ni mara ya kwanza kwa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuandaa futari ya pamoja ya watumishi wake tangu serikali ilipohamia rasmi mkoani Dodoma.