Wizara yathamini mchango wa TOA

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Angellah Kairuki amesema,OR-TAMISEMI inatambua jitihada mbalimbali zinazofanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA) zenye dhima ya kuimarisha ugatuaji wa madaraka kwenye ngazi ya chini ya mamlaka za Serikali za mitaa.
Waziri Mkuu,Mhe.Kassim Majaliwa akipokea Tuzo ya Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumshukuru kwa kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa wakati wa Mkutano wa 13 wa Taasisi ya Maboresho katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA).

Mheshimiwa Kairuki ameyasema hayo Aprili 4, 2023 jijini Dodoma wakati akimkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa katika Mkutano Mkuu wa 13 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (TOA).

"Mheshimiwa Waziri Mkuu, nichukue pia fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu huu wa 13 wa TOA pamoja na kuwa na majukumu mengi ya Taifa.

"Ujio wako ni faraja kwetu na kiashiria cha jinsi unavyothamini mchango wa chombo hiki (TOA), katika jitihada zake za kuimarisha utawala bora wenye dira ya kuwaletea wananchi maendeleo, kama inavyojidhihirisha katika kauli mbiu yao ya mwaka huu inayosema- ”Kukuza Uwekezaji na Viwanda kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Taifa.”

Waziri Kairuki amesema, "TOA imesaidia sana katika kuboresha utendaji kwenye Mamlaka zetu za Serikali za Mitaa kupitia mafunzo na vikao mbalimbali ambapo, viongozi wamekuwa wakikutana na kujadili mambo mbalimbali."

Vile vile, amesema TOA imekuwa ikiratibu mafunzo kwa makatibu tawala wa mikoa,wakurugenzi wa halmashauri na maafisa mbalimbali wa Serikali tangu mwaka 2002.

Kairuki amesema, lengo kubwa ni kubadilishana uzoefu na Serikali ya Japan ambayo imefanikiwa kujenga mfumo imara wa Serikali za Mitaa.

Amesema, mafunzo hayo yamekuwa na tija kwa Taifa kwa sababu imeongeza uelewa wa namna bora ya kuimarisha uendeshaji wa Serikali za Mitaa.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alitambua mchango mkubwa wa Serikali ya Japan kwa kuwawezesha takribani watumishi 6,367 kupata mafunzo ya kubadilishana uzoefu wa namna bora ya ugatuaji wa madaraka kwenye ngazi ya msingi.

Amesema, Serikali ya Japan imeendelea kufadhili progamu hiyo tangu 2006 hadi sasa. "Tunawahakikishia kuwa uzoefu tuliopata kutoka kwao tutautumia katika kuboresha uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hapa kwetu Tanzania,"amesema Waziri Kairuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news